loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukawa wasiharibu nia nzuri ya Rais Kikwete Katiba mpya

Wajumbe zaidi ya 600 wa Bunge hilo la kihistoria, wanakutana baada ya kuwa walishafanya hivyo katika awamu ya kwanza, iliyofanyika kwa siku 70, kuanzia Februari 11 mwaka huu.

Hata hivyo, lililazimika kusimama ili kupisha vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya vikao vya Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/15 ambalo kwa zaidi ya asilimia 60 wajumbe wake wanaingia katika Bunge la Katiba.

Lakini wakati umma wa Watanzania wakisubiri kwa hamu, kuona bunge hilo likiibuka na Rasimu iliyoboreshwa, ikiwa ni kuelekea katika kuifanya kuwa Katiba kamili, tayari baadhi ya wajumbe wa bunge hilo maalumu, wameonesha nia ya kutotaka kurudi bungeni kumalizia kazi iliyoko mbele yao.

Hawa ni wajumbe wanaotoka vyama vya siasa vya upinzani na wafuasi wao, ambao wamebatiza umoja kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Juzi, viongozi wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo, Freeman Mbowe wa Chadema, Ibrahim Lipumba wa CUF na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, walikutana na wanahabari na kutamka kwamba hawako tayari kurudi bungeni, huku wakisisitiza hata vikao vya maridhiano baina yao na CCM, vilivyokuwa vimelenga kuziba mpasuko uliokuwa umeibuka ndani ya bunge hilo, hawana mpango navyo.

Hakika, haya ni maamuzi magumu na yenye kuumiza wengi wenye kuitakia mema nchi hii, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kukukubali kwa nia njema hoja ya kuandika upya Katiba, licha ya kutokuwepo kwenye ilani wala vipaumbele vya CCM.

Na baada ya taratibu zote kufuatwa, ikiwa pamoja na kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais Kikwete akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.

Baadaye aliteua wajumbe 201 kuungana na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kuunda Bunge Maalumu la Katiba.

Kufikia hatua ya uteuzi, hakuna aliyelalamika, bali wajumbe walipongezana na kuhimizana kuunganisha nguvu katika kuisuka rasimu, itakayozaa Katiba bora kwa ustawi wa nchi na raia wake.

Tatizo likaanzia Dodoma katika mijadala mizito ndani ya Bunge, ambako baadhi ya wajumbe waliamini wanaonewa. Wakasusa na kususa kwao ndiko kiini cha vikao vya maridhiano, walivyotangaza kususia.

Tunajiuliza, kama tofauti hizi zinaweza kumalizwa kwa mazungumzo, iweje wajumbe hawa washikilie msimamo wa kutorejea bungeni, na wakati huohuo wakiapa kutorudi kwenye maridhiano?

Tulidhani, kama kweli kundi hili lilikuwa na dhamira ya dhati ya kupatikana kwa Katiba mpya, basi njia mwafaka ni kurudi kwenye uwanja wa majadiliano na watoe hoja na hatimaye mwenye hoja yenye mashiko atashinda.

Na pia wakumbuke kuwa pamoja na kuombwa kurejea bungeni na watu wa makundi mbalimbali ya kisiasa na kidini, rasimu watakayoipitisha haitakuwa mwisho wa taratibu za kupatikana kwa Katiba, bali wananchi ndio watakaokuwa na maamuzi ya mwisho.

Kwa mantiki hiyo, tusiishie kuburuzana, bali busara zitumike kurekebishe yale yanayoonekana kuwa na dosari, kabla ya kufikia uamuzi wa kurudisha rasimu kwa wananchi.

Hicho ndicho wanachokitaka Watanzania, badala ya kushuhudia wajumbe wa Bunge hilo, wakitunishiana misuli, ilhali fedha nyingi za walipa kodi zikiteketea, bila ya dalili ya mwelekeo mzuri wa Katiba mpya.

Ifike mahali wanasiasa wawe na ukomavu wa kisiasa na wenye kuweka mbele maslahi ya Taifa na sio maslahi binafsi. Kama ukweli ndio huu, tunashauri wote wanaofikiria kususia vikao vya Bunge la Katiba, waachane na mawazo hayo.

Badala yake, warejee bungeni kwenye majadiliano, watoe hoja zao nzito wakiwa humo na hatimaye watuletee Watanzania rasimu bora, itakayoamuliwa na wananchi.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi