loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ujue ugonjwa wa homa ya vipindi, kujikinga

Mwishoni mwa mwezi Januari hadi sasa, idadi ya wagonjwa ambao wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huo ambao pia hujulikana kama kidingapopo ni 144, huku mmoja akipoteza maisha. Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donan Mmbando, anasema Wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na asilimia 91 ya wagonjwa wote ambao ni 132 huku Ilala ikiwa na wagonjwa wanane na Temeke wanne.

Anasema kuwa mgonjwa aliyefariki dunia, alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 22 na alikufa baada ya kutoka damu nyingi puani na sehemu za wazi. Ugonjwa huo unaonekana kukua kwa kasi kutokana na ukweli kwamba mara ya mwisho wizara kutoa taarifa ilikuwa Machi 25, mwaka huu ambapo kulikuwa na wagonjwa 70 pekee.

Anasema kata zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo ni Mtoni, Tandika, Yombo, Mabibo, Sinza, Temeke, Mikocheni, Manzese na Msasani ambapo wanawake walioathirika ni 64 na wanawake 80 huku ukiathiri zaidi watu wenye umri wa zaidi ya miaka 15 ambao ni 131. Dk Mmbando anauelezea ugonjwa huo kuwa ni ugonjwa unaosababishwa na kimelea kinachoenezwa na mbu aina ya Aedes.

Anazitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu ambapo dalili hizo huanza kujitokeza katika siku ya tatu na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya vipindi.

“Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na zile za malaria, hivyo wananchi wakipata homa wanatakiwa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria au la ili hatua stahiki zichukuliwe,” anasema.

Anasema vimelea vya homa ya vipindi vinaenezwa kwa binadamu baada ya kuumwa na mbu aina hiyo ambao hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Anasema viluwiluwi vya mbu hao, huweza kuishi katika mazingira ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu, na kwamba mbu aina ya Aedes wana tabia ya kuuma wakati wa mchana.

Mganga Mkuu huyo wa serikali anasema ugonjwa huo hauenezwi kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine na unaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.

“Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa huu wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu,” anasema na kueleza bayana kuwa endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, anaweza kupoteza maisha.

Dk Mmbando anasema kuna aina tatu tofauti za ugonjwa huo ambazo ni homa ya vipindi (Dengue Febrile Illness) ambayo huambatana na dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo na uchovu.

Aina ya pili ni Homa ya Vipindi ya Damu (Dengue Haemorrhagic Fever) ambayo huambatana na kutokwa damu kwenye fizi au puani pamoja na kutokwa damu chini ya ngozi ambapo mgonjwa akiumia sehemu yoyote atapoteza damu nyingi kupitia michubuko.Dk Mmbando anaeleza aina ya tatu ya ugonjwa huo kuwa ni Homa ya Vipindi ya kupoteza fahamu (Dengue Shock Syndrome) ambayo huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi na kupoteza fahamu.

Anasema aina ya pili na ya tatu ni zenye dalili za hatari kwa maisha ya mgonjwa, lakini nchini hadi sasa ni aina ya kwanza pekee ndiyo imeripotiwa. Dk Mmbando anasema jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo ni kwa kuangamiza mazalio ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi.

“Pia ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo na vinginevyo huku ukifyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu,” anasema.

Anasisitiza kuwa ni vema kuhakikisha maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara na kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama Pia ni vema wananchi wakajikinga na kuumwa na mbu kwa kutumia dawa za kufukuza mbu, kuvaa nguo ndefu, kutumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana) pamoja na kuweka nyavu za kuzuia mbu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.

Mganga Mkuu anasema wizara baada ya kubaini kuibuka kwa ugonjwa huo imechukua hatua za kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi. Pia wameimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani.

“Aidha uchunguzi wa ugonjwa huu utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa ya vipindi,” anasema. Vile vile Wizara imetuma vipeperushi vya ugonjwa huo katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.

Anasema pia wametoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani kuhusu namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana na vimelea vya ugonjwa huo.

Dk Mmbando anasema wameimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa homa ya vipindi uliopo kwenye vituo maalumu na kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwadhibiti.

Anasema wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu bali wanashauriwa kwenda katika vituo vya tiba mara mnapoona dalili. Anasisitiza kuwa ugonjwa huo si mpya kwani mara ya kwanza kugundulika kuwepo kwa ugonjwa huu nchini ilikuwa ni Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu waliothibitika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40.

Pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huo na kwamba hakuna mgonjwa aliyepoteza maisha. Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na kwamba wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.

Dk Mmbando anasema kumekuwa na changamoto mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo na vitendanishi vya kuainisha ugonjwa huu kwa ngazi za chini.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi