loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Ukosefu wa maji ‘waiangamiza’ Mwanga

Vijiji vya Ngulu na Mgagao vilivyo katika kata za Kwakoa na Mgagao wilayani humo navyo vinakabiliwa na uhaba wa maji ambao umesababisha shughuli za uzalishaji kukwama.

Uhaba huo unatokana na miundombinu ya maji iliyokuwepo awali kuanzia miaka ya 70, kushindwa kuhimili mahitaji ya sasa kutokana na ongezeko la watu linalohitaji maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kulisha mifugo na kutumiwa katika kilimo.

Vijiji vyote viwili, vyenye wakazi zaidi ya 3,000 kwa sasa vinapata maji kwa ajili ya matumizi yao kutoka kichoteo cha Mabweveke ambayo huingia hapo kwa njia ya mfereji mdogo uliotengenezwa kwa njia ya kienyeji kutoka katika makorongo ya Ngongo na Kisingari yaliyo katika eneo la Mabweveke katikati ya kijiji na kata ya Kilomeni.

Mfereji huo unaoingiza maji katika kichoteo hicho, umepungua kasi yake ya kutiririsha maji na hivyo kusababisha maji kupungua na kutowafikia watumiaji kwa wakati muafaka. Mwenyekiti wa kijiji cha Ngulu, Hashimu Waziri na Mwenyekiti wa kijiji cha Mgagao, Longovilo Avakwa kwa pamoja wanasema kuwa hali hiyo imewafanya waingie katika migogoro ya wao kwa wao kutokana na uhaba wa maji.

Waziri anaongeza kuwa, hivi sasa kutokana na uhaba wa maji, wanavijiji wameingia kwenye migogoro ya matumizi ya ardhi, ambapo wananchi wa vijiji vya Mgagao huvamia vyanzo vya maji vya kijiji cha Ngulu, ambavyo ni vichache kwa ajili ya kunywesha mifugo. “Hali hii imesababisha uzalishaji wetu katika kilimo kushuka, kwa sasa ekari moja inazalisha magunia 5-6, tofauti na awali ambapo tulikuwa tunapata magunia 10-12,” anasema.

Anasema kuna baadhi ya vyanzo maji vilivyowekwa kijijini kwake navyo havifanyi kazi kwa sasa, hali inayowafanya wakazi wake kutafuta maji usiku na mchana. “Sisi ni wakulima, tunahitaji maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kuondoa umaskini kupitia kilimo, lakini hakuna mipango kutoka serikalini ya kukabiliana na tatizo hili la vyanzo vya maji ili tupate maji ya uhakika kwa ajili ya matumizi yetu”, anafafanua.

Anasema kwa hivi sasa vijiji vya Ngulu na Mgagao, vinatumia laini moja tu ya maji ya Mwabashula, ambayo haitoshelezi kwa vijiji vyote viwili. Anasema maji katika vijiji hivyo ni kama dhahabu iliyopotea kutokana na umuhimu wake kwa matumizi ya wakulima na wafugaji.

“Maji hapa, tunayatafuta kama dhahabu, kwa ajili ya kunywa, kuoga, kunywesha mifugo na matumizi ya kibiashara, lakini hatuyaoni, maji, maji, tunahitaji maji, serikali mtusaidie maji,” analalamika Waziri. Mwandishi wa makala haya aliwashuhudia baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ngulu, wakiwemo wanafunzi wakihangaika kutafuta maji, huku baadhi yao wakimuonesha baadhi ya vyanzo vya maji ambavyo havitumiki kwa sasa, wanaomba serikali imalize tatizo la maji.

Daniel Mndeme na Doricah Mwigamba waliokutwa wakitafuta maji, wanasema hawana uhakika wa kupata maji baada ya vyanzo muhimu kuharibiwa na wafugaji. Wanahitaji waimarishiwe miradi ya maji ikiwemo serikali kukinga makorongo ya muhimu yaliyopo yanayotiririsha maji.

Kwa upande wao, Binti John, Anna Ephraimu na Bi Hadija Juma (70), waliokutwa wanatafuta maji, wanasema wana muda wa miaka kumi hawapati maji ya uhakika, kiasi cha kuichukia serikali yao. John anasema maisha yake ya kila siku imekuwa ni kutafuta maji, hajishughulishi na shughuli nyingine tofauti na maji.

“Kuna wakati najiuliza maswali mengi, jinsi ambavyo serikali inavyohudumia watu wake, ni huduma gani hiyo inayotoa, endapo suala la maji ambayo ndiyo uhai imeshindwa kufanya hivyo,” anahoji John. Hadija anasema maji ni changamoto kubwa kijijini kwake, hali inayomfanya kuhisi kuwa hakuna uongozi wa serikali, anakumbuka enzi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere jinsi alivyokuwa akishughulikia matatizo ya maji.

“Wakati wa Nyerere, tulikuwa na miradi ya maji hapa, lakini imeharibika hakuna anayetutengenezea, viongozi wa sasa wanatanguliza siasa mbele, wanaonekana wakati wa kuomba kura tu,” anasema. “Korongo la mto Mkundanyi ambayo hutiririsha maji, inafaa maji yale yakingwe, ili yatusaidie katika matumizi ya kilimo na nyumbani, inafaa izuiwe ili maji ya mvua yavunwe na tuweze kuyatumia, ambayo yatatuondolea tatizo la uhaba wa maji,” anaeleza Mwigamba.

Kwa mujibu wa Mwigamba, wanahitaji kilimo cha umwagiliaji kitachowawezesha kuwa na uhakika wa kupata chakula cha kutosha badala ya kutegemea mvua ambazo hazitabiriki kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. “Miezi kumi sasa hatujapata mvua, tunaomba serikali itusaidie tupate maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, tutapata chakula cha kutosha na kuondoa umasikini na kupata maisha bora,” anasema.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mgagao, Abnaimu Mvungi, Maningo Mbaga, Shabani Ngalevo na Asha Laizer wanasema maji ndio kichocheo kikubwa cha uchumi wao. Maji yamesababisha kuingia katika mgogoro na kijiji cha Ngulu, ili hali wao ni ndugu. Wanasema hali hiyo imechangiwa kutokana na maji kutumiwa na wakulima na wafugaji kutoka vijiji vyote viwili.

“Hivyo utaona maji kwetu ni bora kuliko vitu vingine na ndiyo hutusababishia kutoelewana miongoni mwetu, maana kila mmoja wetu anahitaji maji,“ anaeleza Mvungi. Wanasema serikali ifanye yote, lakini kilicho muhimu kwao ni kupatiwa maji safi na salama ya kunywa kwa ajili ya makuzi na lishe bora kwa familia zao.

Tatizo la maji kutatuliwa sasa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe ambaye pia ni mbunge wa Mwanga, anasema kuwa serikali inafanya juhudi kubwa ya kuwapatia maji safi na kunywa wananchi wa vijiji vya Ngulu, Kwakoa na Mgagao ambako kwa sasa vinapata maji kupitia visima zaidi ya sita vilivyochimbwa kwa ajili ya kutoa huduma ya maji.

Anasema kuwa visima hivyo vilivyochimbwa, visima viwili viliweza kupata maji, ambapo kisima kimoja kina uwezo wa kutoa maji mita za ujazo mbili kwa saa ambacho kwa sasa kisima hicho kilicho katika kijiji cha Mgagao.

“Awali kijiji cha Ngulu kilikuwa kinapata maji kwa kutumia chanzo cha Mabashula, lakini kumekuwepo na matatizo ya uchakavu wa miundombinu ya maji ambayo ni ya siku nyingi, lakini watu wengine wamekuwa wakiharibu miundombinu ya maji na hivyo kusababisha watu wengine kukosa maji, lakini tutawachukulia hatua stahiki,” anasema.

Profesa Maghembe ambaye anasema kuwa hali hiyo inatokana na wananchi hao kutegemea maji ya mvua za vuli kwa asilimia 85 na kwamba baadhi ya visima vyenye uwezo mdogo wa kutoa maji vimefungiwa sola ili viweze kutoa maji ya uhakika kwa muda wote.

“Visima vyenye uwezo mdogo tumevifungia sola ili viweze kutoa maji ya uhakika na kuongeza kuwa malambo ya Doya na Kauzeni ambayo yalikuwa yamejaa mchanga na lile la Nadung’oro upande wa Pangaro yamekarabatiwa na yanatoa maji kwa wananchi,” anasema na kuongeza kuwa upo utaratibu wa kuanza kuyatawanya maji tuliyo nayo kwenye vitongoji vyote ili wananchi waweze kupata maji ya uhakika,” anasema.

Amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuwa na subira wakati serikali kupitia Wizara ya Maji na halmashauri ya wilaya ya Mwanga ikichukua hatua zaidi za kushughulikia tatizo hilo la upungufu wa maji kwa maeneo hayo. Vijiji vingine ndani ya wilaya ya Mwanga ambavyo vimeathiriwa na uhaba mkubwa wa maji ni Kisangiro, Mandaka, Kiruru, Ibwe Ijewa na Lwami.

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi