loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

UCHANGIAJI ELIMU YA JUU: Dhana kongwe iliyoongeza idadi ya vyuo nchini

Licha ya será hiyo kuanza na kushika kasi tangu wakati huo, uchangiaji wa elimu ulikuwepo tangu wakati wa ukoloni na baada ya uhuru hasa kutokana na kuanzishwa kwa Azimio la Musoma mwaka 1974. Katika mfumo mpya ulioanza miaka ya 1990, mwanafunzi alitakiwa kuchangia sehemu ya gharama za elimu tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo alikuwa akipata bure elimu ya juu.

Kabla ya kuanza kwa mfumo wa uchangiaji, serikali ilikuwa ikitoa kila kitu kwa wanafunzi waliopata fursa ya kujiunga na elimu ya juu. Hata hivyo, kuanzishwa kwa mfumo huo, kulitokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuwezesha kuanzishwa kwa mfumo wa wananchi kuchangia gharama mbalimbali badala ya serikali kugharimia kila kitu katika elimu, afya na huduma nyingine.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo huo, kwa awamu ya kwanza mwaka 1992, wanafunzi walianza kugharamia nauli za kwenda na kurudi kutoka chuoni, ada za maombi ya kujiunga na vyuo, ada za kuandikishwa chuoni na fedha za tahadhari. Pia wanafunzi walilipia ada za serikali za wanafunzi vyuoni. Baada ya hapo, awamu ya pili ya uchangiaji katika elimu ya juu ilitekelezwa kuanzia Julai 1994.

Pamoja na gharama zilizohamishiwa kwa wanafunzi na wazazi katika awamu ya kwanza, wanafunzi walianza kugharamia pia mahitaji ya chakula na malazi. Kwa kuwa gharama hizo zilionekana kuwa kubwa, serikali ilianzisha utaratibu wa utoaji mikopo kwa wanafunzi kwa ajili ya gharama za chakula na malazi. Uotoaji huo wa mikopo ulianza rasmi katika awamu ya tatu mwaka 2005.

Awamu hiyo ilianza kwa kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ambayo ilianza shughuli zake rasmi Julai, 2005. Katika awamu hiyo ya utekelezaji wa sera ya uchangiaji, wanafunzi wanatakiwa kuchangia katika maeneo yote yaliyobaki ya gharama za elimu ya juu, yakiwemo ya ada za mafunzo, utafiti, mahitaji maalumu ya vitivo na mafunzo kwa vitendo.

Sheria iliyounda bodi ya mikopo, iliainisha majukumu ya bodi ambayo ni kusimamia uendeshaji wa mfuko wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuweka utaratibu wa kuwatambua wahitaji wa mikopo; kupokea, kuchambua maombi yote na kutoa mikopo kwa waombaji wahitaji, na kuweka kumbukumbu za wanafunzi wanaokopeshwa.

Majukumu mengine ni kukusanya marejesho ya mikopo yote iliyotolewa tangu mwaka 1994; kuweka mtandao wa ushirikiano baina ya bodi, taasisi za elimu ya juu, waajiri na wakopaji; na kuishauri serikali kuhusu masuala ya utoaji na urejeshwaji wa mikopo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, anasema kwamba tangu mwaka 2005, HESLB imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Anasema: Katika miaka minane na nusu tangu kuanzishwa kwake, bodi imeimarisha utendaji kazi na imeendelea kuweka mifumo na vitendea kazi ili kusimamia ongezeko kubwa la mikopo.

“Hivi sasa bodi inatoa mikopo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki (mtandao) katika uchambuzi wa mikopo, utoaji mikopo na urejeshwaji wa mikopo. Vile vile waombaji wa mikopo wanatuma maombi yao kwa njia ya mtandao".

Mwaisobwa pia anasema kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi tangu mwaka 1994/1995 ambapo wakati huo kulikuwa na wanafunzi 6,061 pekee waliojiunga na vyuo mbalimbali vya za elimu ya juu lakini sasa wamefikia wanafunzi 233,000. Kati ya hao wanafunzi 98,371 wanapata mikopo.

Mwaisobwa anasema mikopo itolewayo na Bodi imekuwa sababu ya ongezeko la vyuo vya elimu ya juu kutoka 25 vilivyokuwepo mwaka 2004/2005 hadi vyuo 63 mwaka wa sasa wa masomo wa 2013/2014. Tangu wakati huo hadi Desemba mwaka jana, Mwaisobwa anasema mikopo yenye thamani ya Sh 1,843,483,926,686.58 imetolewa.

Anasema katika mikopo hiyo, Sh 51,103,685,914 zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na Sh 1,792,380,240,772.58 zimetolewa na bodi yenyewe kuanzia Julai, 2005 na wanafunzi walionufaika ni 260,150. Pamoja na uchangiaji huo, dhana hii anasema si ngeni katika historia ya Tanzania kwa kuwa mfumo huo ulikuwepo hata kabla ya uhuru.

Anasema kwamba mwaka 1956, serikali ya kikoloni ilianzisha mfuko uliojulikana kama Tanganyika Education Trust Fund, ambao ulitoa mikopo kwa wanafunzi kutoka familia masikini. Utaratibu huu uliendelea hata baada ya uhuru hadi mwaka 1964 lilipoanzishwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Mwaka 1964 hadi 1974, wanafunzi walitumikia katika Jeshi la Kujenga Taifa kwa miezi sita na baada ya hapo walihakikishiwa kupata kazi serikalini. Kwa kipindi cha miezi 18 walilipwa asilimia 40 ya mishahara yao na asilimia 60 iliyobaki ililipwa serikali, kama uchangiaji katika elimu ya juu kwa mwanafunzi husika.

Kupitishwa kwa Azimio la Musoma mwaka 1974, kulileta mabadiliko katika taratibu za ugharamiaji wa elimu wa juu. Muda wa kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa uliongezwa kutoka miezi sita hadi mwaka mmoja. Wanafunzi waliokuwa wakijiandaa kujiunga na elimu ya juu walitakiwa kufanya kazi angalau kwa miaka miwili kabla ya kuanza masomo yao.

Kutokana na utaratibu huo, wanafunzi walitia saini mikataba ya miaka mitano na serikali ili kufanya kazi serikalini baada ya kumaliza masomo kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi sehemu zingine.

Hiyo ilikuwa njia nyingine ya urejeshaji wa gharama za elimu ya juu. Kwa ujumla, mfumo wa uchangiaji elimu na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, umesaidia vijana wengi wa Kitanzania kupata fursa ya elimu katika vyuo vya elimu ya juu nchini.

Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa iliyopo ni namna ya kurejesha mikopo hiyo kwa kuwa baada ya kuhitimu, wengi wamekuwa wakishindwa kuheshimu makubaliano au kuwa wagumu katika ulipaji.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi