loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tuache kutoa holela taarifa zetu za benki

Hali hiyo imebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei wiki iliyopita. Kimei alisema wameibuka matapeli katika baadhi ya mitandao ya kijamii, ambao wamekuwa wakilaghai wananchi, wakiwataka kutoa taarifa zao muhimu za akaunti za benki, jambo linalohatarisha usalama wa fedha zao, zilizohifadhiwa katika benki.

Kimei alisema hayo jijini Dar es Salaam katika mkutano uliohusu uboreshwaji wa huduma za benki kupitia simu za mikononi, yaani 'sim banking' na njia za wateja kujilinda na uhalifu kwa njia ya mtandao. Kimei alisisitiza kuwa huduma ya sim banking ni salama na imepitia viwango vyote vya kiusalama.

Tunamuunga mkono Kimei, kwanza kwa kuelimisha umma wa Watanzania kuwa kumezuka kundi la waovu hao (matapeli), ambao wamekuwa wakiwaibia Watanzania.

Elimu juu ya kuwepo kwa tatizo fulani ni jambo muhimu kwa jamii yoyote ile. Hivyo, taarifa hiyo ya Kimei itawasaidia wananchi wengi wa mijini na vijijini, ambao baadhi yao wameshalizwa na watu hao hatari kupitia mitandao ya kijamii.

Mbali na elimu, jambo lingine alilosema Kimei ni kuwasisitiza wateja kutunza vizuri taarifa za akaunti zao, ikiwemo kadi zao na namba za siri ili kujiepusha na matapeli hao. Kinachotakiwa ni wananchi na wateja wote wa benki, tutekeleze mwito huo wa Kimei. Tuwe makini na kundi hilo la matapeli.

Tusidanganyike. Tuache kutoa taarifa zinazohusu nyaraka zetu zilizopo benki. Tusitoe taarifa hizo, hata kwa wafanyakazi wa benki. Matapeli wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kufanya uhalifu huo.

Mkurugenzi wa Idara Hatarishi ya benki hiyo ya CRDB, James Mabula anatoa mfano kuwa matapeli hao, huwapigia simu wateja, wakijifanya kuwa wakurugenzi ama wafanyakazi wa benki hiyo na kisha huwadanganya kwa kutaka wawapatie namba za siri za akaunti zao.

Mabula anashauri kuwa njia kubwa ya kujikinga na matapeli hao ni kwa kila mteja, kuacha kutoa taarifa ya namba ya siri ya akaunti yake kwa mtu yeyote na kutunza vizuri kadi ya benki.

Ni vema pia wananchi na wateja wa benki, kuacha kutumia namba za siri ambazo ni rahisi kutambuliwa na matapeli, kama vile mwaka ambao mtu alizaliwa, na namba zinazofanana. Tukumbuke kuwa usalama wa jambo lolote lile, huanzia kwa mtu binafsi.

Tusisubiri vyombo vya dola, kama vile Jeshi la Polisi, kupambana na uhalifu huo. Kila mmoja wetu, achukue tahadhari inayotakiwa, ikiwemo kutotoa holela taarifa zetu za benki.

FUKUTO la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani linazidi ...

foto
Mwandishi: mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi