loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania bila tembo haiwezekani

Sensa ya tembo nchini iliyofanywa Oktoba hadi Novemba mwaka jana, katika maeneo ya mfumo wa Ikolojia wa Selous-Mikumi na Ruaha-Rungwa unaonesha tembo wamezidi kupungua. Katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha-Rungwa sensa ya mwaka 1990 ilionesha kuna tembo 11,712 na baada ya vita dhidi ya ujangili kushamiri idadi hiyo iliongezeka na kufika tembo 35,461 mwaka 2006.

Lakini wimbi la ujangili liliibuka tena na kusababisha idadi hiyo kupungua na kubaki tembo 20,090 hivi sasa, hivyo kufanya jumla ya tembo katika mifumo hiyo miwili ya ikolojia kubaki tembo 33,174 pekee.

Akitoa matokeo ya sensa hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu anasema mwaka 1976 katika mfumo wa Ikolojia wa Selous-Mikumi kulikuwa na tembo 109,419. Hata hivyo, idadi hiyo ilipungua hadi kufika 22,208 mwaka 1991 na kupungua huko kunatokana na wimbi la ujangili unaofanywa dhidi ya wanyama kwa kutoa meno yao.

Kwa mujibu wa Mtaalamu kutoka Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa), Steven Kisamo, mahitaji ya meno ya wanyama hao katika soko la dunia ni makubwa na kwamba yanauzwa kwa bei kubwa. Hali hiyo ndiyo hufanya majangili hutumia nafasi hiyo kuwawinda na kuwaua ili kuchukua meno hayo.

Anabainisha kuwa masoko ya meno hayo yapo zaidi kwenye nchi za Magharibi, Asia na kwingineko duniani na kwamba bei ya meno hayo kwa kilo moja imeongezeka kutoka dola za Marekani 100 miaka ya 1990 hadi kufikia dola za Marekani kati ya 1,200 na 1,500 kwa bei ya sasa.

Na kwa kuwa biashara ya nyara hizo ni haramu, wanaozifanya ni watu wenye pesa na hufanya kwa siri kwa kuwa wanafahamu sio halali na wanapata faida nono, jambo ambalo kwa upande wa pili linamaliza wanyama hao adimu na wakubwa waliobaki duniani.

Nchini Japan meno ya tembo inasemekana hutengeneza vifaa muhimu kama vile mihuri, mapambo, vifaa vya muziki na upande mwingine ni suala la kiimani kwamba bidhaa iliyotengenezwa na meno ya tembo inaleta bahati.

Waziri Nyalandu akizungumzia ukubwa wa tatizo kuhusu tembo anasema juhudi za nchi na zile za kimataifa za kudhibiti kutoweka wa wanyama walio kwenye hatari duniani, zilifanywa ambapo biashara ya meno ya tembo ilipigwa marufuku.

Hatua hiyo ikafanya ujangili kupungua na kwamba waliofanya biashara hiyo haramu waliifanya kwa kificho na hivyo bei ya meno hayo yakapanda thamani kwa kuwa upatikanaji wake ulikuwa mgumu.

Wakati dunia ikipiga vita biashara hiyo, nchini Tanzania pia operesheni Uhai ilifanywa mwaka 1989 hadi 1990 jambo hilo likaleta matumaini ambapo idadi ya tembo iliongezeka kutoka tembo 22,208 mwaka 1991 hadi kufika tembo 70,406 mwaka 2006. Idadi hiyo ni katika Ikolojia ya Selous –Mikumi na kwa upande wa ikolojia ya Ruaha –Rungwa idadi iliongezeka kutoka tembo 11,712 hadi kufika tembo 35,461 mwaka 2006.

Lakini kutokana na wimbi ya ujangili lililoibuka tena miaka ya hivi karibuni limesababisha idadi ya tembo hao kupungua na kutishia uwepo wao kwani hivi sasa wamebaki jumla ya tembo 33,174 pekee katika ikolojia zote mbili. Nyalandu akifafanua anasema kwa ikolojia ya Selous-Mikumi tembo wamepungua kwa asilimia 66, ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009 ambapo kulikuwa na tembo 38,975.

Kadhalika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha-Rungwa tembo wamepungua kwa asilimia 36.5 ikilinganishwa na idadi ya tembo hao mwaka 2009 ambapo walikuwa tembo 31,625. Katika sensa hiyo iliyofanywa kwa ushirikiano wa serikali pamoja na wadau wengine wa nje ya nchi, umebaini kuwa vifo vingi vya tembo havikutokana na vifo vya asili ya wanyama hao bali ni vya kuuawa na kunyofolewa meno yao.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba katika sensa hiyo walithibitisha kuwepo na idadi ya mizoga ya tembo 6,516 katika ikolojia ya Selous-Mikumi na mizoga 3,496 katika Ikolojia ya Ruaha-Rungwa.

Na kwamba vifo vingi vya tembo hao havikutokana na vifo vya asili bali ni vya kuuawa na kwamba asilimia 95 ya mizoga ya tembo katika ikolojia ya Selous-Mikumi ni ya zaidi ya miezi 18 iliyopita.

Kufuatia hali hiyo, Wizara imesema operesheni tokemeza ujangili awamu ya pili itaanza tena, ili kuhakikisha wanyama hao adimu wanasalimika na kuifanya Tanzania kuwa mahali salama pa tembo, kwani Tanzania bila tembo haiwezekani.

Kukamatwa kwa meno ya tembo yenye uzito wa kilo 32,987 ndani na nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2008 hadi Septemba 2013 ni ishara tosha kuwa ujangili ni mojawapo ya sababu kubwa za kupungua kwa tembo nchini.

Kiasi hicho kikubwa cha meno ya tembo pamoja na sababu nyingine za kupungua kwa wanyama hao nchini kuliifanya Tanzania mwaka 2010 kupigwa mstari mwekundu na Jumuiya ya Kimataifa kama nchi ambayo imeathirika zaidi na ujangili na biashara ya meno ya tembo.

Hiyo ikawa sababu ya mkutano wa nchi mwanachama wa CITES, kukataa ombi la Tanzania la kutaka kuuza meno ya tembo tani takribani 90, ambazo zimehifadhiwa kwenye maghala na zinatokana na vifo vya wanyama hao vya asili.

Sababu kadhaa za kutupilia mbali ombi hilo ni kwamba kama ruhusu hiyo ingetolewa, kulikuwa na wasiwasi kuwa meno ambayo yangeuzwa si yale tu yaliyotokana na vifo vya sili kwa wakati ule bali wajanja wangepenyeza na mengine yaliyopatikana kupitia ujangili.

Sababu ya pili ni kwamba Tanzania ilikuwa ikiruhusu kupitisha kwa mizigo ya nchi ya Malawi na Zambia kwa kutumia bandari yake kusafirisha mizigo ya nchi hizo, ambapo majangili walitumia mwanya huo kupenyeza meno ya tembo.

Sababu ya tatu ni kwamba Tanzania ilikuwa haifanyi jitihada za kutosha kulinda tembo wake; hasa katika mbuga za hifadhi kama Selous. CITES iliona kwamba Tanzania ilikuwa na uwezo wa kulinda tembo wake lakini haikutekeleza jukumu hilo kwa dhati na hivyo kusababisha ujangili kushamiri. Hata hivyo, serikali kwa kuona ukubwa wa tatizo iliendesha Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo ilisaidia kupunguza ujangili katika hifadhi mbalimbali.

Hata hivyo, operesheni hiyo imesitishwa kutokana na watendaji kukiuka maadili na itaaza tena kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa wanyama hao. Tembo ni mnyama mkubwa mwenye uwezo wa kula hadi kilo 270, za nyasi kwa siku na kunywa hadi lita 200 za maji mara moja.

Ni aina ya wanyama wakubwa wa kale waliobaki duniani hivi leo. Hivyo wanahitaji ulinzi mkubwa kutokana na meno yao mawili kuwa lulu kwa majangili ambao huwawinda na kuwaua ili kuweza kung’oa meno hayo.

Licha ya ukubwa wake, huku akikadiriwa kuwa na uzito wa kufikia hadi tani nane na urefu wa hadi futi 13, wanyama hao wanaonewa zaidi na majangili wasio na huruma, ambao wakati mwingine hutumia risasi za kivita kuwaua kutokana na ukubwa wao.

Tembo ni kivutio kimojawapo kinachopendwa na watalii ambao huzuru hifadhi mbalimbali za Tanzania kama vile, Ngorongoro, Selous, Tarangire, Mikumi, Ruaha na nyinginezo kuona uzuri wa wanyama hao na wengine wengi.

Shime Watanzania, ni jukumu la kila mmoja wetu kuona thamani ya kulinda rasilimali adimu ya tembo ambao wamebaki kidogo, tuwalinde wasitoweke kwa manufaa ya majangili ambao wanawawinda na kuwaua bila huruma.

Tufahamu kwamba Tanzania bila tembo haiwezekani. Wakitoweka, mbali na kunyima vizazi urithi muhimu, mapato yetu ya utalii yatapungua pia. Sote tuna wajibu wa kuwa walinzi wa rasilimali zetu!

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi