loader
Tushindwe soka hata waamuzi pia?

Tushindwe soka hata waamuzi pia?

Mchezo wa soka ni mmoja ya michezo ambayo Serikali imejikita katika kuisaidia kwa hali na mali hasa tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani. Matokeo chanya yaliyopatikana kutokana na juhudi hizo za Rais Kikwete ni pamoja na kuongezeka kwa hamasa ya mpira wa miguu kwa wananchi pamoja na kampuni mbalimbali kujikita katika kudhamini mchezo huo.

Ila ikumbukwe kuwa ili mchezo wa mpira wa miguu uendelee kuimarika, ni lazima wawepo waamuzi wenye uelewa wa kazi yao. Kwa nchini, suala la waamuzi limekuwa ni tatizo kubwa ambapo kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu uhaba wa waamuzi na hata waliopo wengine hawana sifa stahili.

Waamuzi wengine wamekuwa wakishutumiwa kwa makosa mbalimbali kama vile suala la upangaji wa matokeo ya mechi.

Hilo linajidhihirisha hata katika wiki mbili zilizopita ambapo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunga semina ya waamuzi iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Malinzi alionekana kusononeshwa na kilichoitwa ubabaishaji na ukiukwaji wa maadili kwa waamuzi hao nchini. Alisema TFF imekuwa ikiwasimamisha kazi waamuzi mara kwa mara pindi wakiwakamata kujihusisha na upangaji wa matokeo au matukio mengine yasiyokuwa ya kimichezo.

Malinzi pia anasema kuwa kwa Tanzania licha ya kuwa kuna uhaba mkubwa wa waamuzi, lakini haifai kuwapo na hali ya ubabaishaji wa namna yoyote ile. “Ni kweli shida ipo ya waamuzi lakini sio kigezo kwa waliopo kuendekeza njaa zisizovumilika, inatakiwa kuzingatia maadili ili angalau siku moja tuwe na waamuzi wanaochezesha soka kwenye michuano mikubwa,” anasema Malinzi.

Anaongeza kuwa inasikitisha kuona kuwa katika michuano mikubwa ya hapa hapa Afrika waamuzi kutoka Tanzania hawaitwi. Anaongeza kuwa hiyo inaashiriia kuwa hakuna nia ya dhati ya waamuzi katika kujitangaza na kuonesha uwezo wao ili nao wakapeperushe bendera ya Tanzania nje ya mipaka.

Anasema kuwa haiwezekani kwa zaidi ya miaka 15, Tanzania imetoa mwamuzi mmoja tu kuchezesha michuano mikubwa ambaye alichezesha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Anaongeza kuwa ilikuwa ikitakiwa kuwa na waamuzi wengi wa Tanzania wakichezesha kwenye michuano mikubwa kama vile Kombe la Dunia.

Anaongeza kuwa nchi kama Rwanda imekuwa na waamuzi waliokwenda kwenye michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Brazil mwaka huu. Lakini kwa Tanzania, hakuna hata mmoja hali ambayo inatokana na changamoto nyingi. “Sisi kama TFF tunawaletea mafunzo kama haya, lakini sasa inakuwaje nyie mshindwe kutuletea faida ya kutokana na mafunzo haya, acheni mchezo fanyeni kazi,” alisema Malinzi.

Anaongeza kuwa zipo juhudi za TFF na pia zinatakiwa kuwapo juhudi za waamuzi wenyewe. Waamuzi wengi wanashindwa hata kujiwekea ratiba ya kufanya mazoezi ya kuimarisha fiziki zao. Inatakiwa kwa kila siku kuwa na mazoezi ambayo yatawawezesha hata wakiwa uwanjani kuhimili suala zima la pumzi.

Anakiri kuwapo kwa uhaba mkubwa wa waamuzi nchini hasa katika Mkoa wa Ruvuma alipofanya ziara yaje na kukuta mkoa mzima una waamuzi nane. “Sijui hata huyo bingwa anapatikana vipi kwa kuwa kama mkoa mzima una waamuzi wanane ina maana kuwa hakuna haki kwenye uchezeshaji wa soka hapo, nimeiagiza TFF ifuatilie suala hili,” anasema Malinzi.

Pia Malinzi anaiomba Idara ya Michezo ya Chuo Kikuu Dar es Salaam kuhakikisha kuwa wanashirikiana na TFF katika utoaji wa mafunzo ya uamuzi kwa wanafunzi wa chuo hicho. Ni imani yake kuwa kwa kufanya hivyo wanaomaliza kwenye kitivo hicho watakuwa na sifa za kuwa waamuzi wazuri na sio kutegemea kuwa maofisa wa michezo tu.

“Sisi tupo tayari kusaidiana na kitivo hicho na kuwa hakuna sababu ya kuwaacha wasomi wale wamalize na kufanya shughuli nyingine tu huku hata kwenye uamuzi wanaweza kufanya vema, tufanye kazi pamoja,” anasema Malinzi. Lakini pia anaongeza kuwa waamuzi wasomi wanaweza kuitoa Tanzania kimasomaso kwenye uwakilishi wa medani ya kimataifa kwenye fani hiyo.

Anasema kuwa iwapo nchi ikiwa na waamuzi bora, basi ni dhahiri kuwa hata mchezo wa soka pia utakuwa bora. Anabainisha kuwa moja kati ya vitu vinavyorudisha nyuma maendeleo ya soka nchini ni pamoja na uwepo wa kampuni za nje ya Tanzania zinazochezesha michezo ya kubahatisha kwa ligi ya nyumbani.

Anasema kuwa watu hao iwapo wanajishughulisha na upangaji wa matokeo hayo watajulikana tu na FIFA. Anawataka kutambua kuwa kamwe ofisi yake haitomvumilia wala kumsaidia mtu yeyote ambaye atakamatwa kujihusisha na upangaji wa matokeo.

Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele kwenye nia yake ya kuwa na waamuzi wazuri, TFF ikishirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) liliandaa semina ya siku nne iliyowashirikisha waamuzi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Ilihudhuriwa na waamuzi 27 kati yao wanawake wakiwa tisa. Kwa upande wake, mmoja kati ya waamuzi waliohudhuria mafunzo hayo, Mohamed Mkono wa mkoani Tanga, anasema kuwa katika mafunzo hayo ya siku nne, yamemfumbua macho kuhusu vitu vingi katika fani hiyo ya uamuzi.

“Ni mafunzo muhimu kwetu na TFF ikishirikiana na FIFA iendelee hivi hivi kutuletea kozi kama hizi nyingi ili na sisi hatimaye tuwe wa kimataifa,” anasema Mkono.

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi