Mbali na mpango huo, pia kila shule ya msingi itatakiwa kuwa na mwalimu wa soka wenye leseni inayotambuliwa na Shirikisho hilo na Chama cha Makocha ukiwa ni mkakati wa ufundishaji soka unaokidhi viwango na mfumo ambao utakaopendekezwa kitaifa.
Alisema hayo juzi katika hotuba yake ya ufungaji wa mashindano ya soka kwa vijana yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, yaliyoandaliwa na Kituo cha Maendeleo ya Soka kwa Vijana Mkoa wa Morogoro.
Tanzania imekuwa ikikwama katika mashindano mbalimbali yakimataifa kwa vile haijawekeza kwa vijana wadogo kama zilivyo nchi nyingine duniani.
“TFF tumeliona hilo na sasa tunaandaa mpango kazi wa maendeleo ya soka kwa vijana. Tunatarajia kuuzindua rasmi Oktoba 8, mwaka huu ambapo TFF itaadhimisha miaka 50 tangu tujiunge na FIFA,” alisema Malinzi.
Alisema katika mpango wa kuendeleza soka kwa vijana, TFF itatengeneza utaratibu kwa kila shule ya msingi ipatiwe vifaa vya soka ambavyo ni mipira na viatu, na kuwa na mwalimu wenye leseni ya ukocha.
“Mipira na viatu ni vifaa muhimu katika soka. Tunahitaji mwanafunzi aweze kutumia viatu mchezoni na si kuja kuvitumia ukubwani, kwani wengi wanashindwa kumiliki mpira kutokana na hilo,” alibainisha Malinzi.
Pamoja na kusema hayo, pia alisema TFF inajipanga vyema kuendesha mashindano ya vijana wadogo wenye umri wa miaka 13 kila mwaka na mashindano hayo yataanza rasmi mwaka huu, lengo ni kuwapata watoto wenye vipaji ambavyo vitaendelezwa kwa kuwaingiza kwenye shule za taasisi za michezo.