loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukishukuru kwa kidogo, utabarikiwa kwa makubwa

Kwa kuwa safu yangu hii mara nyingi nazungumzia masuala mbalimbali yaliyopo katika jamii yetu, nimeguswa leo kuzungumzia watu wenye tabia hizi mbili ili kama uko katika kundi la watu wasiokuwa na shukrani, basi ubadilike na wale walioko katika kundi la kushukuru waendelee hivyo na ikibidi waongeze.

Tukianza na watu wenye kundi lisilokuwa na shukrani, watu wa namna hii mara nyingi hawana furaha, ni watu wenye uchungu na mawazo hasi kila wakati, kwao wao kila kitu hakifai. Mara nyingine hupenda kuangalia ambayo hayako sawa katika maisha yao na kutwa kulalamika kuhusu mapungufu yao hayo.

Kama ni mtu wa kufanya kazi basi atalalamikia kazi yake, au atalalamikia mahali anapoishi kuwa hapafai au kukosoa lolote tu ili mradi aridhike, kama hiyo haitoshi huwa ni mtu wa kulalamikia watu wanaomzunguka na hulalamikia kila kitu kilicho karibu naye kwa ujumla ni mlalamishi tu.

Kutokuwa na tabia ya shukrani husababisha mhusika kufukuza marafiki au kukimbiwa na marafiki, kwa sababu haridhiki, hana jema, yeye siku zote kujiona mnyonge na kulalamika tu, kama hufahamu hali hii hukera wale wanaokuzunguka.

Sio hivyo tu, mtu asiyekuwa na shukrani hujiwazia vibaya kuwa hawezi kufanya lolote jema, kimsingi hajiamini na mara nyingine hulaumu watu wengine kutokana na kukosa kwake mwenyewe furaha. Anajaribu kubebesha lawama wengine wakati ni tabia yake mwenyewe ndio inamsababishia hayo.

Huwaza kuwa hawezi kufanya kitu chema hivyo hajiamini. Hata mambo yake yakienda ndivyo sivyo katika maisha yake huona kama kaonewa, badala ya kuangalia wapi amekosea arekebishe, yeye ni kulalama tu.

Lazima ujiwazie mawazo chanya sio kujilaumu tu bila sababu za msingi. Kibaya zaidi hataki kuambiwa ukweli na matokeo yake hujaribu kuwashawishi watu kuwa yeye yupo sawa ila waliomzunguka ndio wabaya, ndio maana kwa tabia hii marafiki au watu walioko karibu naye huamua kujiweka mbali.

Kwa kweli usipokuwa na shukrani, huwezi kuona jambo lolote zuri kwako kwa sababu wakati wote unaangalia upande mbaya wa kila kitu au jambo unalolifanya.

Kama utakuwa na tabia hii kamwe huwezi kufanikiwa kwa sababu unakosa uvumilivu. Kama huna tabia ya kushukuru kwa kila jambo, anza kujitazama na ikiwezekana badilisha mtazamo wako. Jijengee tabia ya kushukuru kwa kila jambo ili hata panapotokea mapungufu uweze kujirekebisha na kuchukua hatua sio kulaumu watu.

Wale wenye tabia ya shukrani, mara nyingi wakati wote huwa watu wenye furaha, hata kama atakuwa na tatizo au anapitia changamoto atashukuru na kufurahia hali hiyo bila hata jirani yake kufahamu jambo linaloendelea katika maisha yake.

Watu wenye tabia ya kushukuru hupenda kusema asante hata kwa mambo madogo na ndio maana utakuta wanabarikiwa zaidi na zaidi. Hata kile ambacho kwako unakiona hakifai kusema asante, yeye atashukuru tu.

Kwa sababu ni mtu wa shukrani, basi huangalia alivyo navyo na kuvithamini, huwezi kumkuta akilalamika kwa kukosa asivyonavyo, anatambua kuwa maisha yake hayahitajiki kuwa sawa asilimia 100 ili yeye awe mwenye furaha.

Mtu wa namna hii huwa na marafiki wengi sio kama mtu asiyekuwa na shukrani, kwa sababu anajitambua na anajikubali, na kushukuru kwa hali alionayo kwa wakati huo.

Ni rahisi kwa mtu wa aina hii kufanikiwa kwa sababu ni mvumilivu na hata akipitia magumu anashukuru, akiwa na imani iko siku atabarikiwa au kupata vile asivyo navyo. Basi siku ya leo jipime ujione uko katika kundi gani ili uweze kubadilika na utakuwa na maisha yenye furaha.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi