loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ubinadamu ulindwe kwa gharama yoyote ile

Taarifa ya polisi ilisema mifuko 85 yenye viungo mchanganyiko vya binadamu, vikiwemo vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu na mifupa, vilikutwa katika eneo hilo.

Ilibainika pia kwamba viungo hivyo, kwa mara ya mwisho, vilikuwa katika maabara ya Chuo Kikuu cha Madaktari cha International Medical and Technological University (IMTU) kwa ajili ya mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari.

Habari hii imeleta taharuki na mkanganyiko kwa wananchi, kutokana na kwamba tukio la aina hii, halijawahi kutokea hapa nchini na ukweli kwamba mwili wa binadanu kwa wakati wote hushughulikiwa kwa heshima na hadhi inayostahili.

Lengo la chuo kikuu chochote cha madaktari la kuwa na viungo mbalimbali vya binadamu kwa ajili ya mafunzo ya vijana, wanaosomea fani hiyo yenye hadhi ya pekee duniani, ni zuri na halina ubishi.

Lakini, kitendo cha kugeuza lengo hilo zuri, kukosea hadhi viungo hivyo, kwa kuvitupa mithili ya taka, hakikubaliki.

Tukumbuke kwamba licha ya IMTU, vipo vyuo vingine vikongwe vinavyotoa taaluma ya udaktari nchini, ambavyo ni Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) na Chuo Kikuu Katoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi (CUHAS).

Lakini, pamoja na vyuo hivyo vikongwe kuwepo muda mrefu, hatujawahi kusikia wala kushuhudia kitendo cha aina hii, licha ya ukweli kwamba nao wanatoa mafunzo ya udaktari na huhitaji viungo vya binadamu kwa ajili ya mafunzo hayo.

Hivyo kwa sasa tunajiuliza maswali mengi, yasiyokuwa na majibu ya moja kwa moja. Kwa mfano, kwa nini wasomi hao waliobobea katika taaluma hiyo nyeti, wafikie hatua hii?

Sisi tunaamini kwamba zipo taaratibu, kanuni na sheria za upatikanaji wa viungo vya binadamu kwa ajili ya mafunzo ya madaktari wetu watarajiwa.

Lakini, pia zipo namna ya kuhifadhi au kuviondoa viungo hivyo, pale madhumuni yake ya matumizi kwa mafunzo yanapokamilika. Inakuwaje utaratibu huo, haukufutwa na chuo hicho?

Tunaiomba serikali ichukue hatua stahiki kwa watuhumiwa katika suala hili ili lisirudiwe katika jamii yetu, inayoheshimu utu na thamani ya binadamu. Taratibu, kanuni na sheria, hazinabudi kufuatwa ipasavyo katika hili.

Tunatoa pongezi maalumu kwa jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua za haraka, walipopata taarifa juu ya suala hili, kwani vinginevyo lisingeshughulikiwa kwa ustadi.Pengine, tungeweza kupata madhara kwa afya na usalama wa wananchi katika eneo vilikopelekwa viungo hivyo.

Lakini hili pia liwe fundisho kwa vyuo vingine, vyenye mahitaji ya aina hii kwa ajili ya wanafunzi kuwa makini kwa kuzingatia yanayotakiwa katika suala hili bila kufanya ajizi. Lengo ni kulinda kwa kila hali hadhi na utu wa binadamu kwa gharama yoyote ile inayostahiki.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi