loader
Dstv Habarileo  Mobile
Uchafu unavyoendelea kujichimbia Dar es Salaam

Uchafu unavyoendelea kujichimbia Dar es Salaam

Ndio maeneo ambayo si jambo la kushangaza kukuta watu wakijisaidia haja kubwa na ndogo, ingawa kwa kujificha, na kufanya maeneo hayo na ya karibu yake kunuka mchana na usiku.

Hata hivyo, wachafuzi hao wa mazingira sasa wameongezeka kutokana na kuyafikia hata maeneo ya wazi, yaliyotengwa kwa ajili ya kutumiwa na watu wengi, mfano barabarani na kwenye viwanja vya mikutano ama vya michezo kama pale Mwembe Yanga.

Siku hizi kulikuta furushi kubwa la taka katikati au pembeni ya barabara ya lami si shida. Awali, ilizoeleka kwamba barabara za lami hasa zile kuu, kama ile ya Bagamoyo, Ali Hassan Mwinyi na nyinginezo, zinabaki safi wakati wote, lakini siku hizi, ukiwahi kupita kwenye njia hizo nyakati za alfajiri utakutana na mizigo ya taka na kujiuliza maswali mengi.

Viongozi wa wilaya za Kinondoni na Ilala wamekwishaeleza misimamo yao kuhusu usafi wa wilaya zao kuwa ni lazima na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam naye kwa upande wake amezungumzia umuhimu wa kuwa na jiji lisilo na harufu mbaya, akisema wakazi wenyewe kwa umoja wao wanaweza kuufanya mkoa wao kuwa mfano wa kuigwa kwa usafi.

Lakini, jambo la kujiuliza ni je, wanaotupa taka ovyo hadi kwenye njia kuu na mbele ya mageti ya makazi ya watu wengine, au kwenye mitaro na vichochoro hawaonekani? Au huko nako kunatakiwa kupelekwe askari wa usalama barabarani ili wawakague watu wanaopita kwenda na kurudi kama wamebeba taka wanazolenga kuzitelekeza mahali kokote?

Jibu ni hapana, kwa sababu, kazi hiyo inazihusu serikali za mitaa, manispaa na viongozi wanaohusika nazo kama wakuu hao wawili wa wilaya walivyozungumza na gazeti hili kuhusu masuala ya usafi na kueleza mikakati yao katika kuzuia uchafu usitupwe ovyo wakati ule mafuriko yalivyoharibu miundombinu na kusababisha maafa kwenye maeneo wanayoyasimamia.

Maeneo kama Tegeta Kwa Ndevu na Makumbusho, sasa yananuka na kuwa sawa na Tandale kwa Tumbo ambako wakazi wameamua kuizoea harufu mbaya na kuendeleza maisha bila hofu ya maradhi ya mlipuko.

Kwa kuizoea hali hiyo, wengine wameendelea kukaanga chipsi, samaki na hata kuuza mahindi ya kuchoma na karanga, pembeni ya mitaro iliyojaa maji machafu yanayotoa harufu mbaya huku wenyeji wakila chakula kibarazani na kutazama takataka zinazoelea kwenye mitaro hiyo ya maji machafu bila kinyaa.

Yote hiyo ni fedheha, ingawa wahusika wenyewe akiwemo Kuluthum Kareem anayefanya biashara ya samaki pembeni ya mtaro wenye maji yanayonuka pale Tandale kwa Tumbo anatamba kwa kusema, “Hii ndio hali halisi. Hata ukilala ndani ukafunga milango na madirisha harufu utaipata tu, sasa kipi bora, uchangamkie biashara au ukimbilie pasipo pako kukwepa harufu? Wenyewe tumeizoea.”

Kulthum anasema matumbo yao yamekuwa sugu na wala mazingira na harufu hiyo haiwasumbui wenyeji kama inavyowasumbua wageni wanaopita kwa magari binafsi au daladala. Anaeleza sababu ya kuwepo kwa uchafu huo kuwa ni kukosa maeneo maalumu ya kutupa takataka kutokana na ufinyu wa ardhi katika makazi yao, pamoja na uwepo wa ‘waswahili’ wengi wasioelewa umuhimu wa usafi wa maeneo yanayo wazunguka.

Godfrey Swai anayefanya biashara ya kutengeneza baiskeli katika eneo hilo la Tandale kwa Tumbo anasema kwamba uchafuzi wa mazingira mahali hapo unafanywa na watu wa eneo hilo pamoja na wapita njia. Anasema, wapo wanaopita na taka kwenye magari na kuzirusha katika mitaro mbalimbali kwenye eneo hilo.

“Nimekwishashuhudia mara kadhaa taka zikirushwa kwa wingi kutoka kwa watu wasio wa eneo hili. Wanavizia usiku au alfajiri na kuleta mifuko iliyokwisha ya mbolea au saruji ikiwa imejazwa taka ngumu na kuitelekeza kwenye mitaro. Kama unakuwa si makini katika eneo lako la kazi, unaweza kukuta umedondoshewa uchafu pia,” Swai anasema.

Anasema yote hayo yanafanywa kwa makusudi na watu wanaotaka kwao kuwe kusafi wakati wote na Kwa Tumbo kuendelee kuwa kuchafu, kwa sababu, asilimia kubwa ya wanaoishi kwenye eneo hilo ni wenye kipato cha kati na cha chini.

Vipi kuhusu mateja?

Mkazi mwingine wa eneo la Kwa Tumbo, Julius Reuben anasema eneo lake la kazi linapendwa sana na mateja kwa sababu wamekuwa wakifuata kivuli wakati wa jua.

Lakini, anasema tofauti na inavyofikiriwa na wengi kuwa mateja ni wachafuzi wakuu wa mazingira, wakinywa viroba vyao huhifadhi vifuko mifukoni mwao au “kuja kunitupia katika kaunta ya baa yangu, si barabarani”. “Inawezekana wengine wakatupa ovyo vifuko hivyo vya viroba, lakini kwa uzoefu wangu kwa mateja, si wachafuzi wa mazingira kama inavyodhaniwa na wengi.

Tena kwa uchafuzi kwa chupa tupu za plastiki ndio hawastahili kulaumiwa kabisa kwa sababu hawana uwezo wa kununua maji hayo. “Teja akisikia kiu bomba linalotiririsha maji karibu yake linakuwa ndio pona yake. Hapati muda wala kuwa na fedha ya kutafuta maji ya chupa ya uhai au mengine. Sana sana wengi wao wanaziokota chupa hizo na kuzikusanya sehemu moja kwa ajili ya kuuza, ili wapate fedha za kununua viroba na unga (dawa za kulevya). Wachafuzi wakuu wa mazingira yetu ni watu wenye utimamu wa akili,” Reuben anasema.

Mitaroni barabara ya Bagamoyo

Wasafiri ndani ya Dar es Salaam wanaotumia vituo vya daladala vya Africana, Mbuyuni, Interchick, Bondeni na Tangi bovu wanasema taka zinazoonekana katika mitaro pembeni ya barabara ya Bagamoyo zinatupwa na watu mbalimbali, lakini waanzilishi wa uchafu huo ni wafanyabiashara wadogo wa samaki ambao humwaga maji na magamba ya samaki yanayonuka katika mitaro hiyo.

Kadhalika, wauza maji na juisi za chupa, biskuti, pipi na sigara nao wanatajwa kuwa wachafuzi wa mitaro kwa sababu huzembea kukusanya taka zinazoangushwa na wateja wao kwa sababu hawajaweka vifaa vya usafi kwa maana ya makasha ya kutupa taka. Ni kwa misingi hiyo inaelezwa kwamba mitaro hiyo ndiyo imegeuka kuwa makasha ya taka ngumu ingawa wakati mwingine huonekana asubuhi wakikusanya taka na kuzichoma moto lakini wanafanya kwa kulipua.

Awadh Shaban anayefanya biashara ya kuchoma mishikaki na kuuza pweza waliokaangwa katika eneo la moja ya vituo hivyo anasema, muda wote anapafanya mahali pake pawe pasafi kwa kuhakikisha anakusanya kila kijiti kinachotumiwa na mteja na kukiweka katika mfuko aliouandaa kwa shughuli hiyo.

“Jirani yangu huchoma mahindi kila unapofikia msimu wa mahindi lakini hata siku moja sijawahi kumwona akiacha ganda la mhindi hapa. Ana toroli dogo analoweka taka zake, hivyo eneo letu la biashara linakuwa safi muda wote,” anasema. Anaongeza kuwa, tofauti na anayekaanga samaki au kuuza samaki wabichi, ni lazima kuwe na harufu mbaya, kwa sababu, maji ya samaki anayowaoshea hayawezi kubebwa nyumbani, kwa hiyo ni lazima yatamwagwa barabarani au mitaroni.

Anasema pweza wake huwasafishia nyumbani, kama anavyofanya kwa nyama anayoiandaa nyumbani na kuhakikisha inabaki kuchomwa tu.

Wazoa taka wa mitaani

Kwa mujibu wa mfanyabiashara mwingine wa genge kwenye eneo la Africana, Ghati Watiku, uchafuzi wa mazingira unachangiwa na wazoa taka wa mitaani wanaotoza kwa Sh 300 kwa mzigo uliokusanywa siku nne hadi tano, kwa sababu hawana sehemu maalumu ya kuzitupa.

Kutokana na maelezo ya Watiku, wazoa taka hao ambao si rasmi kama wale wanaokuja kwa magari hurahisisha usafi wa maeneo wanapoziondoa taka hizo tu na kwenda kuzitupa mahali popote wanapojua wao.

“Kuwatumia watu hawa kunatokana na uzembe wa watu wanaopaswa kuondoa takataka na kuzipeleka kwenye madampo maalumu. Hawapiti wakati mwingine tunakaa na takataka hata mwezi mzima na wakija wanataka walipwe. Kwa kuwa hakuna anayetaka biashara yake ikwame kwa uchafu, tunaamua kuwatumia hawa wa Sh 300 ilimradi maeneo yetu yawe safi,” Watiku anasema.

Anaungwa mkono na mfanyabiashara maarufu wa nyama katika bucha liitwalo Mkulima lililopo Tegeta kwa Ndevu, Zacharia Malugu anayesema kuwa wanalazimika kuwatumia wabebaji hao wa Sh 300 kwa sababu hawawaoni wengine wa kubeba taka katika maeneo ya biashara zao.

Malugu anaeleza kuwa wabebaji wakubwa wanaopaswa kuchukua taka katika mitaa yao ya biashara hutokea mara moja moja au kutoonekana kabisa kwa miezi kadhaa hivyo kulifanya eneo lao la kazi kuwa chafu kiasi cha kuwafanya watafute njia zingine za kupunguza uchafu kama hiyo ya kuwatumia vijana wanaojitolea kuzoa taka kwa gharama hiyo.

“Nadhani umefika wakati wananchi waamue vinginevyo, kama ni kuwakataa wanaopata zabuni za kubeba taka kwenye maeneo yao au kujiwekea utaratibu mwingine wa usafi, vinginevyo Dar es Salaam itaendelea kunuka. Maeneo ni finyu huwezi kuchoma taka hapa wakati mtu mwingine anauza magauni yake ya dukani pale, hivyo suala hili litazamwe na kutafutiwa ufumbuzi,” Malugu anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana anasema uongozi wake una mikakati mingi kuhakikisha usafi wa mazingira katika eneo lake na kwamba kwa kuanza na uchafuzi wa mitaro, kutakuwa na ukaguzi wa mara kwa mara utakaowahusisha wahusika wote wa usimamizi kuona ni wapi kunahitaji udhibiti wa aina gani.

Anasema kama usafi usingekuwa unafanywa na wahusika wenye wajibu huo kutoka serikali za mitaa na manispaa, hali ingekuwa mbaya zaidi kwa sababu wachafuzi ni wengi na hutupa taka hizo usiku na mchana. “Madhara yake tumekuwa tukiyashuhudia wakati wa mvua. Mitaro inapoziba si harufu tu inayokuwa kero kwa watu bali hata mafuriko, kwa sababu maji yanakosa uelekeo kutokana na kuzibwa kwa mitaro na taka ngumu,” Rugimbana anasema.

Anaeleza kuwa hatua ya awali iliyofanywa na uongozi wa wilaya ni kuhakikisha mitaro inazibuliwa na kupanuliwa ili maji yasituame. Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi anasema, wakazi wake wanaelewa kuwa wanapaswa kuweka mazingira yao safi ikiwa ni pamoja na kutotupa takataka ovyo katika maeneo yasiyostahili na mitaroni, na kwamba hatua zinachukuliwa kwa yeyote anayekamatwa akifanya uchafuzi huo.

NDUGU msomaji, kwa muda mrefu nimekuwa nikiandika kuhusu ...

foto
Mwandishi: Namsembaeli Mduma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi