loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tujitayarishe kwa uchaguzi wa serikali za mitaa

Ni miezi mitatu tu imesalia kufikia muda huo, hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya ili kufanikisha suala hilo nyeti. Mojawapo ya mambo yanayotakiwa kufanywa ni kuhamasisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika uchaguzi huo muhimu.

Kushiriki kwa wananchi kwa wingi, kutatuwezesha kupata viongozi bora na makini, watakaohimiza maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Farida Mgomi tayari ametoa mwito kwa wakazi wa wilaya hiyo, kuhakikisha wanashiriki kwenye uchaguzi huo ili kuleta maendeleo.

Aliwataka wajitokeze kwa wingi, kuchagua viongozi wanaowataka. Alitoa mwito huo juzi kwenye maadhimisho ya Siku ya Serikali za Mitaa, yaliyofanyika Kijiji cha Sululu Kata ya Sululu wilayani humo.

Tunaunga mkono mwito wa Mkuu huyo wa wilaya, kwani tunataka watu wengi washiriki katika uchaguzi huo ili kukuza demokrasia iliyopo nchini. Uchaguzi huo ni muhimu kwa sababu unafanyika katika ngazi ya mitaa, ambayo ni muhimu na nyeti.

Mitaa, Vijiji na Vitongoji ndivyo vitovu vya shughuli za utawala katika nchi. Ndiko wanakoishi Watanzania wengi na huko ndiko ambako shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zinafanyika.

Viongozi bora na makini, ndiyo watakaobuni na kulinda utaratibu mzuri wa kuishi. Pia watahakikisha kuwa wananchi wanafuata utawala wa sheria.

Aidha, viongozi bora na makini watasimamia vizuri miradi ya maendeleo na huduma za kijamii zinazotolewa na serikali, kwa vile maji safi, umeme, barabara, mawasiliano na ulinzi wa raia.

Tunapenda kusisitiza kuwa ni jukumu la kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura, kuhakikisha kuwa anashiriki katika mchakato na hatimaye kupiga kura katika siku husika.

Katika miaka ya karibuni, Serikali kuu imegatua madaraka yake kwa serikali za mitaa, yaani imepeleka madaraka mengi mikoani na wilayani kwenye halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji.

Halmashauri hizo nazo zinatenga na kupeleka mafungu mengi katika vitongoji, vijiji na mitaa. Hivi sasa, kwa mfano, katika huduma za afya, kuna Kamati za Afya za Vijiji.

Kamati hizo ndizo zinazopendekeza viwango vya fedha, ambazo kila kaya katika kila kijiji inatakiwa kuchangia katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Hii ni katika wilaya zilizoanzisha Mfuko huo.

Kuna wilaya ambako kila kaya inatakiwa kuchanga Sh 5,000 kwa mwaka. Zingine kila kaya huchangia 10,000 kwa mwaka na zingine kila kaya huchangia Sh 20,000 kwa mwaka.

Mbali na kupendekeza kiwango cha kuchangia, Kamati za Afya za Vijiji pia zina jukumu la kusimamia ukusanyaji wa fedha hizo katika kaya na matumizi yake.

Hali kadhalika, wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa ndio wasimamizi wakuu wa ulinzi na usalama katika maeneo yao kwa kushirikiana na vyombo vya dola, kama Jeshi la Polisi.

Kwa ujumla, serikali za mitaa ni chombo muhimu kwa maendeleo ya Taifa na wananchi kwa ujumla. Ni wajibu wa kila Mtanzania, kuhakikisha kuwa anaimarisha chombo hicho, ikiwemo kushiriki kwenye uchaguzi huo wa mitaa.

FUKUTO la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani linazidi ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi