loader
Dstv Habarileo  Mobile
Udhalilishaji, mateso yaliyohusishwa na Operesheni Tokomeza

Udhalilishaji, mateso yaliyohusishwa na Operesheni Tokomeza

Wabunge hao wengine walifika mbali na kutaka hata mawaziri husika ambao operesheni hiyo inawagusa, nao ni wakati muafaka wa kujiuzulu kwa kuwa wameshindwa kusimamia operesheni hiyo na matokeo yake ikatekelezwa kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake.

Sokomoko hilo, lilianza pale Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alipotoa taarifa ya Kamati ndogo iliyoundwa na kamati yake kwa ajili ya kuchunguza utekelezaji wa operesheni hiyo ambayo ilizua malalamiko bungeni na maeneo mbalimbali nchini.

Akisoma taarifa hiyo hivi karibuni bungeni, Lembeli alisema Serikali haikuwa na nia mbaya kuanzisha operesheni hiyo kwa kuwa ililenga katika kuwasaka na kuwadhibiti majangili ambayo vitendo vyao vilikithiri na kutishia uhai wa wanyama muhimu kama vile tembo.

Anasema kamati ilibaini kuwa, tatizo la ujangili ni kubwa na limekuwa likisababisha idadi ya tembo iendelee kupungua nchini ambapo takwimu zinaonesha kuwa, idadi ya tembo imepungua kutoka 350,000 (miaka ya 1970) hadi kufikia 55,000 mwaka 1989.

“Juhudi za kukabiliana na hali hiyo kupitia Operesheni zilizowahi kutekelezwa huko nyuma zilisaidia kuongeza idadi ya tembo hadi 141,000 mwaka 2006 ingawa ilishuka tena hadi kufikia 110,000 mwaka 2009,” anasema Lembeli.

Anasema kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, vitendo vya ujangili vinavyofanyika nchini vimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni ujangili wa kujikimu unaohusisha watu wenye kipato kidogo na hulenga zaidi katika kujipatia kitoweo na fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji mengine.

Na ujangili wa biashara ambao huhusisha watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na hulenga kupata nyara zenye thamani kubwa na wanyama wanaoathiriwa zaidi ni tembo, faru, simba na chui.

“Mheshimiwa Spika, taarifa ilibainisha kuwa, kuongezeka kwa masoko haramu katika nchi za Asia na Mashariki ya Kati ambayo yanatoa bei kubwa ya nyara hizo, imekuwa ni chachu ya kuimarika kwa mitandao inayojihusisha na ujangili ndani na nje ya nchi na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la vitendo vya ujangili,” alisisitiza.

Anasema kutokana na hali hiyo ndipo ilipoanzishwa operesheni hiyo tokomeza ambapo katika mpango kazi wake, uliainisha kuwa operesheni hiyo itaendeshwa kwa kufanya uchambuzi wa kina wa watuhumiwa wa mtandao wa ujangili wa nyara za Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu.

Anasema pia mpango kazi huo ulilenga kuwakamata watuhumiwa wote waliobainishwa kwenye taarifa za kiintelijensia, kupiga picha na kuchora ramani ya eneo la tukio kwa kila mtuhumiwa, kuhoji na kuandika maelezo ya watuhumiwa wa ujangili na kukusanya na kuhifadhi vielelezo vyote vitakavyokamatwa kutoka kwa majangili kwa ajili ya ushahidi mahakamani.

Lembeli anasema kutokana na michango na malalamiko ya wabunge wakati wakichangia hoja iliyotolewa na Mbunge wa Sikonge Said Nkumba Mbunge, kuhusu operesheni hiyo, Bunge liliagiza operesheni hiyo isitishwe. Anasema baada ya kusitishwa kwa operesheni hiyo kamati yake ilipewa kazi ya kuchunguza malalamiko hayo ambapo kwanza ilibaini kuwa washiriki wa operesheni hiyo walikuwa 2,371.

Washiriki hao ni kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama kama vile wanajeshi 480 kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), askari 440 kutoka Jeshi la Polisi, askari 440 kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) na askari wanyamapori 383 kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Wengine ni askari 99 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), askari wanyamapori 51 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), waendesha mashtaka 23 na mahakimu 100.

Anasema operesheni hiyo iligawanywa kiawamu na awamu ya kwanza ililenga kusaka silaha za kivita na meno ya tembo kutoka miongoni mwa wanaojihusisha na vitendo vya ujangili wakati awamu ya pili ililenga kusaka silaha zisizomilikiwa kihalali na zile zinazomilikiwa kihalali lakini zinasadikiwa kutumika kwenye vitendo vya ujangili.

Aidha anasema katika awamu ya tatu, yenyewe ililenga kutafuta yalipo maghala ya nyara, kusaka wafadhili na wanunuzi wa nyara hizo na kuwabaini watu wanaowakingia kifua wahusika wa vitendo vya ujangili. Katika awamu ya nne ililenga kukamata nyara nyingine mbali na meno ya tembo na kuhakikisha wawindaji haramu, wavunaji haramu mazao ya misitu, watu wanaolisha mifugo ndani ya hifadhi, na watu waliojenga ndani ya maeneo ya hifadhi wanakamatwa.

Akizungumzia mafanikio ya operesheni hiyo, Lembeli anasema tangu kuanza utekelezaji wa operesheni hiyo jumla ya kesi 687 zilifunguliwa zikiwahusisha watuhumiwa 1,030 katika maeneo yote ambapo kati ya kesi hizo kesi 132 tu ndiyo zilikuwa zimetolewa maamuzi na 555 bado zilikuwa katika hatua ya kusikilizwa.

Pia anasema operesheni hiyo ilifanikisha kukamatwa kwa meno ya tembo 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya ngiri 11, mikia ya wanyama mbalimbali 36, Ngozi za wanyama mbalimbali 21, Pembe za Swala 46, Mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621, baiskeli 58, pikipiki nane na magari tisa.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, anabainisha kuwa operesheni hiyo ilikumbwa na changamoto mbalimbali kama vile vifo vya askari sita na watuhumiwa 13.

“Lakini pia tulibaini kuwa operesheni hii ilikumbwa na vitendo vya hujuma kutoka kwa baadhi ya makundi kama vile kuwepo kwa mamluki miongoni mwa washiriki wa operesheni. “ Mfano; kukamatwa kwa askari Polisi na askari Wanyamapori wakisindikiza gari lenye meno ya tembo, na gari la Serikali kutumika kusafirisha meno ya tembo lakini pia vyombo vya Habari kutumika kuvuruga operesheni kwa kueneza propaganda zilizolenga kushawishi wananchi kupinga operesheni hiyo,” anafafanua.

Akizungumzia eneo la tuhuma dhidi ya operesheni hiyo, Lembeli anasema kuwa ingawa lengo la operesheni lilikuwa ni kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya rasilimali za Taifa, utekelezaji wake ulikumbwa na tuhuma kadhaa zikiwemo mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha maumivu, kupata ulemavu wa kudumu na wengine kupoteza maisha.

Aidha anasema pia operesheni hiyo inadaiwa kuwa washiriki wake walikuwa wakitumia vibaya silaha. “Mfano; Mzee wa miaka 70 kuuawa kwa kupigwa risasi 3, nyumba za wananchi kuchomwa moto na mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na kupigwa risasi.

Anasema pia katika hali ya kutisha, kamati hiyo ilibaini baadhi ya wananchi wakiwemo viongozi, madiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watumishi wa Serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza. “Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walikuwa hawajulikani walipo hadi Kamati ilipozuru maeneo hayo.

Mfano; vijana watatu wa Kijiji cha Osteti, Kata ya Chapakazi, wilayani Kiteto, walituhumiwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo. Vijana hao ni Nyafuka Ng’onja, Ng’onja Kipana na Mswaya Karani lakini hadi leo hii hawajulikani waliko. Anasema pia kamati hiyo ilibaini kuwa baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao.

“Mfano; ndugu Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochang anywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanawe wa kiume (11) akishuhudia. Pia alidai kulazimishwa kuchora picha ya chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake,” anasema.

Anasema pia mkazi wa Babati Neema Mose alidai mbele ya kamati hiyo kuwa alivuliwa nguo na kulazimishwa afanye mapenzi na wakwe zake na kuingizwa chupa sehemu zake za siri. Aidha, anasema baadhi ya akina mama walidai kubakwa na kulawitiwa. Mfano; katika Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga, mwanamke mmoja alidai kubakwa na askari wawili wa Operesheni Tokomeza Ujangili mida ya usiku.

Lembeli pia anasema kamati hiyo ilitaarifiwa kuwa baadhi ya watuhumiwa waliopelekwa katika kambi za mahojiano walidai kuteswa kwa adhabu zinazokiuka haki za binadamu huku akimtolea mfano Diwani wa Kata ya Sakasaka Wilaya ya Meatu Peter Samwel, aliyedai kuadhibiwa akiwa mtupu na kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti.

“Mheshimiwa Spika, kutokana na ukatili uliopitiliza, baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina kama vile Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti),” anasisitiza.

Anasema pia kamati hiyo iliarifiwa na wananchi kuwa kulikuwa na upotevu wa mali katika operesheni hiyo ambapo baadhi ya watuhumiwa walipoteza mifugo, mali na fedha zao na kutolea mfano katika Wilaya ya Ulanga Kata ya Iputi mwananchi mmoja alidai kuporwa sanduku la VICOBA lenye Sh 750,000 na simu ya mkononi na askari wa Operesheni hiyo waliovamia nyumbani kwake.

‘Pia ilidaiwa kuwa mifugo ya watuhumiwa ilikamatwa na kuingizwa ndani ya maeneo ya hifadhi na kufa kwa kupigwa risasi au kukosa maji na malisho kutokana na kuzuiliwa kwa muda mrefu. Baadhi ya mifugo ilitozwa faini bila stakabadhi au stakabadhi kuonesha viwango vidogo ikilinganishwa na fedha halisi iliyolipwa,” anasema.

Anasema baada ya Kamati yake kubaini mapungufu hayo ilimhoji Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki na kubaini kuwa operesheni hiyo ilikuwa ya kijeshi kwa sababu ilitekelezwa kwa amri ya jeshi Namba 0001/13 iliyotolewa tarehe 28 Septemba, 2013 na kusainiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Anasema pia kinadharia inaonekana kwamba, Kagasheki alikuwa Msemaji Mkuu, lakini kiuhalisia hakuwa msemaji mkuu wa Operesheni hiyo.

“Taarifa za mwenendo wa operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja kwa Mkuu wa Majeshi na kwamba, hazikumfikia Waziri wa Maliasili na Utalii,” anasema. “Kamati ilibaini kuwa baadhi ya watendaji wa juu wa Wizara Walidaiwa kukwamisha utekelezaji wa maagizo ya waziri huyo, kutokana na kuingilia mawasiliano aliyokuwa anayafanya na baadhi ya watumishi,” anasema.

Anatoa mfano wa majibizano kwa njia ya barua pepe kati ya Waziri na Katibu Mkuu, Waziri na Mkurugenzi wa Wanyamapori na pia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Wanyamapori ambapo waziri anaonekana kushangazwa na hatua ya Katibu Mkuu kuhoji hatua ya yeye kumuita mmoja wa mtumishi wa wizara ofisini kwake.

Kutokana na mambo ambayo kamati hiyo imeyaibua, Lembeli analiomba Bunge liazimie kwamba Serikali ihakikishe kuwa kuna uwajibikaji wa pamoja pale inapoamua kutekeleza jambo la kitaifa kama Operesheni Tokomeza.

Kutokana na taarifa hiyo, wabunge wengi walionesha kuchukizwa na yaliyojiri katika utekelezaji wa operesheni na kutaka uwajibikaji, ambapo Rais Jakaya Kikwete kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwavua madaraka ya uwaziri, mawaziri wanne waliohusika na operesheni hiyo.

Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk David Mathayo na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki ambaye alijiuzulu kabla.

“Mawaziri hawa hawakutenda kitu chochote lakini tatizo walikabidhiwa sekta hiyo kusimamia, na suluhu ya kisiasa ni wao kuachia ngazi, nimesikiliza kwa makini kuna vitendo vimeoneshwa havikubaliki, mauaji, ubakaji, iko mifugo imeuawa, haya yote hayakubaliki, naelewa nia nzuri ya operesheni hii, ilikuwa ni dhamira ya Serikali tuwakamate majangili ila tatizo ni namna operesheni hiyo iliyotekelezwa na kusimamiwa,” anasema Pinda.

Kwa sasa Serikali iko kwenye mchakato wa kuunda Tume ya kimahakama itakayosimamiwa na Majaji kwa ajili ya kuchunguza tuhuma zote dhidi ya operesheni hiyo ili hatua zichukuliwe zaidi dhidi ya wahusika.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi