loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Ukosefu wa vifaa warudisha nyuma mradi wa bwawa Ishololo

Fedha hizo ni katika kuendesha miradi hiyo hususani mabwawa, kununua mabanio ya maji, ambapo vyanzo vya maji kutoka kwenye mito na mabwawa hutegemea msimu wa mvua na mara nyingi hukauka mapema kwa ukame hivyo kutoleta manufaa kwa wakulima.

Licha ya kukauka mapema kumekuwepo na ubabaishaji hata katika ujenzi wa miradi hiyo kwa makampuni yanayochukua zabuni za kuendesha miradi hiyo, huku baadhi yake ikijengwa chini ya kiwango na kuichelewesha kwa kuiwekea hasara halmashauri na wakulima wa eneo husika.

Asilimia 89 ya wakazi wa Halmashauri ya Shinyanga hujishughulisha na kilimo. Na kwamba eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 15,960 lakini zinazotumika ni hekta 2,150 sawa na asilimia 13.5 huku mvua kwa mwaka ikiwa ni milimita 450 hadi 900. Mradi mmojawapo ambao unasuasua ni ule wa ujenzi wa bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa wakulima wa Kijiji cha Ishololo Kata ya Usule katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Kusuasua huko kunatokana na kutokamilika kwake, hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wakulima kuvurugiwa mashamba yao yaliyochukuliwa kwa ajili ya kutengwa kwa mradi huo wa ujenzi wa bwawa. Mradi huo umeonekana kuwa katika mazungumzo na viongozi wa mkoa na halmashauri kwa kuweka wasiwasi huenda usikamilike kwa wakati huku ukitumia fedha nyingi zilizotolewa katika pande mbili za ufadhili.

Diwani wa kata hiyo Amina Bundala akizungumzia mradi huo anasema kampuni iliyopewa zabuni hiyo, wasimamizi wake walifika eneo la mradi na kuanza kazi, ila utekelezaji wake unasuasua.

“Wakati mwingine wiki mzima hakuna kinachofanyika, na hawatoi sababu”, anasema Bundala. Anasema tatizo lililopo ni kwamba mashamba ya wakulima yamevurugwa kwa kuweka mradi wa bwawa hilo, ambalo awali wakulima hao walikubali mradi huo lakini kadri siku zinavyosonga hakuna kinachoeleweka, na badala yake wanapata hasara kwani msimu wa kilimo umeanza na mashamba yao hawajui hatma yake.

Wakulima waliovurugiwa mashamba yao watalazimika kulipwa fidia au kuwanyang’anya wanaomiliki maeneo makubwa na kuwapatia ili kuepusha mgogoro ambapo hakuna manufaa yoyote watakayoyapata labda mradi huo ukamilike kwani imani ipo ya uwepo wa maji kwa muda mrefu bila kukauka kwenye eneo lililoweka mradi wa bwawa.

Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Ishololo, Joseph Mmoja na Kulwa Kija wanazungumzia mradi huo na kusema eneo hilo lilikuwa na bonde dogo lililokuwa likitumia maji kwa muda mrefu hata kufanya vijiji zaidi ya vitano kutumia maji hayo kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kunywesha mifugo.

Wanasema mradi huo ukikamilika kama ilivyokusudiwa wakulima wanaweza kupata manufaa zaidi katika kilimo cha umwagiliaji hasa katika zao la mpunga linalozalishwa kwa wingi ndani ya vijiji hivyo. Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo, Edward Maduhu malengo ya kilimo cha mpunga kwa mwaka wa 2013/14 ni hekta 26,570 na matarajio ya mavuno ni tani 53,140 huenda zisifikiwe au kukaribia kutokana na hali ya mvua kuwa haba.

Pia kutofikia malengo hayo kunasababishwa na kutokamilika kwa miradi iliyokusudiwa kwa wakati kama hiyo ya ujenzi wa bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Mwenyekiti wa kijiji cha Tindeng’hulu, Joachiam Manoni akizungumzia mradi huo anasema watendaji wa zabuni hiyo ni wazembe kwani wamekuwa wakiwashuhudia kutokufanya kazi kwa muda mrefu huku wakitoa visingizio kama vile kudai kijiji cha Ishololo kuna fisi hivyo hawawezi kufanya kazi usiku.

Msimamizi wa kampuni inayolalamikiwa ya Syscon Builders, Nicodems Malunde anasema ni kweli walianza kwa kuchelewa sababu ya kuwepo kwa maji eneo hilo, hivyo kusubiri yakauke na pia uhaba wa maji ya kufanyia kazi. Pia wamekiri kuwepo na uhaba wa vifaa vya kutendea kazi ikiwa wanaeleza kuwa pampu na rola kwenye magari hayo ni mbovu hivyo iliwalazimu kuyakarabati kwa muda mrefu huku wakieleza kuwa kwa muda uliobaki wana uwezo wa kumaliza.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga alisikitishwa na hali aliyoiona mara baada ya kufanya ziara katika eneo hilo huku akiwahoji kuwa wakati wanaomba mradi hawakutembelea eneo husika? Au tatizo la uhaba wa maji ndio wameligundua ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi hata vilivyopo ni chakavu.

Rufunga alieleza kuwa shughuli haiwezi kukamilika kwa ufanyaji kazi wa vifaa kuwa vibovu na kumueleza mkurugenzi watahakikisha mazungumzo yanafanyika na wizara inayoshughulika na TAMISEMI kwa kuomba fedha zirudi za halmashauri.

Pia alitoa agizo kwa kufika Desemba 16, mwaka huu atahakikisha anautembelea mradi huo ili kuona kama umekamilika ikiwa mtu anahitaji kazi ya kuendesha mradi lazima ukamilishe kwa kuwa na vifaa vilivyo na ubora,vibarua jenireta la kufanya kazi usiku ili ikamilike kwa wakati ndio utaratibu.

Mhandisi wa skimu ya umwagiliaji, Gofrey Mbwambo anasema kuwa mradi huo ulilenga kuwanufaisha wakulima na wafugaji kutoka vijiji viwili vya Ishololo na Tindeng’hulu ambao ungeweza kunufaisha wakulima zaidi ya 1,700 na kiasi cha hekta zipatazo 500 zingeweza kumwagiliwa na maji kutoka katika bwawa hilo.

Mradi huo ambao unafadhiliwa na mradi wa uwekezaji katika sekta ya kilimo wilaya (DASIP) imechangia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 740 na mfuko wa umwagiliaji (DIDF) kwenye mradi huo imechangia kiasi cha shilingi milioni 200 na kufanya jumla ya gharama ya mradi kuwa zaidi ya shilingi milioni 940.

Mbwambo anasema kuwa kiasi cha shilingi milioni 200 awali zililetwa kwenye halmashauri kwa ajili ya kutekelezaji mradi huo lakini wizara ya TAMISEMI ilielekeza fedha hii ihamishwe katika ofisi ya mradi DASIP Mwanza ili kuunganishwa na fedha za DASIP zilizotolewa kwa utekelezaji wa mradi huo.

Hali ya utekelezaji mpaka sasa kazi imefikia hatua ya msingi wa bwawa ambayo sawa na asilimia 20 ya kazi kwani ameshafanya kazi ya mita za ujazo 7,200 bado mita za ujazo 30,956 za tuta la bwawa anasema Mbwambo.

Kwa hali inavyoonesha mkandarasi hana uwezo wa kumaliza kazi kwa muda uliopangwa kutokana kuwa na vifaa vichache na uchakavu pia mradi huu hautatekelezeka mkandarasi anamaliza mkataba tarehe 15/12/13 na muda wa mradi wa DASIP unafungwa tarehe 31/12/2013 ikiwemo kufungwa pia kwa akaunti hiyo.

Pia ulipwaji wa awali mkandarasi huyo amekwisha pewa fedha hizo kilichobaki hata asipokimalizia halmashauri tayari itakuwa imepata hasara ya fedha hizo huku wakulima wa mashamba yaliyovurugwa kwa lengo la kuwekwa mradi huo kupata hasara.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mohamed Kiyungi anasema kuwa kwa ushauri kiasi cha shilingi millioni 200 zilizotoka DIDF na kuhamishiwa akaunti ya mradi wa DASIP Mwanza wao kama halmashauri walikuwa wanaomba fedha hizo zirudishwe kwenye akaunti ya halmashauri ili ziweze kuendeleza shughuli za miradi ya umwagiliaji.

Anasema kushindwa kufanya hivyo fedha hiyo itarudi Benki ya Afrika (AFDB) kwa kuwa mradi wa DASIP unaisha muda wake 31/12/2013 ikumbukwe fedha Sh milioni 200 kutoka DIDF haikulenga kuungana na DASIP bali ingelipwa na halmashauri ya wilaya kwenye mradi huo.

Hata hivyo malalamiko yanayoendelea kwa viongozi wa halmashauri hiyo na mkoa kutoshirikishwa kwa namna yoyote katika mkataba wa uendeshaji wa mradi huo.

Ikiwa mkataba wa mradi huu ulifungwa tarehe 15/02/2013 kati ya katibu mkuu na wizara ya kilimo chakula na ushirika na mkandarasi aitwaye SYSCON BUILDERS wa jijini Dar es Salaam chini ya mhandisi mshauri CODA AND PARTNERS ya Kenya baada ya kufunga mkataba mkandarasi alitakiwa kuanza kazi mwezi mmoja baada ya kufunga mkataba huo.

Pia mkandarasi alitakiwa kuanza kazi tarehe 15/03/2013 na kazi hii ilitakiwa ifanyike ndani ya siku 240 sawa na miezi minane, hata hivyo kazi ilianza mwezi Juni kwa kuchelewa miezi mitano.

Mradi huo umekuwa ukionesha wasiwasi wa kutokamilika huku halmashauri ikionesha kupata hasara ya Sh milioni 200 wakulima waliovurugiwa mashamba yao kuweka mradi huo wataingia hasara ambapo wizara inaombwa kuingilia kati suala hili ili kuweza kuwanusuru wakulima wa eneo hilo kutopoteza haki yao.

Mradi huo unaelezewa uliibuliwa na wananchi wenyewe katika bajeti ya kijiji ya mwaka 2011/12 kwa kutaka bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga ikiwa walikuwa wakikosa maji ya kutosha kwa kuliendeleza zao hilo na kupata mavuno ya kutosha huku halmashauri ikipata pato la ndani zaidi kupitia ushuru za zao la mpunga.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi