loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania kuvuna nini Jumuiya ya Madola?

Mwandishi Wetu COSMAS MLEKANI anaeleza zaidi kuhusu maandalizi hayo:

HUKO nyuma Tanzania ilikuwa ikitamba katika Michezo ya Jumuiya ya Madola na wachezaji wake kurejea na medali za aina tofauti kutoka katika michezo hiyo ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne.

Kwa miaka mingi Tanzania ilikuwa ikifanya vizuri, hasa kwa upande wa michezo ya riadha na ngumi, ambapo wachezaji wake walikuwa wakirejea na medali za aina tofauti kutokana na michezo hiyo mikubwa.

Waliofanya vizuri:

Kuna mifano mingi mizuri ya wachezaji wetu kufanya vizuri mfano, akina Filbert Bayi na Gidamis Shahanga ni baadhi ya Watanzania walioweka rekodi za aina yake katika michezo hiyo. Tukianza na Bayi, alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 alipoibuka wa kwanza na kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Christchurch, New Zealand mwaka 1975.

Bayi alivunja rekodi ya mbio hizo iliyokuwa inashikiliwa na Jim Ryun na kudumu na rekodi hiyo ya dunia kwa takribani miaka mitano, huku akidumu na ile ya Jumuiya ya Madola kwa miaka 40. Mbali na rekodi nyingine ya dunia kama ile ya maili moja, Bayi ndiye anayeshikilia rekodi ya mita 1500 ya Jumuiya ya Madola, ambayo haijavunjwa hadi sasa.

Kwa upande wa Shahanga, alifanya maajabu pale alipotwaa medali ya dhahabu katika mbio za marathoni katika Michezo ya jumuiya ya Madola iliyofanyika mwaka 1978 Edmonton, Canada. Shahanga alifanya maajabu na kuwa mwanariadha pekee wa Tanzania hadi sasa ambaye alitwaa medali ya dhahabu katika michezo miwili tofauti ya Jumuiya ya Madola alipotwaa dhahabu katika mbio za mita 10,000.

Michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola ilifanyika Brisbane, Australia mwaka 1982 na kumfanya Shahanga kuwa mwanariadha wa Tanzania mwenye sifa ya pekee kwa kutwaa mara mbili medali ya dhahabu katika michezo tofauti ya Jumuiya ya Madola.

Wengine waliotamba:

Mbali na akina Bayi kuna wanariadha na wachezaji wengine kama wale wa ngumi waliowahi kutamba hadi kutwaa medali za dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Kwa upande wa wanariadha wengine ni kama akina Francis Naali, Samson Ramadhani, Simon Mrashani, Geyway Suja na wengineo ambao walirudi na medali na wengine kupandishwa vyeo na waajiri wao baada ya kufanya vizuri katika michezo hiyo.

Mwaka 1990, mwanariadha Simon Robert ambaye sasa ni marehemu alitwaa medali ya shaba katika mchezo wa marathoni katika michezo iliyofanyika Auckland, Zew Zealand huku michezo iliyofuata bondia Hassan Matumla aliitoa nchi kimasomaso baada ya kuibuka na medali ya dhahabu katika michezo iliyofanyika Vancouver, Canada.

Katika michezo iliyofanyika Kuala Lumpur, Malaysia mwaka 1998, bondia Michael Yomba Yomba alirudi na medali ya dhahabu huku wanariadha Simon Mrashani na Gerway Suja walishinda medali ya fedha na shaba katika mbio za marathoni. Francis Naali alipata medali ya dhahabu katika marathoni katika michezo iliyofanyika Melbourne, Australia mwaka 2002 pamoja na John Yuda ambaye naye alipata medali ya shaba.

Wengine katika ngumi waliofanya vizuri ni Matumla, Willy Isangula na Titus Simba (sasa ni marehemu). Hakuna ubishi kuwa kizazi hicho cha kufanya vizuri sio kwa upande wa riadha hata ngumi, hakipo tena na badala yake wachezaji wetu wamekuwa wakienda kushiriki tu na wala sio kushindana.

Miaka ya hivi karibuni:

Katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imerejea mikono mitupu, ambapo kwa mara ya mwisho Ramadhani ndiye aliyerudi na medali ya dhahabu ya marathoni mwaka 2006 katika michezo iliyofanyika Melbourne, Australia. Huyo ndiye mwanamichezo wa mwisho wa Tanzania kutamba katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola kwani mwaka 2010 katika michezo ya New Delhi, India, Tanzania ilirudi mikono mitupu sio kwa ngumi wala riadha.

Huenda rekodi hiyo mbovu ndio iliyomvuta au kumshawishi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe kuwatafutia kambi nje ya nchi wachezaji wetu wa riadha na ngumi ili angalau wanolewe vizuri na kuwawezesha kurudi na medali. Wanariadha wanatarajia kwenda kupiga kambi katika nchi za Ethiopia, Afrika Kusini na Uturuki wakati mabondia watakwenda Uturuki na China kwa ajili ya kujinoa kwa michezo hiyo.

Kwa mujibu wa makamu mwenyekiti wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Lukelo Willilo, tayari mabondia 16 wamechaguliwa kuanza mazoezi katika timu ya taifa kabla ya kuchujwa na kubaki 12, ambao sita watakwenda Uturuki na wengine kama hao watapiga kambi China.

Kutumia vizuri kambi:

Timu za ngumi na riadha mmepata ofa ya kwenda kujifua nje ya nchi na huko sio wachezaji tu watakaofaidika na kambi hizo, ila hata makocha wao ambao watakwenda kujifunza kitu kipya. Hata hivyo, pamoja na kupewa kambi hizo na viongozi wa BFT pamoja na Riadha Tanzania (RT) kufurahia faida watakayopata kutoka katika kambi hizo, nawaasa kuwa makini na kuzitumia vizuri kambi hizo.

Ni matarajio yangu kuwa vyama vya michezo vitazitumia vizuri kambi hizo ili kuwafanya wachezaji wenu kurudi nchini na medali badala ya kuitwa watalii kutokana na kurudi na mabeki makubwa yaliyojaa nguo na viatu. Imekuwa kawaida kwa viongozi wa vyama au mashirikisho ya michezo kutumia vibaya fursa kama hizo, ambapo badala ya kupeleka wachezaji wenye uwezo wanaostahili kuitwa katika timu ya taifa, wanawapeleka jamaa zao.

Kwa upande wa ngumi, tayari kumekuwa na kasoro zilizoanza kujitokeza baada ya BFT kuchagua mabondia wasio na uzoefu katika mchezo huo wa ndondi na kuwaacha wengi wenye uzoefu. BFT wenyewe wanadai kuwa mabondia wengi wenye uzoefu walioachwa waliachwa sababu ya utovu wa nidhamu hasa baada ya kutoshiriki katika mashindano ya wazi yaliyoandaliwa na DABA.

Mabondia hao walishindwa kuhudhuria mashindano hayo ya DABA baada ya kuhudhuria yale ya mkoa, ambayo yalifana ukilinganisha na yale ya BFT yaliyofanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Dar es Salaam.

SEPTEMBA 16 ya kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi