loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Teknolojia ya Uhandisi Jeni inafaa mazingira ya Afrika

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Hassan Mshinda, amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wa kila mwezi wa kutathmini sayansi na teknolojia nchini kwamba usalama kwa afya na mazingira wa GMO, unalifanya suala la teknolojia ya uhandisi jeni kuwa si la kujadiliana tena.

Dk Mshinda anasema nchi yetu, inatakiwa kufanya kampeni kubwa ya kuondoa au kufuta kanuni ambazo zimetengenezwa katika mtazamo wa nchi za Ulaya, ambazo hazijafanya utafiti kuhusu uzuri au ubaya wa GMO, lakini zinatakiwa kufuata mtazamo wa Marekani, ambayo haiweki vigingi wa matumizi ya teknolojia hiyo nchini.

Anasema nchi inatakiwa kuachana na kanuni zinazohusianisha GMO na athari za mazingira, ambaao zinachangia nchi kubaki nyuma kutokana na kutotumia teknolojia hiyo inayoboresha mazao na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Nchi za Ulaya zimekuwa zikitumia teknolojia ya uhandisi jeni katika masuala ya afya, isipokuwa hawajafanya utafiti katika masuala ya kilimo cha mahindi, pamba na soya na mazao mengine na ndio maana hawatoi kipaumbele katika matumizi ya teknolojia hiyo.

Nchi hizo zimeacha kutunga sheria na kanuni za teknolojia ya uhandisi ya jeni, kutokana na kutotoa kipaumbele kwa teknolojia hiyo, kwani hazina uhakika nayo na hivyo hazioni umuhimu wa kutunga sheria na kanuni.

Kutokana na nchi hizo kutokuwa na kanuni na sheria kuhusu matumizi ya jeni katika kuboresha mazao kama mahindi na mtama, hazitilii maanani wala kuweka uzito, tofauti na Marekani ambayo inazalisha mahindi na ndio maana imetunga kanuni za kuruhusu mazao hayo yenye teknolojia uhandisi ya jeni kuzalishwa kwa wingi.

Bara la Afrika kwa ujumla ikiwamo Tanzania, inatakiwa kuwa na mfumo wake kulingana na mahitaji ya Kiafrika ili kupata faida inayotokana na GMO ambazo zimekuwa suluhisho la mazao na mimea ambayo imekuwa ikiharibiwa na wadudu au kukauka shambani.

Costech imekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi ya teknolojia ya GMO, hasa baada ya kuwa na uthibitisho wa kisayansi kwamba haina madhara kwa afya na mazingira yetu na hivyo inapigia debe matumizi ya teknolojia hiyo katika nyanja mbalimbali za uzalishaji ili kupata maendeleo.

Msimamo wa Costech ni kuhakikisha kwamba teknolojia hiyo ambayo imethibitika kisayansi kwamba inaweza kuleta mabadiliko makubwa bila madhara katika mazingira, afya na uchumi, ni vema ikatumika katika kuboresha mazao nchini. Kwa msingi huo, Costech licha ya kuhimiza matumizi, imekuwa tayari kufadhili miradi ya kilimo inayotumia teknolojia ya GMO.

Lengo la Tume ni kuhakikisha Watanzania kwa wingi wao wanapata maendeleo kutokana na kutumia teknolojia hiyo na kuachana na upotoshaji kwamba teknolojia hiyo haifai. Costech inathibitisha usalama wa teknolojia hiyo kutokana na kupata uthibitisho kutoka kwa nchi baadhi za Afrika ambazo zimetumia na kuleta mafanikio makubwa.

Miongoni mwa nchi hiyo ni Afrika Kusini, Misri na Burkina Faso, ambazo tangu zimeanza kutumia teknolojia hiyo, zimepata mafanikio makubwa na hakuna athari za kimazingira na kiafya. Nchi hizo zilizotumia teknolojia hiyo, hazijapata hasara kutokana na matumizi ya GMO kwa binadamu na wanyama, bali zimeongeza uzalishaji wa nafaka yakiwamo mahindi na soya.

Changamoto iliyopo ni kwa Tanzania kubadilisha kanuni na sheria au kuzitenganisha za kilimo na nyingine hasa za mazingira, ili kutunga nyingine zitakazosaidia kutumia GMO katika uzalishaji mazao ya kilimo na hivyo kuwagusa wakulima asilimia 80 ambao ni wakulima.

Kuendelea kubalika kwa kanuni zinazokwamisha matumizi ya GMO ni sawa na kuwanyima haki wakulima ambao ni wengi nchini na ndio wanaoshika uchumi na nchi kutokana na sekta hiyo kuhusisha wananchi wengi zaidi. Nchini nyingine duniani ikiwamo China, hazijasuasua katika kuanza kutumia teknolojia ya uhandisi jeni.

Taarifa zinaonesha kwamba kwa muda mfupi zimesonga mbele katika kilimo hasa katika uzalishaji wa nafaka kama mahindi na mazao ya biashara kama pamba. Nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, zinatakiwa kuiga mtindo wa China na Marekani, ambayo ni mataifa makubwa duniani katika uchumi kutokana na kutumia teknolojia hiyo ambayo imeleta mabadiliko katika kilimo na katika ubora wa mazao yanayolimwa.

Bara la Afrika lipo nyuma kutokana na kutotumia teknolojia nyingi ikiwamo ya uhandisi jeni licha ya ukweli kwamba imeonesha mafanikio katika mataifa makubwa ya Marekani na China.

Tanzania haina uhaba wa wataalamu, wakiwamo wa Kituo cha Utafiti wa Mazao, Mikocheni na wasomi wengine wanaandaliwa kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa ajili ya kuandaa mbegu hizo muhimu katika maendeleo ya kilimo nchini.

Nchi haina uhaba wa vituo vya sayansi na maabara kama ilivyokuwa mapema miaka ya 1990, hivi sasa kutokana na dunia kuwa kijiji, wanasayansi dunia nzima wanashirikiana katika kutengeneza mbegu za teknolojia hiyo, hivyo ni rahisi kwa nchi ikiazimia kutumia teknolojia hiyo ni rahisi kupata mbegu hizo.

Dk Mshinda anasema, nchi za Afrika zinatakiwa kuachana na kuiga mtindo wa taasisi za Ulaya ambazo zinatumia wanaharakati wa kitaifa na kimataifa katika kupinga matumizi ya teknolojia hiyo, bila hata kuwa na utafiti wa kisayansi isipokuwa nguvu ya ushawishi.

Nchi za Afrika zinatakiwa kuwa na uamuzi wake zenyewe kwa ajili ya maendeleo yake, bila kufuata matakwa na mitazamo ya Ulaya katika kutumia teknolojia ya uhandisi jeni. Uamuzi huo utazisaidia nchi hizo kupata maendeleo badala ya kubaki nyuma kiteknolojia.

Katika suala hili, nchi za Afrika zinaweza kuiga au kufuata mfano wa Marekani na China ambazo zimetumia teknolojia ya uhandisi jeni ambazo zimesaidia katika kuboresha mazao ambayo sasa hayaharibiwi vibaya wala hayaathiriki kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa kutumia teknolojia hii inaaminika kwamba nchi za Afrika Tanzania ikiwamo, zitapata faida ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo imesababisha uhaba wa mvua na hivyo jamii kukumbwa na njaa, lakini kwa kutumia teknolojia hiyo kutaongeza chakula, uhakika na kulima mazao yanayovumilia ukame na kuiva mapema.

Wakati umefika kwa Afrika, Tanzania ikiwamo, kuanza kutumia teknolojia ya uhandisi jeni katika kuzalisha mazao mbalimbali nchini, yakiwamo mahindi, muhogo na mazao mengine ambayo ni suluhisho katika kupambana na maradhi, kujikinga na njaa na kuwa na chakula cha uhakika.

SEKTA ya ubunifu (sanaa) na uchumi ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi