loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Uchafu wazagaa tena Dar es Salaam

Maeneo hayo ni Kariakoo, Jangwani, kituo cha daladala cha Tabata kilichopo barabara ya Mandela, kituo cha treni cha Mabibo, Mabibo sokoni, Manzese, Buguruni sokoni, Bunju, Boko, Mwananyamala, Kinondoni na Mbweni.

Utafiti uliofanywa na gazeti hili kwa wiki nzima, umebaini taka nyingi zimelundikana katika maeneo hayo bila kuzolewa kwa muda mrefu.

Taka hizo zinatoa harufu kali na nzi wamejazana kila mahali, hivyo kuleta kero kwa wananchi. Wakazi wa maeneo hayo waliohojiwa na gazeti hili, walishutumu viongozi wa Manispaa za Kinondoni na Ilala kwa kuzembea hadi kusababisha kero hiyo.

Aidha, walidai juhudi zilizoanzishwa na Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki na Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe za kusafisha jiji, zimezorota hivi sasa, kwani hawasikiki tena wakihimiza suala hilo.

Aidha, waliwashutumu wabunge wa Dar es Salaam na viongozi wa serikali za mitaa, kwa kufumbia macho uchafu, ulioanza kujazana tena mitaani na barabarani.

Wengine walilaumu makandarasi waliopewa zabuni ya kuzoa taka, kwa madai hawaonekani mitaani na pia viwango wanavyotozwa ni vikubwa mno.

Wazoaji taka hao wanadaiwa kutoza kati ya Sh 10,000 na Sh 30,000 kwa kila nyumba, kiwango ambacho ni kikubwa na wananchi wengi wa kawaida hawawezi kukimudu.

Mkazi wa mtaa wa Kariakoo kata ya Kariakoo, Hafsa Jumanne alisema wanalazimishwa kulipa ada ya uzoaji taka ya Sh 15,000 kwa madai wapo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Nashangaa waraka wa Manispaa ya Ilala unasema ada ya uzoaji taka iwe kati ya Sh 5,000 na 10,000 sasa wao wamezidisha na kwa sasa tuna karibu wiki mbili taka hazijazolewa”, alisema.

Mkazi wa Mbweni Teta wilayani Kinondoni, Zuhura Makwaia alisema wanatozwa Sh 30,000 kwa mwezi kama ada ya uzoaji taka na Kampuni ya Sumaita.

“Wanatutoza Sh 30,000 kwa mwezi na wanakuja kuchukua taka mara moja kwa wiki ambayo ni Alhamisi, wengine hawana uwezo wa kulipa, wanalazimika kuchimba mashimo ndani ya nyumba zao au kutupa kwenye viwanja vya watu ambavyo havijajengwa nyumba,” alisema.

Hata hivyo, gazeti hili lilipopiga simu kwenye Kampuni hiyo ya uzoaji taka kwa kutumia simu ilizoandika kwenye gari lao la uzoaji taka, lilielezwa ada ni Sh 30,000 kwa mwezi na wanachukua mara moja kwa wiki.

foto
Mwandishi: Sophia Mwambe

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi