loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ugonjwa wa kisukari ni hatari, hauchagui umri

Hivi sasa tafsiri ya ugonjwa wa kisukari duniani kote ikiwemo Tanzania, unahesabiwa kuwa ni mama wa magonjwa yote. Daktari yeyote aliyesomea udaktari anapaswa kujua kuwa hata yeye anaweza kuugua kisukari.

Ni haki yako mwananchi na ni wajibu wako kupata taarifa iliyo kamili na sahihi. Usidanganyike, Babu wa Loliondo amewabamiza na kuwaumbua wasomi, wanataaluma, viongozi wa dini na serikali na umma wote kwa ujumla, duniani kote kuwa anatiba ya magonjwa sugu, kisukari, saratani, Ukimwi na upungufu wa nguvu za kiume.

Narudia mama wa magonjwa yote duniani ni KISUKARI. Haina maana kisukari kinaleta Ukimwi, bali mwenye ugonjwa wa kisukari kinga yake ya mwili inapungua, na ana uwezekano wa kuugua magonjwa lukuki ikiwemo ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Kwa lugha nyingine unaugua Ukimwi bila virusi vya Ukimwi mwilini mwako.

Lakini Mungu apishilie mbali unapata Ukimwi (VVU) na huku una ugonjwa wa kisukari, hapo mambo yatakuwa mazito. Kwa bahati mbaya Mungu awasaidie wagonjwa wote wenye kisukari, Ukimwi, kifua kikuu na presha, na wengine wanakuwa na saratani.

Magonjwa kama hayo yote sugu kasoro kifua kikuu (tiba ya kifua kikuu ipo na inajulikana na inapatikana) ndiyo yaliyovuta hisia na uamuzi wa umma wa Tanzania na nje ya Tanzania kujikita Samunge kwa babu.

Tiba ambayo haikuwa sahihi. Unapougua kisukari usitafute mchawi na usiogope kuijulisha familia yako, ndugu jamaa na marafiki zako, usijinyanyapae kwa ugonjwa ambao ushahidi upo unaweza kuishi na maisha yako yakawa ya kawaida bali ufuate miiko, masharti, maagizo na dawa za kutumia bila kukosa.

Kama huna kisukari hakikisha unabadili mfumo wa maisha yako kuepuka gonjwa hilo. Aina za kisukari ziko mbili kuu. Aina ya kwanza (type 1 diabetes) inawapata watoto na vijana, na aina hii ya kisukari ima faima lazima mgonjwa apewe homoni ya insulini kwa kudungwa au kujidunga yeye mwenyewe sindano hiyo katika uhai wake wote.

Kisukari cha aina ya kwanza hujitokeza pale kinga yako ya mwili inapoharibu seli za kongosha lako (ziitwazo beta cells) ambazo hutengeneza homoni ya insulin yenye uwezo wa kurekebisha matumizi ya sukari mwilini mwako.

Ni asilimia 5 hadi 10 ya watu huugua kisukari aina ya kwanza. Aina ya pili (type 2 diabetes) ugonjwa huu wa aina yake upo kwa wingi wa asilimia 90 hadi 95 ya watu wanaoishi na kisukari.

Ni ugonjwa ambao mtu anaukokota katika maisha yake jinsi anavyoishi, kwa maraha yake na utashi wake.

Kisukari cha aina hii hujitokeza wakati kongosho lako linashindwa kutengeneza homoni ya insulin kwa wingi, au usishangae seli zako zenyewe zinaweza kuisusia hiyo insulin (ikashindwa kunaswa kwenye seli zako).

Somo hili ni tata kidogo kwa wale ambao hawakujifunza bayolojia ya kongosho na utengenezwaji wa homoni ya insulin.

Kuna baadhi ya mafundi na waganga wa jadi wanatamka kuwa bandama (spleen) hutengeneza insulin. Na hayo wanayasema kwenye runinga na radio na mtangazaji anasikia kwa kuwa bayolojia halikuwa somo lake anamezea wakati yule mtu ana zungumza utumbo (uongo uliokithiri na yeye pia huyo fundi hakusoma bayolojia ameghushi taaluma hiyo).

Bila ya kuwa na homoni ya insulin huwezi kumeng’enya, kusafirisha na kusharabu sukari yako (glucose) mwilini mwako hata kidogo, lazima insulin iwepo. Mwili wako unavunja vunja vyakula vyote tunavyokula hususan vya wanga (carbohyrdrates) ili sukari aina ya glucose ipatikane.

Aina hiyo ya sukari ya glucose ndiyo nishati yako (kama vile petroli au dizeli) ambayo seli zako za mwili mzima unategemeaglucose hiyo ili uweze kuishi na kufanya kazi. Wakati glucose inapokaa na kulundikana kwenye damu yako badala ya kuingia kwenye seli zako, hapo ndipo kisukari hujitokeza. Dalili za kisukari ni mlimbiko dalili wa kadhia nyingi kama: kupata haja ndogo kwa wingi na mara kwa mara hata usiku mtu huamka zaidi ya mara tatu au nne, kusikia kiu sana, kusikia njaa sana, kuishiwa nguvu, kukonda, kupungua uzito ghafla, kupungua uwezo wa macho kuona, kuwa na vidonda visivyopona, kupungua kwa nguvu za kiume, muwasho mwilini na kadhalika.

Utakapopima damu yako kwa sukari na au ukapimwa mkojo ukawa na sukari au bila sukari, lakini kipimo cha damu kitakuwa sahihi kujua una kiwango gani.

Kwa kuwa kote duniani huadhimisha siku ya ugonjwa huu kila ifikapo Novemba 14, badala ya kusubiri kupata taarifa sahihi ufikapo wakati huo, ni vyema watu wakazidi kuelimishwa juu ya ugonjwa huu.

Ni matumaini yangu kuwa wananchi watasikia mengi kutoka kwa wataalamu waelekezi wa ugonjwa wa kisukari, kwenye vyombo vya habari, ikiwemo magazeti, radio, televisheni na vipeperushi mbali mbali.

Baadhi ya matatizo yanayojitokeza kwa wagonjwa wanaougua kisukari duniani kote ambayo yanaonekana kwa dhahiri ni watu kukatwa miguu yao kwa kuwa na vidonda miguuni kwa muda mrefu na misuli yao, mishipa ya damu na neva kufa.

Madonda hayo hutoa harufu mbaya sana na hatima yake ni watu zaidi ya milioni moja duniani kote hukatwa miguu yao. Kadhia hiyo huitwa gangrene (gangrin). Tiba yake ni kukatwa kiungo hicho na kuacha sehemu ambayo itaweza kuishi.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Dk Ali Mzige

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi