loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ukawa waige ustahimilivu na busara za Wapalestina

Ukawa waige ustahimilivu na busara za Wapalestina

Hiyo ni kauli ya Dk Saeb Erekat, mpatanishi mkuu wa Palestina katika mgogoro unaowahusu wao na taifa la Kizayuni la Israel ambao umedumu kwa nusu karne sasa.

Dk Erekat aliitoa kauli hiyo katika kipindi cha ‘Head to Head’ kinachorushwa na runinga ya Al- Jazeera mara baada ya mtangazaji wa kipindi hicho, Mehdi Hasan, kumuuliza mpatanishi huyo kwa nini ameendelea kukaa meza moja kwa takribani miongo miwili na watu wanaoua Wapalestina huku matumaini ya kufikia suluhisho la kuwa na nchi mbili likionekana kutofanikiwa na kuwa kama ndoto.

Dk Erekat ambae amewahi kujiuzulu katika nafasi hiyo mara nane, alionesha kupinga kujitoa moja kwa moja katika majadiliano hayo licha ya kwamba wao hawaitambui Israel (hawana imani nayo) na kusisitiza kamwe hawatatambua uwepo wa taifa hilo katika ardhi ya Wapalestina ambao ulifanyika katika vita ya mwaka 1967.

Anaamini licha ya changamoto kubwa wanazozipata katika kutafuta suluhu ya kudumu ya kuutanzua mgogoro baina yao, lakini kupitia majadiliano wanaamini kuwa ndio njia sahihi ya wao kufanikiwa kama walivyofanikiwa kwa taifa hilo kupandishwa hadhi kwenye Umoja wa Mataifa (UN) kutoka nafasi ya taasisi mwanachama mtazamaji asiye na haki ya kupiga kura na kuwa nchi mtazamaji isiyo mwanachama.

Narejea hapa nyumbani ambako kuna mkwamo wa kisiasa kuhusiana na kupatikana kwa katiba mpya ambapo wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wana mgogoro na wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chama kinachotawala, ambao wanashutumiwa na Ukawa kuhodhi mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba hiyo, hususani kipengele cha muundo wa muungano, aidha wa serikali mbili am tatu.

Wakati ngwe ya pili ya Bunge Maalum la Katiba ikiwa imeshaanza kunang’oa nanga tangu Agosti 5, baadhi ya abiria ambao ni muhimu katika safari hiyo kubwa ya kuelekea katika ujenzi na mustakabali mpya wa taifa letu la Tanzania hawamo ndani yake. Wao wamebaki majumbani mwao, wanawaangalia wanaosafiri.

Hii ni safari ambayo imekuwa ikililiwa na kusubiriwa kwa miongo kadhaa ikiaminiwa kuwa ndio itatufikisha katika tiba mujarabu ya matatizo yetu ya miaka nenda rudi, safari ambayo viongozi wengi waliikwepa na hawakutoa idhini ya kuanza kwake bali ni Rais Jakaya Kikwete ndiye aliamua kuthubutu kwa kuianzisha safari hiyo.

Licha ya miito mbalimbali kutoka kwa wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini ya kuwataka wasafiri hao (Ukawa) kukubali kukaa meza moja na mahasimu wao na pia kurejea bungeni kuendeleza majadiliano, wao hawajataka kusikia la mnadi sala wala la muadhini.

Nimeanza makala yangu kwa mfano wa Wapalestina ambao miaka nenda rudi wamekuwa ni watu wanaoishi katika wakati mgumu kuliko taifa lolote lile hapa duniani, watu wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wanaishi katika jela ya wazi, wameuawa na wanaendelea kuuawa kinyama na taifa la Israel linalotiwa jeuri na mataifa makubwa marafiki zake, hususan Marekani.

Hata hivyo, licha ya masaibu yote hayo ambayo yangewafanya wahamie tu msituni na kuendeleza mapigano, wameendelea kukaa meza moja na wavamizi wao katika kutafuta suluhu ya kudumu ya matatizo yao, ambayo muanzilishi wake anajulikana wazi, na ulimwengu mzima unajua hivyo.

Najiuliza hapa, kwa nini Ukawa, katika siku chache za kuelekea kwenye kuanza kwa ngwe ya pili ya Bunge maalumu wakagoma kukaa na wenzao kutafuta dawa ya tatizo?

Hii ni kwa sababu kumbukumbu zinaonesha waliitwa Mwenyekiti wa Bunge maalumu ili kukaa meza moja na kujadiliana katika mazingira ya amani na utulivu, lakini tofauti na wenzao wa Palestina ambao wanaendesha majadiliano katika hali ya vitisho na hofu kubwa hawa Ukawa walikataa.

Mwenyekiti wa Bunge maalumu la katiba, Samuel Sitta, amewataka mara kadhaa viongozi wa Ukawa wajitokeze wakae meza moja watafute mwafaka, lakini wapi, wamekataa kata kata. Hawakufika kabisa katika eneo la majadiliano, eti hawana imani naye. Haya masuala ya viongozi wetu wa upinzani kusema hawana imani na fulani hayajaanza leo wala jana.

Alipoteuliwa Jaji Joseph Warioba kuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya katiba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walipinga mjumbe wao Profesa Mwesige Baregu kuwemo katika tume hiyo wakisema hawakuwa na imani na Mwenyekiti wa Tume.

Leo hii wanampongeza Warioba na wanataka maamuzi yaliyoko kwenye rasimu yake yaheshimiwe, nini kimewabadilisha sasa na kuwa na imani na Warioba ambae walimuona kama ‘kibaraka’ wa CCM wakati ule na kusema kweli Warioba hajawahi kukana kuwa kada wa chama hicho?

Natumaini, kipindi kile kama wangeombwa kukutana na Mzee Warioba kabla ya kazi ya kukusanya maoni kuanza wangekataa pia wakidai hawana imani naye kama ilivyo sasa kwa Sitta. Wajiulize kama awali walionesha kutokuwa na imani na Jaji Warioba baadae wakaikubali kazi yake, kwa nini sasa wasimuamini kwanza Mzee Sitta ambaye hawajui ana nini ndani yake?

Hata waswahili wana usemi wao kwamba kataa neno, usikatae wito. Mimi ninaamini hapa Ukawa walikwenda upogo. Wangekuwa na hoja nzuri zaidi sasa kama wangelikubali wito ule wa Sitta ambaye inasemekana aliwahi pia kuwafuata Zanzibar walikokwenda baada ya kutoka bungeni lakini wakakataa kukutana naye.

Ukawa hawana budi kuchukua mfano wa viongozi wa Palestina, wa kutumia njia ya majadiliano pale wanapoombwa kufanya hivyo ili kutafuta suluhu katika kuwawezesha wananchi kupata katiba yao. Busara siku zote ni kukutana kwanza na hasimu wako mjadiliane na pale unapoona ndivyo sivyo, ndipo unakuja na hoja za kupinga na kukataa.

Kumkataa mchumba ambae hujamuona si jambo sawia hata kidogo, muone kwanza ndipo mengine yafuate. Leo hii sisi wananchi tukiwauliza Ukawa kwa nini mmekataa kuonana na Sitta, jibu litakuwa hatuna imani naye, kisa anatoka CCM ambacho wabunge wake ndio wengi bungeni lakini tukumbuke pia kwamba wakati anachaguliwa kuwa Mwenyekiti Ukawa walimbariki.

Ukawa kuendelea na kibwagizo cha ‘hatuna imani naye’ bado wanatuacha njia panda sisi wananchi wa kawaida ambao tuna kiu ya kuona tunapata katiba mpya itakayofufua matumaini mapya ya taifa letu.

Kama nilivyosema awali, kilichowatoa Ukawa bungeni ni zile shutuma za kuwa wenzao wa CCM waliacha kujadili rasimu na kuwajadili wao, shutuma za matusi, vitisho kebehi kwao na harufu ya udini kuanza kuingia ndani ya mchakato huo, hivyo wakaona wajiondoe.

Sawa hakuna mtu anayependa kuona mambo hayo yanaingia kwenye mchakato, ila njia ya majadiliano ndio ingekuwa sahihi hasa, kwani hapo ndipo wangekubaliana nini kifanywe wawapo ndani ya bunge hilo la katiba na hatua gani zichukuliwe pale mmoja anapoenda kinyume na makubaliano waliojiwekea, kutofanywa hivyo, natumai shutuma zao hazijapatiwa ufumbuzi.

Majadiliano ni njia ya kutafuta suluhu na kuwekeana masharti katika mambo muhimu na kwa yeyote atakayekiuka masharti hatua stahiki huchukuliwa na kulaumiwa.

Ninajua wameshaombwa sana, lakini nami niwaombe Ukawa wawe na uvumilivu wa kisiasa, uzalendo na kusikilizana, warejee bungeni kwani huko ndiko mahala sahihi pa kushindania kwa hoja.Kubaki mtaani na kuacha wachache wajadili rasimu, ni kutotutendea haki sisi wananchi ambao ndio wenye katiba, la sivyo wataubeba mzigo wa lawama.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji katika gazeti hili anayepatikana kupitia simu 0658010594

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Yusufu Ahmadi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi