loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Timu ya Tanzanite isaidiwe kufikia malengo

Ni timu ya vijana wadogo yenye vipaji vikubwa ambavyo vikiendelezwa kwa umakini na kusaidiwa wanaweza kutumika katika timu ya Taifa ya Wanawake, ‘Twiga Stars’. Timu hiyo imetokana na vipaji vilivyoibuliwa Airtel Rising Star, ambapo kwa mwaka huu kulikuwa na timu za wanawake tofauti na miaka iliyopita ambapo timu za wanaume ndizo zilizopewa kipaumbele zaidi.

Kocha wa timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars,’ Rogasian Kaijage aliwapata vijana chipukizi 34 na kuwapeleka kambini ili kuwachuja na kupata 25 ambao watagawanywa kwenye mafungu matatu. Kwa mujibu wa Kaijage, uteuzi huo ulizingatia nyota chipukizi wenye vipaji ambao watakuwa chachu na nguzo kwa soka la wanawake miaka kadhaa ijayo kwa kuwa na timu imara ya vijana na ile ya Twiga Stars.

Kaijage alisema programu yake aliigawa sehemu tatu kuanzia mwaka 2013/14; 2013/ 15 na nyingine kuanzia mwaka 2015 na kuendelea. Anasema kwa vile vijana wengi bado ni wapya wanaandaliwa sio kwa ajili ya kushinda katika mchezo uliopita au sasa, bali kwa ajili ya kusaidia kwenye Twiga Stars, haijalishi kwamba wangefungwa mabao mangapi.

Anasema ni vipaji vipya ambavyo vinatengenezwa na vinaweza kuja kuwa msaada mkubwa baadaye ikiwa tu vitaungwa mkono na Watanzania katika kuendelezwa na kupewa mafunzo ya kutosha kwa manufaa ya baadaye. Soka la wanawake kwa ujumla ukianzia Twiga Stars na hiyo mpya ya vijana, haina ufadhili wowote mpaka sasa.

Sio kwamba uongozi uliopita ulikuwa hautafuti udhamini, walikuwa wakizungumzia ingawa ilionekana kugonga mwamba. Kutokana na changamoto hiyo, Rais mstaafu wa TFF Leodegar Tenga alizungumzia umuhimu wa timu ya Tanzanite ilivyo na thamani kubwa ikiwa itaungwa mkono kwa ajili ya kuendelezwa.

Anasema: “Ili timu yetu ya Tanzanite iweze kufanya vizuri na hatimaye kufanikiwa kufuzu mashindano ya vijana ya Kombe la Dunia, inahitaji msaada kutoka kwa wadau, na ndipo watafanikiwa.” Ili kufanya maandalizi ya kutosha wanahitajika kukaa kambini kufuliwa wakati huo kuna mahitaji muhimu kwao kama watoto wa kike, chakula na mengine, lakini je, watafanikiwaje ili kutimiza kile wanachokikusudia kama sio wadau?

Bado vijana wana safari ndefu mbele hawajachelewa kuna timu nyingine zinakuja mbele watahitaji tena kuwa kambini, wadau wanatakiwa kujitokeza kuisaidia kujiandaa mapema. Hiyo ni changamoto kwa uongozi mpya wa TFF chini ya Rais mpya, Jamal Malinzi na wenzake kuangalia ni kwa vipi wataisaidia timu hiyo kupata msaada kutoka kwa wadau wa soka ili kuendelea kufanya vizuri na kucheza kwa kujiamini pindi wanapokuwa uwanjani.

Katika ahadi zao nyingi walizotoa, ni uwekezaji wa soka kwa wanawake, vijana na watoto. Hiyo yote ni kwa sababu waligundua kuwepo kwa upungufu mwingi ikiwa hilo la kukosa wadhamini. Sasa matarajio na mategemeo ya wengi ni kushuhudia utekelezaji wa kweli unafanyika kwa vitendo zaidi kuliko siasa.

Pia ni imani kuwa ukweli wa yale yaliyozungumzwa yataanza kuonekana kuanzia kwenye timu ya Tanzanite ambayo inajiandaa kutafuta nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia.

Ujio wa wadhamini utatokana na jinsi timu hiyo itakavyopewa kipaumbele na uongozi huo, watakavyohamasisha wengine kuunga mkono kwa sababu sio kweli kwamba wanaweza peke yao, bila kuonesha jitihada nyingine za kutafuta wadhamini kama ambavyo wale waliopita walivyofanikiwa kupata udhamini katika timu nyingine.

Kama inavyofahamika soka ni mchezo wa kibiashara, wadhamini wana nafasi ya kutumia fursa hiyo kwa vile bado timu yenyewe iko safarini kuendelea kutafuta nafasi hiyo kubwa, huenda wakafanikiwa kutokana na matokeo mazuri waliyoanza kuonesha.

Kama ambavyo tumeshuhudia mafanikio ya wadhamini kwenye timu ya Taifa ya wanaume na hata klabu kubwa, vile vile, ni matarajio ya wengi kuona kuwa timu zote za wanawake zinatafutiwa nafasi kwa lengo la kufanya vizuri zaidi.

Ni wazi kwamba hata wachezaji watakapoona wanathaminiwa wataonesha moyo katika kufanya juhudi wakati huu au wakati ujao watakapohitajika kwenye kikosi kikubwa au kidogo. Sio vyema kusikia mambo mabaya ambayo tulipata kuyasikia mwaka jana kwamba wanawake wanajihusisha na vitendo viovu, kashfa ambayo inawaathiri wachezaji kisaikolojia.

Hayo ni baadhi, kuna suala la ushabiki wa Watanzania uwanjani. Wiki iliyopita kilitangazwa kiiingilio kidogo ili tu kuwezesha wananchi wengi kwenda uwanjani na kushabikia. Ili soka letu likue ni muhimu kuweka kando suala la ubaguzi kwa kuchagua ni timu gani ya kwenda kuishangilia.

Tanzanite ni timu ndogo inahitaji mashabiki wa aina zote, kama ilivyo kwa wanaume ambapo tumeona wanawake wengi wakienda uwanjani kushangilia Simba na Yanga. Timu hiyo itaonesha uwezo wake ikiwa watu watakuwa wakijitokeza kwa wingi na kuchangia kiingilio kitakachowawezesha kupata mgawo mzuri baadaye.

Kuna haja kubwa ya kujenga utamaduni kuishangilia kila timu ya Tanzania, sio tu pale inapoonesha matokeo mazuri hata kama ikishindwa wapewe moyo ili wawe na morali ya kufanya vizuri wakati ujao. Tujifunze kimataifa wanavyofanya, wana mapenzi ya dhati kwa timu na klabu zao ndio maana ukiangalia kila michezo inajaza watu.

Hata nyumbani inawezekana, tuisaidie Tanzanite ije na mbinu za kufanya vizuri zaidi wakati ujao ili hatimaye watimize malengo ya kucheza Kombe la Dunia nchini Canada mwakani.

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi