loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tukatae chumvi, sukari, maji kwenye pamba

Kwa vyovyote vile, hii ni habari mbaya kwa taifa letu, ambalo uti wa mgongo wa uchumi wake unategemea kilimo, likiwemo zao la biashara la pamba.

Hakuna ubishi kwamba habari hii, inasikitisha na inapunguza kwa kiwango kikubwa ubora wa pamba yetu katika soko la ndani na nje ya nchi kwa kutupachika jina la ‘Pamba ya Tanzania haina ubora’, jina ambalo likiachiwa kukua, litakuwa kizingiti katika kupiga hatua ya maendeleo yoyote kupitia zao hilo.

Habari hiyo ilifafanua madai kwamba baadhi ya wakulima wetu katika wilaya za Bariadi na Itilima mkoani Simiyu, walikuwa wakiweka maji kwenye pamba ili kuongeza uzito, hususan wakati inapotangazwa bei ndogo ya zao hilo.

Kama vile hilo halitoshi, inadaiwa pia kuwa wanunuzi na wahasibu kwa upande wao, hunyunyuzia chumvi na sukari kwa lengo hilo hilo la kuongeza uzito wa pamba ili kupata faida. Kwa mtindo huu, tutafika kweli katika harakati ya kujikwamua na umasikini?

Mtafiti wa Kujitegemea wa zao la Pamba, Godfrey Chambua ameripotiwa akibainisha kwamba kuanzia mwaka 2005 hadi 2009, uzalishaji wa zao la pamba ulikuwa mkubwa na kuweza kuliingizia taifa Sh bilioni 92, hivyo kuongoza kuwa zao la kwanza kwa kulipatia taifa pato kubwa.

Lakini, baada ya hapo hali ya uzalishaji kwa mujibu wa mtafiti huyo, iliendelea kushuka kwa msimu wa mwaka 2012/2013 hadi msimu tulionao hivi sasa. Kwa vyovyote vile, hali hii haioneshi dalili njema kwa zao hili na uzito wake katika uchumi wa nchi yetu.

Katika hili, tungependa kuzikumbusha mamlaka zinazohusika na zao la pamba, bodi, menejimenti na wananchi kwa ujumla, kushirikiana kudhibiti hali hii ambayo tunaweza kuiita ni ya kuhujumu uchumi wetu, kwa kudiriki kuuza pamba yenye mchanganyiko wa chumvi, sukari na maji kwa kisingizio chochote kile.

Tunataka kuwakumbusha wenzetu, wanaofanya mchezo huu mchafu, kwamba unatuangamiza sote kiuchumi. Tunawasihi waache na kinyume chake wahusika katika usimamizi wa zao hilo, wawachukulie hatua za kisheria kudhibiti hali hiyo, isiyovumilika kwa maendeleo na ustawi wa taifa letu.

Hivi kwa mtindo huu, kwa nini bei ya zao la pamba kutoka Tanzania isishuke? Ushindani katika medani za biashara ya kimataifa, unatokana na ubora wa bidhaa inayouzwa.

Sasa kama bidhaa yetu, ndiyo inasheheni uchafu kiasi hicho, nani atakayekubali kutupa fedha zake kwa kununua pamba kutoka Tanzania? Wahenga walisema ‘’ Mwenye macho haambiwi tule’’.

Tusikubali kuruhusu hali hiyo iendelee huku tunaona bila kuchukua hatua, bali sote tushirikiane kwa hali na mali kuikabili vilivyo, isije kuota mizizi miongoni kwa wakulima na wanunuzi wetu. Tukishirikiana, tunaweza kushinda vita hii ya uhujumu wa uchumi wetu, kwani Umoja ni nguvu.

FUKUTO la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani linazidi ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi