loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Udugu wa China, Tanzania waimarika

Uhusiano huo ulianzishwa wakati wa waasisi wa mataifa haya mawili; Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Tse Tung wa Jamhuri ya Watu wa China.

Katika maadhimisho ya miaka hiyo 50 ya ushirikiano huo, Makamu wa Rais wa China, Li Yuanchao alifanya ziara ya siku sita nchini ambayo, licha ya kumfikisha katika hifadhi za Taifa, alifanya kazi nyingine mbalimbali ikiwamo kutia saini mikataba ya ushirikiano na kuzungumza na wawekezaji.

Moja ya kazi alizozifanya Juni 23, mwaka huu ilikuwa ni kuweka jiwe la msingi la Jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), linalokusudiwa kujengwa kwenye kiwanja namba 2217/1/168 Kitalu A, CBD katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kilichopo katikati ya Barabara za Sokoine/Morogoro/ Mansfield/Zanaki, wilayani Ilala.

Kiwanja hiki kipo eneo la Avalon, karibu na Ofisi za Jiji la Dar es Salaam na pia lango la bandari la kuingilia na kushukia meli ziendazo na kutoka Zanzibar. Mradi wa jengo hilo ni ubia kati ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere na CRJE (Estate) Ltd ambayo ni kampuni tanzu ya CRJE (China Railway Jianchang Engineering Company Ltd) ambayo nayo ni Kampuni tanzu ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Wadau wengine wa mradi huu ni International Finance Corporation (IFC) ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya Dunia. Msaidizi Maalumu wa Mkurugenzi Mtendaji wa MNF, Gallus Abedi, amezungumza na gazeti hili kuhusu mradi huu mkubwa na kueleza kuwa awali, taasisi hiyo ilipewa eneo katika kiwanja namba 60 na 61 katika Barabara za Sokoine na Shaaban Robert kwa ajili ya ujenzi wa jengo lao.

“Viwanja hivi tulipewa na Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, baada ya Mwalimu (Julius Nyerere) kuomba tupatiwe kiwanja kwa ajili ya ujenzi. Mwalimu alieleza hilo katika kikao kisicho cha kawaida cha Bodi kilichofanyika Agosti 1996 akiwa Mwenyekiti. “Alilieleza hili katika kikao kingine cha kawaida cha Bodi kilichofanyika Novemba mwaka huo wa 1996.

Kwa hiyo, ilipofika mwaka 2008, kuanza maandalizi ya kuviendeleza viwanja hivi. Taasisi ilikuwa tayari kuanza ujenzi, lakini ikapewa masharti kwamba inaweza kujenga ghorofa tano tu, wakati sisi tulitaka kujenga majengo mawili ya ghorofa 14 na jingine ghorofa 20,” anasema Abedi.

Anasema kutokana na hilo, Rais wa sasa, Jakaya Kikwete alimuagiza aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuwatafutia eneo jingine ambalo halina masharti ya ujenzi.

Mwanasiasa huyo wa zamani anaongeza kuwa baada ya kushughulikia suala hilo, hatimaye Luhanjo aliwapatia kiwanja hicho namba 2217/1/168; na kwamba wakati wakianza maandalizi ya ujenzi wa kiwanja cha awali, walikwisha ingia mkataba na Kampuni ya CRJE (Estate), hivyo wakaendelea nao.

Kwa mujibu wa Abedi, jengo wanalotaka kujenga ni la minara pacha (Twin Towers) linaloendana na mazingira ya sasa na hivyo, hapo watajenga jengo hilo lenye ghorofa 28.

“Makisio ya gharama ya mradi huu ni Dola za Marekani milioni 77 sawa na Shilingi 127,777,650,000,” alieleza Abedi na kuongeza kuwa katika gharama hizo, mgawanyo wake ni dola milioni 55.9 zitatolewa na CRJE (Estate) Ltd na dola milioni 21.8 zitatolewa na IFC,” anasema mwanasiasa huyo wa zamani.

Anasema umiliki wa eneo hilo ni wa miaka 99, na kwamba kwa mujibu wa ubia wao, MNF itanufaika katika maeneo mawili, wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi.

“Wakati wa ujenzi, watakuwa wanatupatia Dola za Marekani 100,000 kila mwaka kwa miaka mitatu yaani dola 300,000 kwa miaka hiyo mitatu na wakimaliza kujenga, watatupatia mita za mraba 5,600 katika jengo hilo,” anafafanua msaidizi huyo maalumu wa Mkurugenzi Mtendaji wa MNF, Joseph Butiku.

Abedi anafafanua zaidi kuwa Taasisi ya Mwalimu Nyerere tayari imeshaamua matumizi ya mita hizo 5,600 za mraba katika jengo hilo. Anasema mita 2,000 zitakuwa kwa ajili ya ofisi na mita 3,600 zitapangishwa kwa ajili ya kupata fedha za kujikimu za Taasisi hiyo iliyoanzishwa Juni, 1996.

Anayataja matumizi hayo ya mita zao 2,000 kuwa ni ofisi za utawala, programu za taasisi na uhasibu, maktaba ya MNF, maonesho na nyaraka za kazi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kumbi za mikutano.

“Pia kutakuwa na Taasisi ya Mafunzo ya Viongozi. Zamani mafunzo kama haya yalikuwa yanatolewa na Chuo cha Kivukoni, lakini sasa hata Uongozi Institute hawatoi mafunzo haya, kwa hiyo tutakuwa na mafunzo hayo maalumu kwa viongozi,” anafafanua Abedi aliyewahi kuwa Mkuu wa mikoa kadhaa nchini.

Anasema katika kitako cha jengo hilo kutakuwa na sehemu ya maegesho ya magari na pia kutakuwa na podium sita, ambazo ndimo mtakuwa na ofisi zao pamoja na zile maalumu za kupangisha.

“Kuanzia ghorofa ya sita kwa kila mnara, kutakuwa na hoteli yenye vyumba 250, hii itakuwa hoteli ya five star (nyota tano) ambayo itaendeshwa na kampuni maarufu ya hoteli ya Rotana Hotel Management Corporation ya Dubai,” anasema Abedi na kuongeza: “Eneo lote hili kwa minajili ya kujulikana kwake na kuwa na trademark (alama ya kibiashara), litajulikana kama The Mwalimu Nyerere Foundation Square.”

Kwa mujibu wake, makubaliano ya ubia wa mradi huu ni BOT (Build, Operate and Transfer) yaani Wekeza fedha, Jenga, Endesha na Kabidhi kwa mwenyewe, na utakuwa wa miaka 40.

Anasema tofauti na miradi mingine ya BOT, katika mradi wao huo wa Jengo la MNF, wamepewa ofisi ndani ya jengo husika na eneo walilopewa ni kubwa kufikia baadhi ya majengo mapya yaliyojengwa au yanayoendelea kujengwa sasa katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi, Mkurugenzi Mtendaji wa MNF, Joseph Butiku anasifu ushirikiano kati ya Tanzania na China na kwamba kuwapo kwa Makamu wa Rais wa China katika shughuli hiyo ni kielelezo cha uungaji wao mkono juhudi za Taasisi hiyo, Tanzania na Afrika kwa ujumla, kuendelea, kuimarisha na kulinda uhuru na usawa.

Butiku anaishukuru Serikali kwa kuwapa kiwanja cha kuendeleza mradi huo, akitoa pongezi maalumu kwa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyeanzisha juhudi za kuwapatia ardhi katika kiwanja cha awali.

Anasema Taasisi ya Mwalimu Nyerere imedhamiria kuendelea kujikita na Serikali na watu wa China, katika urafiki wao na kuunga kwao mkono juhudi za maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa misingi ya maslahi kwa pande zote, na kuheshimiwa uhuru na utu wa nchi hizi mbili.

“Ni katika dhamira hiyo, kwamba tunaamini mradi huu sio tu utanyanyuana kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na China, lakini pia utakuwa wa manufaa kwa Taasisi na CRJE (East Africa) Ltd,” anasema Butiku. Taasisi ya Mwalimu Nyerere, mbali na kuendeleza mambo yalioanzishwa na kusimamiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, imekuwa ikijielekeza katika kuimarisha amani, upendo, utawala bora na maendeleo kwa jamii ya Watanzania, Afrika na dunia nzima.

Kwa upande wake, Kampuni ya China Railway Group Limited imeahidi kwamba utakuwa mradi wa daraja la juu katika menejimenti, ubora, ufanisi na teknolojia.

Katika hotuba yake, Rais wa kampuni hiyo, Dai Hegen anasema mbali ya kujenga jengo hilo kwa kuzingatia ubora, ufanisi, teknolojia na uzoefu, kampuni hiyo itaisimamia kampuni yao tanzu vizuri kupanua biashara zake nchini Tanzania, ili kuwa na maendeleo mazuri na kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania.

“Inaaminika kwamba kwa kufanikiwa katika uhusiano huu, tutakuwa na uzoefu katika kusaka fursa zaidi kwa jamii ya Tanzania na tutaendelea kuiunga mkono CRJE, kampuni yetu ya hapa nchini, kupanua biashara zake Tanzania, na kwa hiyo, kuimarisha uhusiano mwema kati ya China na Tanzania,” anasema Dai.

Anasema litakapokamilika, litakuwa na miundombinu bora ya kibiashara ya kuvutia wawekezaji zaidi na watalii nchini Tanzania, na pia kutengeneza fursa zaidi za ajira kwa jamii ya Tanzania. Dai anasema Jengo la MNF ni mradi mkubwa wa kwanza kwa China Railway kuwekeza katika Afrika Mashariki. Kampuni hiyo ni miongoni mwa kampuni kubwa za kimataifa za ujenzi duniani.

Anasema CRJE East Africa Limited, ni kampuni tanzu inayomilikiwa na China Railway, na ambayo ilikuja Tanzania wakati wa ujenzi wa Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) katika miaka ya 1970.

“China Railway imeshuhudia historia ya kuvutia ambayo nchi zetu mbili zimekuwa zikiheshimiana, kuaminiana na kuungana mkono kila moja. Udugu huo wa kudumu pia umetusaidia kupata mafanikio makubwa hadi sasa,” anasema Rais huyo wa kampuni hiyo ya China.

Kama kuna sherehe ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyohudhuriwa na viongozi mashuhuri kwa wakati mmoja, basi uwekaji wa jiwe la msingi la jengo hilo la Mwalimu Nyerere Foundation Square, iliweka rekodi.

Ukiondoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Li Yuanchao ambao walishirikiana katika kuweka jiwe hilo la msingi, walikuwapo marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, pamoja na waliowahi kuwa mawaziri wakuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba na John Malecela.

Si hao, walikuwapo waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, wadhamini wa MNF, watendaji wa CRJE (Estate), IFC, Al-Hatimy ambao ni wasanifu wa jengo hilo na Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta.

Wengine ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amir Manento, mabalozi, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Nape Nnauye, Sir George Kahama, Balozi Christopher Liundi na Mzee Pancras Ndejembi na viongozi wengine wa kada mbalimbali.

foto
Mwandishi: Mgaya Kingoba

Post your comments