loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Tanzania kusuluhisha mgororo Sudan Kusini

Uamuzi huo umetangazwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye hata hivyo amesema usuluhishi huo utakuwa wa kichama na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kitaongoza usuluhishi huo katika mazungumzo yatakayofanyika Arusha.

Rais Kikwete alisema jitihada hizo za Tanzania hazitaingilia mazungumzo ya kujaribu kusimamisha mapigano nchini humo yanayoendelea huko Addis Ababa, Ethiopia.

Alisema Mwenyekiti wa SPLM, Rais Salva Kiir ndiye ambaye ameiomba Tanzania kusaidia jitihada za kisiasa za kupatanisha pande ambazo zinavutana na kutofautiana ndani ya chama hicho.

Alisema anaamini kuwa mapatano ndani ya chama, yatafanikisha kumaliza mgogoro wa kisiasa katika serikali ya nchi hiyo ambayo imegawanyika na kusababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Kikwete alitangaza jitihada hizo za upatanishi za Tanzania wakati alipohutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi na kupitia kwao taifa kwenye sherehe ya kuzima Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Kilele cha Wiki ya Vijana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Alisema Tanzania imekubali kusaidia ndugu zao wa Sudan Kusini kwa nia ya kutimiza wajibu wake wa kimataifa na kwa kuongozwa na kaulimbiu ya Oktoba mwaka 1959 ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliitoa wakati Tanganyika bado ikidai uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. Rais Kikwete alikariri kaulimbiu hiyo maarufu:

“Sisi Watu wa Tanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambako hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”

“Nchi yetu ina uhusiano wake na watu wengine duniani hasa wanyonge, wenye dhiki na wasiokuwa na amani. Dhamira hii ya Mwalimu na nchi yetu ilitimizwa Desemba 9, 1961, siku Tanganyika ilipopata Uhuru ambako Bendera ya Taifa huru la Tanganyika na Mwenge wa Uhuru vilipandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro na Mwenge kuwashwa,” alisema.

Alisema tangu wakati huo mpaka sasa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kumulika nchi nzima ukipita katika mitaa, vijiji, shehia na majimbo, wilaya na mikoa ukieneza ujumbe wa udugu, umoja, upendo, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi