loader
Dstv Habarileo  Mobile
Uke wenza chanzo cha kusambaratika kwa ndoa Zanzibar

Uke wenza chanzo cha kusambaratika kwa ndoa Zanzibar

Hata hivyo, ruhusa hiyo ya wanaume imegeuka kuwa shubiri kwa wanawake ambao kwa kawaida hakuna anayefurahia kuona kwamba mumewe anaongeza mke wa pili. Tafsiri ya uke wenza ni mume kuoa zaidi ya wake wawili ambapo wanawake hao wanalazimika kuishi pamoja kwa kupata huduma zote kutoka kwa mume mmoja.

Historia katika vitabu mbali mbali vitakatifu inaonesha kwamba Nabii Ibrahim hakusalimika na mikasa ya wanawake na uke wenza ambapo mke wake wa kwanza Bibi Sara ndiye aliyemshawishi kuoa mke wa pili kwa ajili ya uwezekano wa kupata mtoto baada ya wao wawili kuishi muda mrefu bila ya mafanikio.

Hata hivyo Bibi Sara wakati akiwa katika uke wenza huo na bibi Hajra, alipambana na vituko vingi ambapo wivu ni moja ya matatizo makubwa katika uke wenza kwa wanawake wawili. Kwa nini wanawake wengi wa Kiislamu wanachukizwa na tabia ya kuishi uke wenza ambao ndio chanzo cha kuyumba kwa ndoa na baadaye kuvunjika huku watoto wakikosa matunzo ya baba na mama na wengine kuingia katika ajira ngumu za watoto?

Rabia Abdalla Zahoro ambaye amepewa talaka na mumewe aliyeishi naye kwa zaidi ya miaka 15 na kubahatika kupata watoto 6 alisema mwanamume anapooa mke wa pili ambaye anakuwa mpya wanakuwa na dharau kwa mke wa kwanza ambaye anaonekana kama aliyechakaa.

Alijitolea mfano, akisema mumewe aliamua kwenda kuoa mke wa pili baada ya yeye kuwa na watoto wengi huku mumewe akidai kwamba hapati muda wa kustarehe au utulivu wa hali ya juu kutokana na kelele za watoto.

“Unajua wanaume ni watu wa ajabu sana ukiwa hujapata mtoto ni sababu kubwa ya kupewa talaka, lakini wakati mwingine wanaamua kuoa mke wa pili kwa sababu tu mke wa kwanza amekuwa na ulezi wa watoto wengi na yeye hudai kukosa muda wa kufanya starehe au utulivu katika nyumba,” alisema.

Lakini alisema wanawake wengi hawapendi uke wenza kwa sababu wanaogopa ushirikina, ambao unatokana na ushindani wa mapenzi kwa wanawake wawili au watatu hadi wanne waliopo katika ndoa moja. Kauli hiyo iliungwa mkono na Zuwena Kona mkazi wa kijiji cha Nungwi ambaye alidai kwamba ndoa yake ilivunjika mara alipoingia katika uke wenza, ambapo alipambana na vitimbi vya ushirikina.

“Sisi wanawake wengine tunaposikia mume wako kaoa mke wa pili basi tupo tayari kudai talaka kwa sababu uke wenza hutawaliwa na uswahili wa ushirikina wa ushindani wa mapenzi,” alisema. Karani wa Makahama ya Kadhi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Asma Fransic alisema kesi nyingi zinazofikishwa katika mahakama hiyo ni wanawake kudai talaka kutokana na wanaume kuongeza mke wa pili na matokeo yake kuanza kutelekezwa.

Asma alisema katika mwaka 2012 zaidi ya ndoa 10 zilisambaratika kwa talaka kufuatia wanawake kulalamika kuingia katika ukewenza ambapo malalamiko ya matunzo na kutelekezwa yaliibuka. “Ndoa nyingi zinavunjika kutokana na malalamiko ya wanawake kuishi katika ukewenza huku wakikosa huduma muhimu za matunzo na watoto kutelekezwa,” alisema.

Alisema mapema mwaka 2012 wanaume 5 walipigwa faini na Mahakama ya kadhi na kutakiwa kuwasilisha fedha za matunzo kwa watoto wao baada ya kutengana. Mhadhiri mwandamizi wa Chuo kikuu cha taifa Zanzibar (SUZA), Dk Issa Haji Ziddy alisema wanaume wengi wanaamua kuongeza wake bila ya kuzingatia masharti yaliyowekwa katika Quran ambapo unatakiwa kuzingatia suala zima la matunzo kwa mwanamke na watoto.

Alisema wanaume wanaamua kuoa wake zaidi ya watatu lakini hawazingatii masuala ya uwezo katika kuwahudumia wanawake na watoto. “Wanawake wengi wanachukia uke wenza kwa sababu wanaume wanapoamua kuongeza wake hawazingatii masharti ikiwemo uwezo wa kuwahudumia wake na watoto,” alisema.

Dk Ziddy alisema upo umuhimu wa kuwepo kwa mkataba wa ndoa ambao utaweka masharti kwa wanandoa ikiwemo suala la kutunza watoto pamoja na mgawanyo wa mali ili kuepuka wanawake kutelekezwa wakati wanaume wanapoamuwa kuongeza mke.

“Zipo nchi za kiarabu tayari wanao utaratibu wa mkataba wa ndoa ambao unaweka masharti ya ndoa mwanamme kabla ya kuoa mke wa pili kwanza anatakiwa kwenda mahakama ya kadhi ambapo ataulizwa anaongeza mke wa pili kwa sababu gani na vipi atamtunza mke wa kwanza pamoja na watoto,” alisema Ziddy.

Ofisa mwandamizi wa taasisi ya Save Children Fund Zanzibar, Mubaraka Maaman alisema kusambaratika kwa ndoa ndiyo chanzo kikubwa kwa watoto kuingia katika ajira ngumu na kuacha shule.

Maaman alisema utafiti uliofanywa na Shirika la Save Children Fund umebaini kwamba zaidi ya watoto 20,000 Unguja na Pemba wamejiingiza katika ajira ngumu ya watoto ambayo chanzo chake ikiwemo kusambaratika kwa ndoa na wanaume kutelekeza wake zao.

Alisema migogoro ya ndoa kwa wanaume kuacha wake zao ndiyo chanzo cha kusambaratika kwa ndoa na watoto kujiingiza katika ajira mbaya ya watoto ambayo hatimaye watoto kuacha shule. “Ajira mbaya za watoto chanzo chake kikubwa ni kusambaratika kwa ndoa kwa wanaume kutelekeza watoto zao na kukosa haki za msingi ikiwemo elimu,” alisema.

Kadhi mstaafu wa wilaya ya mjini Mwanakwerekwe Ali Suleiman alikiri kuwepo kwa tatizo la wanaume kuamua kuongeza mke wa pili au watatu bila ya kutekeleza masharti ya ndoa ikiwemo matunzo kwa mke na watoto. Alisema hiyo ndiyo moja ya sababu kubwa kwa wanawake kuamua kudai talaka kwa sababu kwa wanaume wengi wanaamua kuongeza mke wa pili baada ya kuanza kumchoka mke wa kwanza kwa sababu mbali mbali.

“Sheria ya ndoa ipo wazi sana mwanaume anapoongeza mke wa pili, kwanza anatakiwa kutoa kutoka nyumba zawadi ya aina yoyote ile lakini pia anatakiwa kutoa taarifa kabla kwa mke wa kwanza kuhusu mipango yake ya kuoa mke mwingine,” alisema. Lakini alisisitiza na kusema suala la uwezo ni muhimu sana ambapo linakuja moja kwa moja katika matunzo ya mke na watoto ili kuepuka utekelezaji wa familia.

Kadhi wa wilaya ya Kaskazini Unguja ambaye hufanya kazi zake katika Mahakama ya Mfenesini, Khamis Kassim Haji, alisema katika kipindi cha miezi saba jumla ya talaka 26 zimetolewa ambazo zimedaiwa na wanawake kwa sababu ya kukataa kuishi katika mazingira ya uke wenza.

“Ni kweli wanawake wengi hawapendi kuishi katika mazingira ya ukewenza kwa sababu mbalimbali, lakini moja kubwa wanaume wanaamua kuongeza mke wa pili kwa ajili ya kumkomoa mke wa kwanza tu,” alisema. Baadhi ya wanaume wanadai kwamba wanalazimika kuongeza mke wa pili au wa tatu kutokana na visa vya wanawake ikiwemo wivu wa kupindukia pamoja na kushindwa kutekeleza huduma za ndani ya ndoa.

Utafiti mdogo wa kihabari uliofanywa na TAMWA kutembelea Mkoa wa Kaskazini Unguja huko Nungwi, wanaume wanadai kwamba wanakosa huduma za mapenzi ambapo wanalazimika kuoa wake wengine zaidi. Ali Juma mkazi wa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja alisema wanaume wengi wa kijiji hicho wamelazimika kuoa wake kutoka mkoa jirani wa Tanzania Bara huko Tanga kwa ajili ya kupata utulivu wa mapenzi.

“Unajua sisi wake zetu wa hapa kijijini hawatupi mapenzi na utulivu na ndiyo maana tunalazimika kwenda Tanga kuoa wake wa huko ambao ni mafundi katika mapenzi ya ndani,” alisema. Kombo Faki mkazi wa Potoa alisema wanaume wanaoa wake zaidi ya wawili au watatu kwa ajili ya kupunguza jeuri au kiburi cha mwanamke kinachotokana na wakati mwingine dharau ambayo inatokana baada ya kuishi kwa muda mrefu na kuzoeana.

“Ni kweli ukitaka kupunguza jeuri ya mwanamke basi muolee mke wa pili ataacha mara moja kiburi chake na kuanza kurudisha mapenzi ya mumewe,” alisema Kombo. Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Hassan Othman Ngwali alithibitisha kuwepo kwa tatizo la uke wenza na kuwepo chanzo cha talaka pamoja na wanawake kutelekezwa na watoto.

Alisema sheria ya kadhi ipo wazi ambapo mwanamume anatakiwa kulinda matunzo ya watoto na kudhibiti tatizo la utelekezaji wakati anapooa mke mwingine au uke wenza. “Uke wenza kwa kawaida hauna matatizo isipokuwa wanaume ndio wenye matatizo ambao wanashindwa kutekeleza masharti ya ndoa, matokeo yake wanawake wanaogopa au wengine hudai talaka mara tu wanaposikia au kupewa taarifa ya uke wenza,” alisema.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi