loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uhuru Marathoni ni zaidi ya mbio

Amani ya Tanzania imejengwa kwa miaka mingi, hivyo sio kitu cha kuichezea kwani inaweza kutoweka mara moja endapo Watanzania hawatakuwa makini kuilinda. Katika kuhakikisha amani hiyo haichezewi wala kuharibiwa na mtu yeyote, waandaaji ambao wamekuwa wakiandaa mbio hizo za marathoni za Uhuru, mwaka huu wameamua ziwe na ujumbe huo wa kuimarisha na kuitunza amani ya nchi.

Tayari baadhi ya watu au vyama vya siasa kwa njia moja ama nyingine vimeanza kuichezea amani ya nchi yetu iliyotafutwa na kuimarishwa kwa miaka mingi iliyopita.

Uhuru Marathoni:

Kwa mujibu wa Mratibu wa mbio hizo za Uhuru Marathoni, Innocent Melleck, mbio za mwaka huu zimepangwa kufanyika Desemba 7, mgeni rasmi akiwa ni Rais Jakaya Kikwete. Mbali na Rais Kikwete, pia Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Dk Mohammed Gharib Bilal na Mizengo Peter Pinda, watashiriki katika mbio maalumu za kilometa tatu ambazo ni kwa viongozi.

Mwaka jana, mbio hizo zilifanyika kwa mara ya kwanza na kushirikisha wakimbiaji 2,146 wakati mwaka huu wanatarajia kushiriki zaidi ya wakimbiaji 20,000 na tayari 10,000 wameshajiandikisha. Mshindi wa mwaka jana katika mbio za kilometa 42 kwa upande wa wanaume alikuwa ni Jamin Ikai wa Kenya.

Mwaka jana, fomu za kushiriki zilikuwa Sh 2,000 kila moja, lakini mwaka huu fomu hupatikana kwa Sh 500 tu, lakini kwa wale wanaotaka kushiriki mbio za kilometa tatu wanatakiwa kulipia Sh 100,000 kwa fomu. Melleck anasema kuwa fomu za kilometa tatu zinatolewa kwa Sh 100,000 kwa kuwa ni mbio maalumu ambazo zitashirikisha viongozi wa kitaifa pamoja na wale wa taasisi mbalimbali hapa nchini.

Mbio za Uhuru zina uhusiano na zile za Marekani zenye umaarufu mkubwa za Boston Marathoni ambazo hufanyika kila mwaka. Mbio za mwaka huu zitakuwa zikizinduliwa katika mikoa tofauti, ambapo jijini Dar es Salaam zinatarajia kuzinduliwa Septemba mosi katika nyumba ya Baba wa Taifa, Mwalimu JUlisu Nyerere, Msasani jijini Dar es Salaam.

Melleck anasema kuwa katika uzinduzi huo, Mama Maria Nyerere naye atakuwepo katika uzinduzi huo maalumu kwa ajili ya kuimarisha amani na mshikamano hapa nchini.

Baadhi ya changamoto:

Katika mwaka wa kwanza wa mbio hizo, mwaka jana kulikuwa na baadhi ya changamoto, ambazo zilijitokeza kutokana na uchanga wa mbio zenyewe, lakini mwaka huu wamepania kuzishughulikia changamoto hizo ili kuboresha zaidi.

Baadhi ya changamoto zenye ni pamoja na uhaba wa maji barabarani na hivyo kuwafanya wanariadha kupatwa na kiu kali na kutokuwa na wasimamizi wa kutosha kwa ajili ya kuwaonesha njia wakimbiaji. Mwaka huu, kutakuwa na vituo vingi vya kugawa maji kwa washiriki hivyo hakutakuwa na usumbufu kama ule uliojitokeza mwaka jana.

Kingine ni kwa waandaaji kutomleta mwanariadha wa kike ambaye ni bingwa wa dunia, Mkenya Edna Ngeringwony Kiplagat licha ya kutangazwa sana kuwa mwanariadha huyo atakuwepo katika mbio hizo. Hata hivyo, Melleck anakiri changamoto hizo huku akisisitiza kuwa mwaka huu mwanariadha huyo atakuwepo pamoja na nyota wengine kibao kutoka nchi mbalimbali.

Pia kingine ni kwa washindi wengi wa mbio hizo ukiondoa yule wa mbio za kilometa 21, Jackline Sakilu ambaye alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za umbali huo, walikuwa ni wanariadha kutoka Kenya. Anasema kuwa ushiriki wa wakimbiaji wa nje ni muhimu sana kuwepo ila kinachotakiwa ni kwa wanariadha wa Tanzania kujiandaa vizuri ili kukabiliana na ushindani huo kutoka nje ya nchi.

Pia uwepo wa wanariadha wa nje huongeza changamoto kwa wanariadha wa Tanzania nao kufanya vizuri katika mashindano hayo baada ya kufanya maandalizi ya uhakika. Changamoto nyingine ambayo ni ya kifundi iko kwa Riadha Tanzania (RT) ambao licha ya kulipwa fedha na waandaaji wa Uhuru Marathoni, lakini bado walijiweka kando katika uendeshaji wa mbio hizo.

RT kupitia Kamati yao ya Ufundi walitakiwa kusimamia mbio hizo kwa upande wa ufundi, lakini hawakufanya hivyo. Pia mwaka huu waandaaji wa mbio hizo wanatarajia kuwalipa RT fedha ili wasimamie mbio hizo, ambazo zinakuwa kwa kasi sana.

Maandalizi muhimu:

Kwa kuwa wanariadha wa Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya vibaya katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, waandaaji wa Uhuru Marathoni tayari wana mpango wa kuanzisha kituo cha michezo kwa ajili ya kuwalea wanariadha chipukizi.

Shule hiyo inatarajia kuzinduliwa rasmi kabla Rais Kikwete hajaondoka madarakani mwakani. Kituo hicho kitasaidia kuwaandaa wachezaji au vijana kabla hawajashiriki mashindano yoyote ili wafanye vizuri katika mashindano husika.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi