loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tuisaidie jamii kushiriki uchaguzi

Utafiti huo wa awali umefanywa kwa lengo la kusaidia ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mchakato wa uchaguzi, uongozi na uteuzi.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, yaliyotangazwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Alexander Makulilo, vijana ndio wanaotumiwa kufanya vurugu katika uchaguzi, lakini waathirika wakubwa ni wanawake na watu wenye ulemavu.

Mbali ya sababu hiyo, utafiti huo pia umebaini kuwa sababu nyingine ya ushiriki mdogo wa wanawake na wenye ulemavu kwenye uchaguzi ni mfumo wa uchaguzi unaotaja mshindi ni aliyepata kura nyingi, hivyo kutaka uchaguzi wa uwakilishi.

Pia, daftari la kudumu la wapiga kura limedaiwa kuwanyima haki baadhi ya vijana waliofikia umri wa kushiriki kwenye uchaguzi, kutokana na mfumo wa kuboresha daftari hilo kufanyika kwa muda fulani.

Kwetu sisi kama chombo cha habari chenye jukumu la kusaidia kukuza demokrasia na elimu ya uraia, tumeona si vizuri matokeo haya ya utafiti yakapita bila kuungwa mkono, kutokana na ukweli kwamba idadi ya wanawake na watu wenye ulemavu kwenye uchaguzi, imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka.

Ni ukweli usio na shaka kwamba sababu zilizotajwa katika utafiti huo ndiyo sababu ambazo zimekuwa zikidaiwa kwa muda mrefu kuwa kiini cha kuzuia idadi kubwa ya wapiga kura kujitokeza kwenye uchaguzi.

Wakati ambapo awali sababu hizi zilikuwa zinatajwa bila ya kuwepo kwa utafiti wowote wa kitaalamu, safari hii, utafiti huu wa TCD umeweka bayana kwamba ni kweli wanawake na watu wenye ulemavu wamekuwa wakishindwa kushiriki kwenye uchaguzi, kutokana na sababu zilizoainishwa.

Hivyo basi pamoja na kuunga mkono matokeo ya utafiti huu, ni imani yetu kwamba pamoja na kueleza nini tatizo, mamlaka husika ikiwemo TCD yenyewe watatumia matokeo hayo, kutafuta mbinu au njia za kuweza kukabiliana na changamoto zilizotajwa kwa lengo la kubadili hali hiyo ili kuongeza idadi ya wapiga kura.

Suala la idadi ya wapiga kura kupungua mwaka hadi mwaka, si tu kwamba limekuwa likiwahusu wanawake na wenye ulemavu pekee, bali limekuwa likiihusu jamii nzima ya Watanzania, kwani takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wapiga kura katika uchaguzi mdogo na uchaguzi mkuu, imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka.

Inawezekana kwamba sababu zilizotajwa kuwa ndio chimbuko la wanawake na wenye ulemavu, kushindwa kujitokeza kupiga kura, ikiwemo vurugu zinazodaiwa kufanywa na vijana, ndizo pia zinachangia kuyafanya makundi mengine ya kijamii kushindwa kujitokeza kwenye uchaguzi, na kama hali ni hiyo basi tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi.

Ni kutokana na dhana hiyo, ndio maana tunazishauri mamlaka zinazohusu ukuzaji wa demokrasia na elimu ya uraia, kuutumia utafiti huu katika kukabiliana na tatizo hilo ili ikiwezekana kuanzia uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani, tuweze kushuhudia idadi kubwa ya wananchi wakijiandikisha na wakijitokeza kupiga kura, tofauti na ilivyo sasa.

Vinginevyo kama hili halitafanyika, bila shaka matokeo ya utafiti huo hayatakuwa na manufaa yoyote kwa wananchi, na Watanzania wataendelea kushuhudia uwepo wa wapiga kura wachache kwenye uchaguzi, suala ambalo ni la hatari katika nchi inayoheshimu utawala bora na ukuaji wa demokrasia kama Tanzania.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi