loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tumuige Mfutakamba kusambaza nakala za Katiba ya sasa jimboni

Wanaposikia malumbano, mivutano au kususa kuhusu ushiriki wa kutoa maoni ya namna ya Katiba mpya, wanashangaa kwani ya zamani bado hawajaiona.

Kampeni za asasi za kijamii nchini pamoja na jukwaai la katiba kupitia kwenye vyombo vya habari kuhusu mchakato wa namna ya kuandaa Katiba mpya, wengi wa wananchi wanashindwa kushiriki kutokana na kutoijua vizuri Katiba ya mwaka 1977.

Wananchi hao, wanapenda kujua undani wa Katiba hiyo, ndiyo maana baadhi ya vikundi vya kuhamasisha kuhusu wananchi kushiriki katika kutoa maoni vinapata wakati mgumu kwani wananchi hawayajui yaliyomo katika katiba ya sasa.

Elimu juu ya katiba ya sasa hawajapata, ndiyo maana inakuwa vigumu kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kukusanya maoni kwa ajili ya uundwaji wa Katiba mpya.

Mbunge wa Igalula, Dk. Athuman Mfutakamba amepambana na malalamiko ya wananchi wa Kata ya Igalula wilayani Uyui, mkoani Tabora, ambao wameeleza wazi itakuwa vigumu kutoa maoni kwenye mchakato wa Katiba mpya kwa kuwa hawajui wala hawajawahi kuiona hiyo ya zamani.

Dk. Mfutakamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, amekumbana na changamoto hiyo, akaahidi kuchapisha zaidi ya nakala 250 za Katiba ya sasa ili wananchi wa kata za jimbo hilo wasome wajue kuna nini ndani yake.

Wananchi wa Igalula ni miongoni mwa Watanzania zaidi ya asilimia 80 wanaojua Kiswahili ambao wangependa kusoma Katiba iliyopo sasa, ili kutoa maoni ya kuandaa katiba mpya.

“Mheshimiwa waziri kwetu sisi itakuwa vigumu kutoa maoni kuhusu Katiba mpya kwani hata hii iliyopo hatuijui kabisa, hivyo mnapotuhamasisha tutoe maoni yetu tunaona kama mnatuonea,” wanasema wananchi wa Igalula.

Kutokana na changamoto hiyo muhimu, Mbunge Mfutakamba ameamua kutoa elimu kwa njia ya kuchapisha nakala 50 za katiba kwa ajili ya kila kijiji cha jimbo hilo. Lakini pia ameahidi kuweka nakala tano za katiba ya sasa katika ofisi ya mtendaji wa kijiji ambazo wananchi wa vijiji husika watatakiwa kusoma na kujadiliana kuhusu mambo yaliyomo ndani yake.

Juhudi za Mbunge wa Igalula, zinatakiwa kuigwa na kuungwa mkono na wabunge wengine nchini na hata wadau wengine, ili kuwapa fursa wapigakura kusoma katiba ya sasa na kuijadili ili washiriki katika mchakato wa kuandaa katiba mpya.

Mbunge huyo anaungana na juhudi za Rais Jakaya Kikwete ambaye anasema Tume ya Kukusanya Maoni itaanza kwenda vijijini ili kuonana na wananchi watoe maoni yao.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni mwendelezo wa juhidi zake tangu Novemba 29, 2011, alipotia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, kuruhusu mchakato wa Katiba mpya.

Kutia saini kwa Rais Kikwete kunakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa limepitisha muswada huo uliowasilishwa na Serikali katika kikao kilichopita cha Bunge.

Kutiwa saini kwa muswada huo ili uwe sheria, pia ametoa ufafanuzi na msisitizo Rais Kikwete wakati akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka 2010, kwamba wananchi washiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao.

Siku chache zilizopita, Rais Kikwete pia ametangaza wazi kuwa Tume ya Kukusanya Maoni kuhusu Katiba mpya itaanza kupita mikoani kuanza kazi ya kukusanya maoni. Hiyo ndiyo nafasi adhimu kwa wananchi, wanatakiwa kuitumia fursa hiyo katika kutoa maoni yao kuhusu wanavyotaka katiba hiyo iwe ambayo ni nguzo muhimu katika mustakabali wa nchi yetu.

Rais Kikwete anatamani Uchaguzi Mkuu wa 2015, ufanyike kwa kutumia Katiba mpya, jambo ambalo tume ya kukusanya maoni inatakiwa kuwa na muda wa kutosha katika kukusanya maoni mikoani.

Tume ya Kukusanya Maoni ya namna ya Katiba mpya inavyotakiwa iwe, itapata mafanikio makubwa kama wananchi watakuwa wanaelewa upungufu wa katiba iliyopo na kutoa marekebisho yao.

Kwa majimbo ambayo wabunge au wadau wengine wa maendeleo wanataka wananchi wao washiriki kikamilifu wamwige Mfutakamba kwa kusambaza katiba za sasa kwa wananchi wao ili washiriki katika kutoa maoni ya namna katiba mpya itakavyokuwa.

Kutokana na kutoelewa mambo yaliyomo katika katiba ya sasa, wananchi katika makongamano au mijadala mbalimbali, wamekuwa wakitaka wapate nakala za katiba ya sasa lakini pia wanaitaka Tume ya ukusanyaji wa maoni ufanye kwa uwazi na kwa maslahi ya Watanzania wote.

Miongoni mwa wananchi hao ni wa majimbo ya Kigoma Mjini na Kigoma Vijijini ambao katika mdahalo ulioitishwa na mtandao wa asasi zisizo za kiserikali (Kiungonet) wameomba Tume ya kukusanya maoni ifanye kazi kwa uwazi na haki.

Wananchi hao wamependekeza pia Bunge Maalumu la Katiba litakaloundwa, lazima liwe na uwakilishi sawia kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii nchini. Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba amewataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni yao wakati Tume ya kukusanya maoni itakapofika kwenye maeneo yao.

Mbunge huyo amewaonya wananchi wa jimbo lake kuwa, wasikubali kudanganywa na baadhi ya wanaharakati na vyama vya siasa vyenye lengo la kupotosha umma kuhusu mchakato huo wa Katiba mpya, wao washiriki.

Katiba ya 1977 inayotumika sasa ni matokeo ya katiba kadhaa tangu uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961. Katiba ya Jamhuri ikaja mwaka mmoja baadaye na ilidumu hadi 1965 ambayo iliundwa baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964 na ilidumu hadi 1977 ilipoundwa ya Muungano inayotumika hadi sasa.

Baada ya katiba hiyo, kulifanyika marekebisho mengi yakiwamo ya 1984 ambayo yaliingiza masuala ya haki za binadamu kwenye Katiba hiyo.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi