loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tuoneshe uzalendo kwa vitendo siyo kwa hotuba, midahalo

Ukiangalia kwa undani sana utakutana na sura mbili za kisiasa upande wa kwanza wa siasa ni ile siasa ya kuchafuana na siasa ya pili ni ile ambayo inalenga kukiingiza chama madarakani yaani kinatanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya taifa kwa ujumla wake. Huku wapinzani wakielekeza nguvu zao kwenye kuilaumu Serikali kwa kuonesha jinsi gani imeshindwa huku wao wakisahau wajibu na nafasi yao.

Kimsingi haihitaji pesa nyingi sana kwenye chama ili kuweza kuleta maendeleo ya wananchi na pia siamini kabisa kama kwa kuwa na chama ambacho kimeongoza kwenye uchaguzi ndiyo kuleta maendeleo, siamini hilo hata kidogo. Mbadala wake naamini kwamba utayari wa chama na mtu binafsi na kujitoa kwa mtu husika na chama husika ndicho kinachoweza kuleta maendeleo kwa wananchi kwa ushirikiano hasa kwa ushawishi wa kiongozi husika.

Ubunge au udiwani haina maana ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa kitanzania ila mbadala wake ni kutambua kero za wananchi wa eneo husika na kutafuta njia za kuzitatua na kufanikisha lengo hilo kwa kiasi fulani huo ndiyo uongozi tunaoutaka.

Ni mara nyingi sana wanasiasa wa vyama pinzani hasa CHADEMA na CUF wamekuwa wakipinga jitihada zinazofanywa na chama tawala katika kuleta maendeleo ya wananchi hata kwa hicho kidogo wanachokibeza lakini angalau wamejitahidi hasa kwa kuzingatia nchi ilikotoka na changamoto ilizozipitia lakini bado angalau kwa sasa wananchi wanapata hicho kidogo kilichopo katika hali ya kawaida tulipaswa kuwatia moyo ili angalau chama husika kama kikiendelea kuwa madarakani kiweze kuzidisha hapo padogo panapobezwa.

Lakini mbadala wake tumeshuhudia wapinzani wetu wakizunguka taifa zima kwa helkopta kutangaza maovu ya Chama tawala swali langu la msingi ni kwanini hizo fedha wanazotumia kuzunguka wasitumie japo kuchangia kwenye maendeleo ya taifa japo kwenye sekta mojawapo ya wanazozipigia kelele kila kukicha?

Sisemi kwamba wasifanye hivyo maana kwa kufanya hivyo pia wanakitangaza chama lakini kwanini wasitoe fungu japo kidogo la ruzuku yao wakaboresha japo sekta mojawapo na tukaamini kuwa wana moyo na uzalendo wa kuikomboa nchi yao? Sisemi haya ili kuwafanya waache jitihada zao lakini ni lini na wao wataonesha mfano wa mambo fulani fulani katika kutetea maslahi ya taifa hili?

Katika nchi za wenzetu upinzani ni wakati wa kampeini zikiisha tu wote wanakuwa wamoja na kushirikiana na chama tawala kuijenga nchi au taifa husika kwanini hapa kwetu wapinzani wetu wasifanye hivyo? Kwanini wao Januari mosi hadi Januari mosi kazi yao ni kubeza tu huku hawaoneshi uzalendo wao katika taifa?

Maana ili ubeze la mwenzio inabidi uwe na mashiko kwamba mimi nimefanya hiki mbali ya upinzani iweje wewe ushindwe ili hali mtawala? Hapo Watanzania watawaelewa lakini sivyo mnavyofanya! Matokeo yake mnaumbuana wenyewe kwa wenyewe jamani siasa inaenda hivyo?

Mheshimiwa Mbatia kiukweli ni mpinzani wa kuigwa kwa mtazamo wangu kwa maana mbali yakuwa ni mpinzani bado Rais wetu aliona ni vyema amteue kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siyo kwasababu ni maswahiba hapana bali ni kwa sababu katika maongezi yake mengi na matendo yake mengi anatanguliza utaifa kiuhalisia ndiyo maana hata Rais wetu alimuona na hivyo kumpa nafasi ya kuwa bungeni.

Hatahivyo leo sikulenga kuwasifia viongozi wa kisiasa ila nimelenga kubadilisha mtazamo wa kisiasa wa wanasiasa wetu na hivyo kuwafanya sasa wawe wanasiasa wenye mrengo wa kulikomboa taifa letu kwa vitendo lakini si kwa kuongea kwenye mihadhara tu lakini kwa vitendo hakuna kitu. Tuangalie hili la magari ya kifahari.

Kimsingi magari haya yanatesa taifa kwenye utunzaji lakini mbona wabunge wote wanapopewa magari haya hawayakatai? Lakini wakiwa nje wanasema CCM inatumia magari ya kifahari ilihali naye ndilo analoendesha na wala halikatai sasa hapa tunapinga nini na tunakubali nini?

Kwanini umnyoshee kidole mwenzako ilihali vitatu vinakutazama wewe? Ili wananchi tuwaelewe wapinzani kuwa mnalengo la kuikomboa nchi yetu, anza kwa kuonesha mfano kwa hicho kidogo mnachokipata! Kwa mfano kila jimbo linapewa fedha ya maendeleo ya jimbo, je wabunge hawa fedha hizi wanazitumia inavyotakiwa?

Je wanazitumia kuleta maendeleo kwenye maeneo yao japo kwa kuanza tu alafu wailalamikie Serikali kwa kutokamilisha kama Mbunge wa Singida alivyoiomba Serikali imalizie ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa huo?

Au lenu ni kulalamika tu? Haina haja kila siku mnaishia kusema serikali haifanyi hiki, serikali haifanyi kile kwanini siku moja tusiseme sisi tumeanza ila serikali imeshindwa kumalizia ili wananchi na wao waone na kufanya uamuzi? Kwanini kila siku nyinyi ni kulalamika tu?

Hivi ni lini tuliwahi kumuona mbunge yeyote wa marekani au seneta yeyote akimlalamikia Rais Obama kuwa hafai haleti maendeleo au hili au lile? Haya yote hayapo huko kwasababu kabla hajaanza kulalamika kwa wananchi, anajiuliza maswali mengi kwamba hivi maendeleo yangu mwenyewe naletewa na nani?

Hivi ni kilalamika nikaulizwa mimi nimeanza kufanya nini nikashindwa na kumpelekea bwana mkubwa ambaye ni Serikali akashindwa kumalizia?

Tuangalie hili nalo, wakati kiongozi mkubwa wa upinzani akizunguka taifa zima kuhutubia upinzani, mbunge wake ambaye alikuwa ni Naibu Katibu wa Upinzani Bungeni akashutumiwa na mbunge mwenzake kwa ufisadi ule ule, sasa hali kama hiyo tunafikiri ni Mtanzania gani ataamini kuwa tupo tayari kulijenga taifa iwapo ninyi wenyewe uzalendo umewapiga chenga?

Labda hili la kutumia kidogo mlicho nacho ni shida je, kuisaidia Serikali kuwatafuta wawekezaji ambao hawatolitia taifa hasara nalo mnashindwa? Au na lenyewe mnatupa nje ya mchakato? Vipi wote hamna akaunti za nje? Na je wote watoto wenu wanasoma nchini? Vipi hili la kutibiwa nje ya nchi haliwakumbi? Sasa kama haya yote mnahusika, uzalendo mnaoimba kila siku uko wapi?

Na vipi wote mnakaa majimboni kwenu? Au mnaenda wakati wa mihadhara yenu na kampeini? Lengo la leo siyo kuamsha hisia zenu za hasira na hivyo kuwafanya mnitafute kunimalizia hasira hizo ila lengo langu la msingi ni kwamba tusiwe watu wa kulalamika kila siku ila muda mwingine tuoneshe mifano kwa vitendo ili tuamini kuwa ninyi ni wazalendo, siyo kuhutubia sana kwenye mihadhara huku hata kidogo mnachokipata hamkitumii na wananchi wanaozunguka majimbo yenu. Na hili jingine linanikera sana “kuzira bungeni”.

Jamani hivi mnapotoka nje ya Bunge mnajua nyuma kunajadiliwa nini? Sasa ikitokea mkatoka na kumbe kulihitajika mchango wenu ni nani atakaye wawakilisha?Au mnapotoka bungeni mnamkomoa nani?

Maana mwisho wa siku naona tunaanda maandamano na mihadhara kuhutubia kuwa serikali iliyo madarakani haina uzalendo na nchi, hivi katika hali ya kawaida ni nani ana uzalendo Yule anayebaki hadi mwisho wa tukio ambaye hata likitokea la kutokea anauwezo wa kuwaeleza wananchi wakamuelewa au yule anayekimbia hata kabla ya muafaka kufikiwa?

Wakati wa Musa kuwaongoza wana wa Israel tunaambiwa alikutana na vita kali sana kwa uongozi na wana wa Israel wenyewe lakini hata siku moja Musa hakuacha kumpigia Mungu magoti huku akiomba amuoneshe jinsi ya kutatua changamoto zilikuwa zinatokea mbele yake. Hivi tujiulize angekuwa mtu wa kulalamika kila siku Mungu angefanyaje?

Mlipaswa kufanya hivyo; mpingwe, mkataliwe, mzomewe lakini endeleeni kupambana na siyo kutangaza siasa ya chuki na vita huku nyuma hakuna lolote mnalolifanya. Siku zote mtu wa kulalamika hana jema niaminivyo mimi.

Kwa mfano muda tunaotumia kuzunguka taifa zima mngeutumia kukaa na wananchi wenu na kusikiliza kero zao nadhani ingewasaidia kujua ni kitu gani cha kufanya katika kutatua kero hizo lakini mbadala wake tunaishia kuwa wahubiri wa siasa za chuki badala ya kuwa wanasiasa vitendo.

Maandiko yanasema hivi, akupigaye shavu la kushoto mgeuzie na lile la kulia wala usimrudishie huo ndiyo uungwana kwa vitendo. Nimalizie kwa kusema hivi, upinzani wetu wa hapa nchini haulengi kujenga ila badala yake unalenga kutengeneza chuki kati ya watawala na wataliwa suala ambalo litaliweka taifa pabaya.

Tusidhani kwamba kwa kufanya hivyo mataifa yenye nia mbaya na nchi hayafurahi! Hapana ila mbadala wake yanafurahi kuona hiyo hali na hivyo kuzidi kupandikiza chuki kwetu Watanzania ili mwisho wa siku tutawaliwe kiulaini. Hebu tubadilishe mfumo wa siasa ya upinzani na tuangalie jinsi ya kulikomboa taifa letu kwa pamoja na siyo kwa kutangatanga tu kama mbayu wayu. Tanzania ni yetu sote, wa kuijenga ni sisi sote tushirikiane kufanya jambo hilo.

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Shahada ya Mawasiliano ya Umma na Habari. +255 712 246001, flugeiyamu@ gmail.com

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba ...

foto
Mwandishi: Felix Lugeiyamu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi