loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ubakaji, utelekezaji watoto isiwe miradi ya visasi na kukomoana

Huenda ndiyo sadaka yake. Kesi dhidi yake imetamatishwa kwa kukubali kulipa Sh 580,000 taslimu zikiwa gharama za matumizi, matibabu na mavazi kwa ajili ya mtoto aliyedaiwa kuzaa na Maria Bonphas.

Akalipa kiasi hicho kupitia kwa dada yake, Bahati Michael, mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Utemini mjini Singida, Ferdinand Njau na kukubali kufanya hivyo ifikapo Juni 10, mwaka huu.

Huu ni ungwana maana watoto ni wa taifa, lazima watunzwe na kusaidiwa. Ametimiza utume maana waamini wangeendelea kuumia kuona padri wao anahangaika mahakamani kutokana na kile kinachodaiwa kwamba ni chuki, fitina na uchochezi unaodaiwa kufanywa na wale wanaoaminika kutopenda uchapakazi wake na hata nafasi ya masomo aliyopata padri huyo nje ya nchi.

Hili ndilo angalizo la kwamba, tuhuma za ubakaji na utelekezaji watoto zisigeuzwe kuwa miradi ya kukomoana na kulipizana visasi dhidi ya viongozi wa dini na wanasiasa huku baadhi ya wahusika wakichochea kwa sura ya kutaka waonekane wanasaidia, kumbe wana ajenda ndani yao.

Tukiacha hilo la Padri, gazeti moja la kila siku, mwanzoni mwa mwaka limekuwa na habari isemavyo, 'Aua Mkewe Wakigombea Ndoo ya Maji'.

Gazeti limemnukuu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela akisema kuwa, Salehe Mohamed (75), mkazi wa Irisya wilayani Ikungi, aliingilia ugomvi kati ya wake zake wawili waliokuwa wakigombea ndoo ya maji na kusababisha kifo cha mke mkubwa wakiwa shambani.

Kamanda Kamwela akasema baada ya Salehe na mkewe mdogo kugundua kuwa mke mkubwa amefariki, walishirikiana kumbeba na kumpeleka katika kibanda cha jirani na shamba hilo kisha wakamfungia kamba shingoni kusingizia kuwa alikuwa amejinyonga.

Kadhalika, Desemba 13, mwaka uliopita, mkazi wa kitongoji cha Songambele mjini Tarime, alikatwa mapanga na mumewe katika mguu wa kulia kwa madai kuwa, amemzuia mtoto wao wa kike mwenye umri wa miaka 14 kwenda kukeketwa.

Mwanamke huyo anakumbwa na masaibu hayo baada ya kumwambia mumewe asimpeleke mtoto wao kukeketwa kwani mila hiyo hatari imepitwa na wakati. Kwamba siku moja kabla, baada ya mke huyo kutoka mnadani Nyamwigura, alikuta binti yake, mumewe na mama yake mdogo wote hawapo na alipouliza aliambiwa wamempeleka kukeketwa.

Amenukuliwa akisema, “Mume wangu aliporudi nyumbani asubuhi alinikuta na nilipojaribu kumuuliza kuhusu suala la mtoto wangu alipompeleka, alishikwa hasira na kuanza kunikimbiza kwa panga ili anikate… Nilipiga yowe kuomba msaada ghafla, nikaanguka chini ndipo alipopata nafasi ya kunikata mguu.”

Kimsingi ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni vitendo vinavyodhoofisha ustawi wa jamii na kukuza uchumi katika familia nyingi na ndiyo maana Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na washirika wake katika Mpango wa Kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ujulikano kama GEWE II, kimelivalia njuga tatizo hili.

Tafiti nyingi zinaonesha kuwa ingawa wapo wanaume wanaonyanyaswa na wanawake majumbani au kazini ingawa wanaifanya siri, wanawake katika Tanzania wanaamini kuwa mume ana haki ya kumpiga mkewe endapo watatofautiana au kukorofishana.

Kijitabu kidogo cha Ukatili majumbani kilichoandikwa mwaka 2004 na Kituo cha Msada wa Kisheria kwa wanawake, kinazitaja baadhi ya aina za ukatili wa kijinsia hasa nyumbani kuwa ni pamoja na kupiga wanawake, ubakaji katika ndoa na wanawake kuingizwa vitu sehemu za siri.

Jarida la mafunzo la Ukatili majumbani dhidi ya wanawake la mwaka 1997 lililotolewa na ECA-WIDNET linautaja ukatili na unyanyasaji mwingine wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kuwa ni pamoja na vipigo vinavayosababisha maumivu, majeruhi na hata vifo; Pamoja na wanawake kutishiwa au kukatwa mapanga. Lingine kwa mujibu wa chapisho hilo, ni kitendo cha polisi na vyombo vingine vya dola kutochukulia malalamiko ya wanawake kwa uzito na umakini wakisema ni mambo ya kifamilia na kindoa.

Tamwa katika chapisho lake la mwaka 2001 liitwalo 'Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, 1998: Fahamu Baadhi ya Vipengele' inasema kuhusu ukatili kwa watoto ukurasa wa 17:

“Sheria inasema bayana kuwa mtu yeyote ambaye ana wajibu wa kulinda usalama wa mtoto chini ya miaka 18 na badala yake akamtendea vibaya, kutomjali au kumwacha mtoto huyo, au kama mtoto huyo ni wa kike, akasababisha mtoto huyo kukeketwa au akamweka katika mazingira ambayo yatampelekea mtoto huyo kushambuliwa na kutendewa vibaya, kutojaliwa au kutelekezwa katika mazingira yanayoweza kumsababisha kuumia kiafya ambako kunajumuisha kupoteza uwezo wa kuona, kusikia, au kusema au kupoteza kiungo cha mwili au kuathirika kiakili, basi aliyepelekea athari hizo kwa mtoto atakuwa ametenda kosa la ukatili kwa mtoto.”

Ripoti iliyotolewa Julai 22, 2013 na Tamwa kuhusu utafiti wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia uliofanyika katika wilaya 10 za Tanzania Bara na Visiwani, inabainisha kuwa, matukio ya kupigwa kwa wanawake nchini Tanzania bado yanaendelea.

Inazitaja sababu za ukatili huo kuwa ni pamoja na wivu wa mapenzi, ulevi, kukosekana kwa uaminifu kwa wanandoa, maisha magumu na ndoa za wake wengi. Ripoti hiyo ya Mpango wa GEWE II unatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili 2012- 2014 ikiyahusisha mashirika watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia yakiwamo ya TGNP, TAWLA, ZAFELA na Kituo cha Usuluhishi cha TAMWA (CRC) inasema:

“Hata hivyo, baadhi ya matukio ya wanawake kupigwa hayaripotiwi polisi ama mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe.”

Katika kisa mkasa cha ripoti hiyo ya Tamwa na washirika wake katika GEWE II inaelezwa kuwa Hellena Sikombe, mkazi wa Kifuru wilayani Kisarawe ambaye ni mama wa watoto wawili anasema, Aprili 10, 2013 wakiwa wanakunywa pombe pamoja na Edina Gazula, alipigwa na rafiki wa mume wake.

Ripoti inasema, “Alipomwambia mumewe, Mathew Lubida kwamba anakusudia kumfikisha rafiki huyo polisi, mumewe alimzuia huku akisisitiza kuwa, hatua hiyo itasababisha uhasama na majirani zao.”

Tamwa katika ripoti hiyo inasema, ukeketaji nao ni tatizo ambalo bado lipo nchini ingawa kwa baadhi ya wilaya unafanyika kwa siri kukwepa mkono wa sheria. Ripoti inasema wanaoendeleza mila ya ukeketaji katika kata za Kivule na Kitunda wilayani Ilala katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kiasi kikubwa ni wenyeji kutoka katika mikoa ya Dodoma na Mara ambayo mila ya kukeketa watoto wa kike imetawala.

Katika moja ya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka, mintarafu ukeketaji, anamnukuu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk Isha Mahita akisema ukeketaji wanawake una athari nyingi ikiwamo ya wanawake wanaokeketwa kutokwa damu nyingi na wengine kupoteza maisha.

Athari nyingine kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa afya na ripoti hiyo ya Tamwa, ni pamoja na mwanamke aliyekeketwa kutohisi hamu ya tendo la ndoa, kupasuka msamba wakatio wa kujifungua na hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na ngariba kutumia kifaa kimoja kukeketa wanawake wengi.

Tafiti pia zinaonesha kwamba kutokana na maingiliano ya sasa, wanawake waliokeketwa wako katika hatari ya kukimbiwa na waume zao kwani inaelezwa kwamba mwanamume akishafanya mapenzi na mwanamke asiyekeketwa hunogewa na kumtelekeza mkewe aliyekeketwa.

Uchunguzi uliowahi kufanywa Nyamongo, Tarime na mwandishi Hamisi Kibari, ulionesha kwamba kutokana na uwepo wa mgodi unaoleta wanawake wasiokeketwa kutoka sehemu mbalimbali imekuwa ni tatizo kwa ndoa nyingi.

Vijana wa Kikurya wakiwaandama warembo wasiokeketwa na kutelekeza familia zao. Wanaume waliohojiwa walikiri kwamba wanapata raha ya tendo la ndoa wanapojamiiana na wanawake wasiokeketwa kuliko wake zao waliokeketwa ambao pia inatakiwa wanaume wawandae muda mrefu ili 'kuwaridhisha'.

Lakini ripoti na tafiti zinasisitiza kwamba ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ukiwamo wa ndoa za utotoni, ubakaji na utelekezaji watoto ni mambo yanayopaswa kupigwa vita kwa nguvu na kwa umakini mkubwa ili kuepusha uwezekano wa baadhi ya watu kutumia mambo haya kama miradi ya kujipatia vipato na kuwakomoa wengine.

Mfano ni sauti kadhaa zinazotajwa na baadhi ya waamini wa Jimbo Katoliki la Singida wakidai tuhuma dhidi ya Padri Makuri ama zipo au hazipo katika usahihi wake, zimepangwa na kushinikizwa na watu wasiopenda maendeleo yake.

Ndiyo maana inatakiwa tuhuma za ubakaji na utelekezaji zisigeuzwe kuwa miradi ya kukomoana. Joseph Sabinus ni mwandishi wa kujitegemea

“WANAOFANYA shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi