loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tatizo wabunge wetu hawaaminiani

Wajumbe wetu katika Bunge hilo sio wamoja hata kidogo na bahati mbaya sio wamoja katika suala la kuandika Katiba mpya, ambayo ni chombo cha wananchi wote hata wale ambao sio wanachama wa vyama vya siasa.

Hilo wabunge wetu hawalioni hata kidogo.

Kwa mgawanyiko huu ndio maana naingiwa na wasiwasi kama Katiba mpya itaweza kuandikwa na hao wabunge wetu.

Pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa na tume ya marekebisho ya katiba, naona kama kazi hiyo itakuwa ni ndoto maana katika mvutano wa namna hiyo sioni mwanga kama wajumbe wa bunge hilo wanaweza kukaa pamoja na kuwa kitu kimoja.

Sioni kama wanaweza kuridhiana maana katika ibara hizo mbili tu mambo kwao sio muafaka hata kidogo, wanalumbana na hata kuaminiana hawaaminiani hata kidogo.

Kutokana na kutoaminiana imefikia hatua hata wanazomeana hadharani. Hebu fikiria wabunge wetu wanapofikia hatua ya kuzomeana kweli hapo kuna maridhiano yatakayofikiwa. Naona giza jamani!

Na kinachoniuma zaidi ni mamilioni ya walipa kodi yanavyotoketea lakini hakuna hata ibara moja ambayo imepata muafaka, licha ya Bunge lenyewe kubakiwa na wiki mbili liweze kumalizika.

Wabunge wetu jamani tuoneane huruma, wekeni pembeni itikadi zenu jifungieni ili mpate maridhiano kwa mambo ambayo mnaona ndio njia pekee ya kuweza kuandika katiba mpya. Hivi vyama hivi mnavyoshabikia mmezaliwa navyo?

Nani alizaliwa kati yenu akajikuta ni Chadema, CUF au ni CCM. Wote si mmejiunga navyo tu ukubwani na kuamua kufuata hiyo itikadi. Lakini nyie wote mlioko ndani ya mjengo mmezaliwa Tanzania na mtakufa mtaiacha Tanzania itaendelea kusimama.

Sasa kwa kutambua hilo kwa nini msiingiwe na uzalendo hadi angalau mkaonea huruma pesa za walipa kodi?

Tunajua mlichagua kuanza na hilo gumu ili huko mbele mambo yaende vizuri, sawa ulikuwa ni uamuzi mzuri sasa tunaomba basi kila upande uone umuhimu wa kufikiwa muafaka wa ibara hizo mnazogombania.

Wajumbe 600 akili tofauti ndani ya siku takribani miezi miwili mambo yamekuwa magumu kiasi hicho, lakini naamini mkiacha ushabiki na kuamua kwenda na maslahi ya taifa hili naamini mtatupatia katiba nzuri zaidi.

Hizi sala ambazo mnaombewa na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini, hebu ziwaingie nyie wajumbe ili mlionee huruma taifa letu. Hatutaki kuingia kwenye machafuko ya aina yoyote ile ndio maana tukawatuma huko mje na katiba nzuri.

Sasa wenyewe angalieni katiba nzuri ni ipi, serikali mbili, tatu au moja. Kazi mnayo nyinyi lakini kwa kuangalia Tanzania ya miaka 50 ijayo.

Ninavyowaangalia kwenye runinga na ushabiki wenu huo mnajidanganya kama mtakuwa na maridhiano wakati wa kupiga kura.

Hizo theluthi mbili mnazozitafuta kila upande kwenu itakuwa ni shida kama hamtakuwa na maridhiano. Hakuna ubabe wala umaarufu ndani ya hilo bunge, kinachotakiwa ni kunyenyekea na kukubali kupata na kukosa.'

Give and Take' na baadaye mtapata 'win win situation' katika hilo nani atamlalamikia mwingine.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Shadrack Sagati

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi