loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uharamia wapunguza meli zinazoingia Tanzania

Tangu karne hiyo uharamia umekuwa ukitokea katika maeneo mengi hapa duniani. Hadi sasa uharamia upo na unaendelea kuenea katika sehemu nyingi za dunia na hivyo kusababisha hasara kubwa ipatayo Dola za Kimarekani bilioni 13 – 16 kwa mwaka.

Mwanzoni kabisa uharamia ulikuwepo na ulizoeleka katika maeneo kati ya Bahari ya Pacific na Bahari ya Hindi, South China Sea, Ghuba ya Guinea. Strait of Malaca na Singapore ambapo maeneo haya yanahudumia meli za kibiashara zaidi ya 50,000 kwa mwaka.

Lakini miaka ya karibuni uharamia umeibuka kwa kasi kubwa katika maeneo ya Ghuba ya Aden na ukanda wa Somalia. Kuna uharamia wa aina mbili ambao ni uharamia wa kupora meli na huu hutokea katika Ghuba ya Guinea.

Uharamia mwingine ni ule wa kudai kigombozi ambao ulianza kutokea Ghuba ya Aden na Ukanda wa Somalia na sasa umeenea katika ukanda wa mashariki mwa Afrika wa Bahari ya Hindi.

Ghuba ya Aden ni mlango wa meli za kibiashara zinazotoka au kwenda katika mabara ya Asia na Afrika na kwenda au kutoka mabara ya Ulaya na Amerika. Aidha Ukanda wa Somalia ni sehemu ya Bahari ya Hindi inayopitisha mizigo kwa wingi kuja Afrika kutoka mabara mengine.

Uharamia katika maeneo haya umekuwa ni tishio kwa usafirishaji wa kimataifa (International Shipping) tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka ya 1990. Serikali ya Siad Barre (1969- 91) ilipata msaada kutoka nchi za Ulaya ili kuendeleza uvuvi.

Baada ya kuanguka kwa serikali yake mwaka 1991, mapato ya uvuvi yalipungua. Wavuvi wadogo wadogo waligeuka na kuwa maharamia wakilalamika kuwa meli za kigeni za uvuvi zinatishia maisha yao na wao wakasema kwamba “kama hatuwezi kuvua samaki basi tutavua wavuvi wa kigeni”.

“Hivi ndivyo uharamia ulivyoanza kama njia ya kulinda maji yao kabla wana mgambo na wafanya biashara hawajaanza kushiriki,” anaeleza Mkuu wa Kamandi ya Wanamaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Said Shaaban Omar.

Anasema kipato kikubwa kinachotokana na uharamia kimevutia vikundi vingi vya vijana wa kisomali kujiingiza katika uhalifu huo na kuna mambo mengi ambayo yamechangia kuwepo kwa uharamia katika maji ya Somalia.

“Kwanza mizizi ya uharamia ni kuanguka kwa serilali ya Siad Barre, mengine ni ugumu wa maisha ya Wasomali, uchafuzi wa mazingira na moyo wa kijasiriamali wa Wasomali,” anaeleza.

Uharamia Somalia na sehemu nyingine umepata kasi kubwa ikiwa kama njia ya kujipatia kipato kikubwa na kwa haraka kuliko njia nyingine yoyote. Anasema wakati uharamia ni kitendo cha madhara, lakini faida yake ina uzito mkubwa ukilinganishwa na madhara hayo.

Aidha anasema umasikini, ukosefu wa ajira, kipato kidogo, upungufu wa mifugo na maliasili za baharini kutokana na ukame, uvuvi haramu na hali ya kisiasa vyote vimechangia kuibuka na kuendelea kwa uharamia katika maji ya Somalia.

Kuibuka kwa uharamia katika pwani ya Somalia na baadaye kusambaa kwenye maeneo mengine kumeweka sura mpya ya majukumu ya Jeshi la Wanamaji, sio kwa Tanzania pekee bali nchi nyingi duniani.

Kabla ya mwaka 2010, matukio mengi ya uharamia yalikuwa yakitokea katika ukanda wa maji ya Somalia na Ghuba ya Aden. Matukio hayo yalienea hadi nje kufikia kiasi cha maili za bahari zaidi ya 1,000 kutoka nchi kavu na huku yakizisogelea nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi upande wa Kusini mwa Somalia ikiwemo Msumbiji, Kenya na Tanzania.

“Hali hii ya kuenea kwa vitendo vya kiharamia katika maji yetu yalitokana na uwepo wa majeshi ya wanamaji ya kigeni katika Ghuba na Somalia. Maharamia waliona wahamie kwenye maeneo yaliyonekana kupwaya kiulinzi,” anaeleza.

Anasema hadi kufikia mwaka 2011, maharamia waliweza kuteka meli 25 na kushikilia idadi ya mateka 601 katika ukanda wa Somalia. Katika kufanya uhalifu huo maharamia wamekuwa wakiteka meli kubwa na kuzitumia kama meli za vituo vyao vya kushambulia (Attacking Ships/ Mother Ships).

Meli hizo zilizokuwa zinatumika ambazo kwa sasa zimeachiliwa huru ni pamoja na LPG Tanker YORK, MT MOTIVATOR, MT HANNIBAL II, MV IZUMI, MV POLAR na MV GEMIN.

Anasema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwaka 2010 inaeleza kwamba mashambulizi ya uharamia yaliongezeka kwa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2009 ambapo zilitolewa taarifa za uharamia 440 ikilinganishwa na taarifa 404 za mwaka 2009.

Anasema Uharamia katika maji ya Tanzania ulianza Januari 2010 na kushamiri zaidi Machi 5, 2010 ambapo maharamia waliweza kufanikiwa kuteka meli ya kwanza ijulikanayo kama MV UTB OCEAN.

“Hadi kufikia Desemba 2010, yalitokea matukio 29 ya uharamia ambapo manne yalifanikiwa, ishirini yalitolewa taarifa, katika matukio matatu likiwemo shambulizi la meli yetu MCHONE lililotokea Septemba 25, 2010,” anasema.

Anaeleza kwamba katika matukio hayo maharamia 12 walikamatwa na askari wa hapa nchini na matukio mengine mawili yaliingiliwa na meli vita za kigeni.

“Kuanzia Januari 2011 hadi Juni 2011, jumla ya matukio matano yalitokea katika maji yetu, kati ya haya moja lilifanikiwa la kuteka meli ya mv Gemini umbali wa maili za Bahari zipatazo 125NM (Km 232) kutoka Dar es Salaam na matukio manne yalitolewa taarifa,” anaeleza.

Aidha kuanzia Julai 11 hadi Septemba 11 ulikuwa ni msimu wa upepo mkali ambapo ni vigumu kwa boti ndogo zinazotumiwa na maharamia kuweza kuingia baharini na kufanya kazi na hivyo kukifanya kipindi hicho kuwa cha likizo kwao.

Matukio ya uharamia yameongezeka kwa kasi hasa baada ya kumalizika kipindi hicho ambapo kwa muda mfupi wa mwezi mmoja wa Oktoba 2011 yametokea matukio manne mfululizo.

Katika tukio lililotokea Oktoba 3, 2011 meli ya kampuni ya kuchimba mafuta ya MV SAM-S ALLGOOD ilivamiwa maili 20(37km) kutoka Mafia ambapo askari waliwakamata maharamia saba eneo la uchimbaji mafuta ambapo Oktoba 6, 2011 meli ya mv Kota Nasrst ilivamiwa maili za bahari 166(300km) kutoka bandari ya Dar es Salaam.

Oktoba 17 ilivamiwa meli ya MT GAS BALI maili za bahari 20(37km) kutoka Pemba ambapo pia mv Emirate Zambezi ilivamiwa Oktoba 18, 2011 Maili za Bahari 34 (62 KM) kutoka Kisiwa cha Unguja.

Anasema vitendo vya Uharamia katika eneo la maji yetu vimeleta athari za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja katika ulinzi, usalama na zaidi uchumi wa nchi kushuka.

Upande wa uchumi wa Tanzania, bandari ambazo ni njia kuu za biashara za kimataifa hazipokei mizigo kama ilivyokuwa awali kabla ya uharamia kutokana na Meli kubwa za kibiashara za kimataifa kuogopa kuja Tanzania kwa kuhofia kutekwa.

“Pamoja na kujitahidi kutekeleza majukumu yetu lakini Kamandi ya Jeshi la Wanamaji bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali za kiutawala na kiutendaji ikiwemo ukubwa wa eneo la bahari na mtawanyiko wa maziwa yetu,” anasema.

Changamoto nyingine ni upungufu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na kutokuwa na meli za kutosha na zenye uwezo wa kudhibiti maeneo yetu ya ulinzi. Nyingine ni ufinyu wa Bajeti ya Uendeshaji wa Jeshi la Wanamaji, mbinu mpya zinazotumiwa na maharamia kama vile kutumia meli za uvuvi na meli zilizotekwa kama uhalifu mwingine baharini na maziwani.

Changamoto nyingine ni ufahamu mdogo kwa watanzania kuhusu maliasili zilizopo baharini na umuhimu wa ulinzi imara, kuongezeka kwa dharura au majanga baharini, maziwani na kwenye mito na uwezo mdogo katika kukabiliana nayo.

Kutokana na hayo kuna umuhimu mkubwa wa Kamandi ya wanamaji nchini kulinda mipaka ya maji na maliasili zake. “Kunahitajika kuimarisha Jeshi la Wanamaji ili liweze kukabiliana na majukumu yake na hasa kipindi hiki cha matishio. Ni dhahiri kwamba uvunaji mzuri wa maliasili za baharini unatokana na ulinzi imara wa bahari na hakuna ulinzi imara bila vifaa,” anasema.

Mahitaji ya ulinzi katika bahari yanaongezeka kwa kasi sana kwa mfano, sasa hivi makampuni mengi ya uchimbaji mafuta yanafanya shughuli hizo Tanzania. Sasa hivi kampuni za Petrobrass na BG wameanza kwa kasi jambo ambalo linahitaji ulinzi muda wote.

“Kushindwa kwetu jukumu hili kunakaribisha uwezekano wa matumizi ya makampuni binafsi ambayo yanachipua siku hadi siku. Hali hii ni hatari kwa usalama wetu. Ni wazi kwamba jukumu la ulinzi wa bahari lazima litekelezwe na JWTZ” anaeleza.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Hellen Mlacky

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi