loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tutatue matatizo Hospitali ya Tumbi

Barabara hiyo kuu pia huenda mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya hadi Zambia na Malawi. Aidha, Mkoa wa Pwani unapitiwa na barabara kuu nyingine iendayo mikoa ya Kaskazini ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Mara na kwenda Nairobi nchini Kenya na Kampala nchini Uganda.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi barabara za mkoa huo, zina shughuli nyingi usiku na mchana kuanzia mwezi Januari hadi Desemba kila mwaka.

Wingi wa pilikapilika hizo za barabarani na uzembe wa madereva, umesababisha mkoa huo kuwa na ajali nyingi na za mfululizo. Watu wengi wameuawa na maelfu wengine kujeruhiwa katika ajali hizo.

Lakini, jambo la kusikitisha ni kuwa Hospitali Kuu ya Mkoa, Tumbi, inayotegemewa na wananchi wengi wa mkoa huo na maeneo jirani, ina matatizo mengi hivi sasa, hivyo kuathiri ufanisi wake.

Wiki iliyopita, Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Bryson Kiwelu alibainisha matatizo kadhaa, yanayokabili hospitali hiyo.

Alisema hayo kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa waandishi wa habari wa mkoa huo.

Kiwelu alibainisha kuwa hospitali haina vifaa vya kutosha vya kupimia magonjwa mbalimbali, ikiwemo CT scan na X-ray. Mathalani, zinahitajika mashine nne za X-ray, lakini iliyopo ni moja tu.

Kwa upande wa mashine za Ultra-sound, zinazohitajika ni kumi, lakini zilizopo nne. Baadhi ya wagonjwa, ikiwemo majeruhi wa ajali za barabarani, wamekuwa wakipoteza maisha wakiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo hivyo, ikiwemo vya CT scan na X-ray.

Jambo lingine lililo wazi ni kuwa usafirishaji wa wagonjwa, hasa majeruhi, kwa kutumia gari la wagonjwa, kutoka Tumbi hadi Muhimbili, umekuwa ukitumia fedha nyingi, hasa za kununulia mafuta.

Hospitali hiyo iliyopo wilayani Kibaha, inakabiliwa na matatizo mengine ya uhaba wa madaktari. Dk Kiwelu amebainisha kuwa hospitali hiyo ya mkoa, ina upungufu wa madaktari 11, ambapo waliopo ni sita.

Hili ni pengo kubwa na linatakiwa kuzibwa mapema. Matatizo mengine ni ya maji na ucheleweshwaji wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD).

Matatizo yote hayo, yapo muda mrefu, licha ya hospitali hiyo kupandishwa hadhi hivi karibuni kuwa ya rufaa ya mkoa.

Kwa ujumla, wakati hospitali za mikoa mingine, zina vifaa vinavyolingana na hadhi ya hospitali hizo, hali ni tofauti kwa Tumbi.

Tunamuunga mkono Mganga Mkuu huyo, aliyeomba hospitali hiyo kutupiwa jicho ili matatizo yake yatatuliwe haraka.

Tunasema hivyo kwa sababu ya umuhimu mkubwa wa hospitali hiyo, hasa kutibu watu wanaojeruhiwa katika ajali za barabarani.

Pia, Hospitali ya Tumbi inategemewa na wananchi wengi wa mkoa huo na maeneo jirani, kama vile baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam.

Wakazi wa Dar es Salaam, hasa wa maeneo ya Mbezi, Kibamba na Kiluvya, walikuwa wakitibiwa Tumbi kwa wingi huko nyuma. Lakini, kwa sasa hali ni tofauti, kutokana na matatizo mbalimbali ya hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa Kiwelu, Tumbi inahudumia wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku na ina vitanda 254 vya kulaza wagonjwa.

Hii ni idadi kubwa. Kuna umuhimu kwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, zinatakiwa kupanga mipango ya dhati, kurejesha hadhi ya hospitali hiyo.

Huko nyuma ilikuwa hospitali, inayokimbiliwa na watu wengi, kutokana na ubora wa huduma zake. Serikali Kuu nayo isaidie hospitali hii.

Tusiliachie Shirika la Elimu Kibaha peke yake, kusimamia hospitali hiyo muhimu. Tufuatilie kwa makini maendeleo ya hospitali hiyo na kutatua matatizo yake.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi