loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Timu ya nyika iliandaliwa kibabaishaji

Awali, uongozi wa Riadha Tanzania (RT) ulisema kuwa ungepeleka jumla ya wachezaji 22, lakini ilijikuta ikipeleka idadi hiyo pungufu kutokana na kutokuwa na wanariadha wa kutosha. Pamoja na RT kupitia Katibu Mkuu wake, Suleiman Nyambui kusisitiza kuwa, timu hiyo imejiandaa vizuri baada ya kuchaguliwa kupitia mashindano ya wazi ya mbio za nyika nchini yaliyofanyika Arusha, haikuwa hivyo.

Hata hivyo, timu hiyo ambayo iliongozwa na Rais wa zamani wa RT, Francis John, haikuandaliwa vizuri kabisa, kwani hata umri wa wachezaji haukuzingatiwa. Wadau mbalimbali wa michezo na hasa wale wa riadha wamekuwa wakilalamika kuona riadha inaporomoka wakati huko nyuma Tanzania ilifanya maajabu katika mchezo huo duniani kwa wanariadha wake kutamba.

Timu ya Taifa

Timu ya Taifa ya riadha iliyoshiriki mashindano ya mbio za nyika ya Afrika nchini Uganda ilijaa vituko baada ya RT kuonekana wazi kuwa hawakujiandaa. Pamoja na kusema kuwa timu hiyo itakuwa na wachezaji karibu 22, lakini ilikuwa na wachezaji 12 tu, ambao walitakiwa kushiriki katika mbio za junior na zile za wakubwa (seniors).

Hata hivyo, Tanzania haikuingiza timu ya junior uwanjani baada ya kubainika kuwa wanariadha wa umri huo wa Tanzania walikuwa na umri mkubwa tofauti na kanuni za sheria za mchezo huo zinavyohitaji. Wachezaji hao waliotakiwa kukimbia mbio za juniors ambazo ni za kilometa sita, ilibidi kuhamishiwa katika mbio za wakubwa ambazo ni za kilometa 12.

Hivyo, kitendo cha kuwakimbiza wachezaji hao katika mbio za wakubwa wakati walijiandaa vizuri kulisababisha kufanya vibaya katika mbio hizo ambazo hawakujiandaa kushiriki, kwani zilikuwa kubwa zaidi yao. Kawaida kanuni za riadha za kimataifa zinaeleza wazi kuwa wachezaji wa juniors katika mashindano husika ni wale waliozaliwa mwaka fulani hadi tarehe 30 ya mwezi huo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui alisema kuwa hajui lolote kuhusu tatizo hilo kwani hadi sasa bado hajapata ripoti ya mashindano hayo.

“Kwa kweli mimi sijui lolote kuhusu hilo kwani bado sijapata ripoti ya mashindano hayo, bora umenikumbusha nitampigia sasa hivi Francis (John) aniletee ripoti kamili ya timu ya Tanzania,” alisema Nyambui wiki hii alipozungumza na gazeti hili na ambaye hajui hata timu hiyo ilishika nafasi ya ngapi kwa kuwa bado hajapata taarifa kwa kiongozi huyo wa msafara.

Lakini Nyambui anakiri kuwa ni kitendo kibaya kwa wadogo ambao walijiandaa kukimbia mbio za kilometa sita na baadaye walikimbia kilometa nane kwa upande wa wanawake kwani kuliwakosesha ushindi. “Ni kweli pamoja na kuwa na tofauti ya kilometa mbili lakini sio vizuri kwa juniors wanawake waliotakiwa kikimbia mbio za kilometa sita kukimbia kilometa nane,” anasema Nyambui katika mazungumzo hayo.

Viongozi wa timu:

Timu hiyo ilikuwa na viongozi watatu ikiongozwa na Rais wa zamani wa RT, Francis John wakati viongozi wengine ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT, John Bayo na Katibu Msaidizi wa Chama cha Riadha cha Zanzibar (ZAAA), Mlingi Bwire.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa wachezaji wa kike, lakini timu hiyo haikuwa na matroni, kitu ambacho sio cha kawaida na ni hatari kwa timu yenye wanawake kukosa matron. Katibu Mkuu wa RT, Nyambui akizungumza madai hayo anasema kuwa, RT haikuwa na fedha hivyo ilibidi kupeleka viongozi wachache.

Taarifa zingine zinathibitisha kuwa viongozi wa timu hiyo iliyokwenda Uganda kwa basi, walijigharamia wenyewe kwa fedha zao za mfukoni. Wachezaji wa timu hiyo kila mmoja alipewa kiasi cha Sh 20,000 ikiwa ni posho wakati wa safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda huku wakati wa kurudi kila mmoja alipewa Sh 30,000 na hivyo kufanya posho aliyopewa kila mchezaji kuwa jumla ya Sh 50,000.

Maandalizi ya Zimamoto:

Kiujumla maandalizi ya timu ya Tanzania iliyoshiriki mashindano hayo ya mbio za nyika ya Afrika, iliandaliwa kizimamoto na ndio maana haikufanya vizuri. Pamoja na RT kuwa na taarifa ya muda mrefu kuhusu mashindano hayo, lakini bado walishindwa kuichagua na kuipa maandalizi ya mapema kwa ajili ya mashindano hayo.

Mbali na kuchelewa kuichagua, timu hiyo pia haikuandaliwa vizuri kiasi cha kufanya hata kukosa idadi ya wachezaji iliyotarajiwa awali na hivyo kuvunja baadhi ya timu na kubaki na chache.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi