loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ulevi chanzo cha watoto wa mitaani

Ulevi chanzo cha watoto wa mitaani

Kwa kiasi kikubwa, katika familia nyingi nchini ulevi huo unafanywa na wanaume. “Wanaume wengi wako radhi kuwatelekeza na kuwaacha bila mahitaji wanawake na watoto nyumbani ili wakatumie pesa walizo nazo kwa anasa mbalimbali na inapobidi wanauza mali za nyumbani ili wakastarehe,” anasema Libenti Lukaya, mkazi wa Temeke.

Ndoa nyingi huathirika kutokana na tabia chafu ya ulevi iliyopo miongoni mwa wanafamilia hasa wanaume, kiasi kwamba ulevi huo huchangia wanaume kusambaza virusi vya Ukimwi kwa wake zao.

Mmoja wa wahadhiri katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliyopo Dar es Salaam, Deodat Babili aliwahi kusema, “Jitu linakunywa na kulewa ovyo ovyo linafanya ufuska, kisha linakwenda kuangamiza familia nyumbani…” Watoto wengi katika familia wanakosa malezi bora na huduma muhimu, kutokana na madhara ya pombe kwa wazazi na hasa, wanaume.

Hali hiyo ndiyo iliyosababisha hata Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kuanzisha Kituo cha Usuluhishi (CRC) kinacholenga kusuluhisha migogoro ya kifamilia na hasa kuwasaidia waathirika wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Kazi hiyo inafanywa pia na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kupitia mpango wa kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini, ujulikanao kama GEWE II .

Kwa mujibu wa uchunguzi wa mwandishi, kwa wastani kituo hicho hupokea takribani mashauri 35, ambapo waathirika wanaojitokeza kuomba msaada wa kisheria, huutaja ulevi wa pombe wa kupindukia, kama kichocheo na chanzo kikuu cha vitendo vya ukatili, wanaofanyiwa baada ya wanaume kushindwa kutimiza wajibu wao.

Kwa kushirikiana na mashirika mengine, yakiwamo ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na TAMWA yenyewe, taarifa kutoka TAMWA zinasema zaidi ya asilimia 70 ya wahitaji wa huduma hizo wanaofika vituoni hapo, hunufaika kwa msaada na ushauri na kumaliza matatizo.

Katika moja ya mazungumzo na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka anasema ulevi wa kupindukia ni moja ya vyanzo vya ongezeko la watoto wa mitaani, wanaokimbia familia zao kukwepa kushuhudia au kuhusishwa katika migogoro na kukosa mahitaji muhimu.

Anasema kutokana na hali hiyo ndiyo maana TAMWA na taasisi washirika, wamejitosa kutetea ustawi wa waathirika wa tatizo hilo. Mmoja wa mapadri wa Shirika la Mapadri wa Afrika (White Fathers), Padri Baptiste Mapunda, anasema unywaji pombe wa kupindukia unachangia umaskini katika familia, kwani wanaume wengi wanatumia muda wao mwingi wa uzalishaji katika ulevi, badala ya kuzalisha mali.

Anasema taasisi kama TAMWA, CRC, TAWLA, TGNP na ZAFELA zinazowasaidia waathirika hasa wanawake na watoto, lazima zisaidiwe. Hivi karibuni Mtaalamu wa Magonjwa ya Akili ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa Sehemu ya Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza, Afya ya Akili na Dawa za Kulevya wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Joseph Mbatia alinukuliwa akilaumu unywaji wa pombe kupindukia, kwamba una madhara kiakili, kiuchumi na kijamii.

Katika baadhi ya maeneo mkoani Mara anapotoka mwandishi wa makala haya, bado kuna kasumba ya wanawake kushiriki uzalishaji mali, lakini wakiwa hawana haki ya maamuzi wala matumizi ya mali wanazochuma na ili kuzitumia. Badala yake, licha ya kuzalisha mali hizo, lazima wapige magoti kuomba kupewa kiasi, kadiri ya matakwa ya wanaume katika familia zao.

Mkazi wa Buhemba wilayani Tarime (jina tunalihifadhi) anasema amekuwa akilalamikiwa na mkewe mara kadhaa anapokuwa katika biashara ya dagaa ili kujikimu na watoto, yeye (mume) hufika katika biashara hiyo na kuchukua mauzo yote ili kwenda kutumia katika ulevi wa pombe na sasa anafanya juhudi za kuuza kiwanja.

Katika tukio la hivi karibuni lililoripotiwa katika Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi wilayani Tarime, mtu huyo aliyesuluhishwa na hatimaye mkewe kuomba yaishe, alituhumiwa kunywa pombe na kisha kuuza mabati yaliyoezekwa katika nyumba ili akalipe pombe. Hali hiyo ilisababisha vijana kadhaa kutumwa kwenda kuezua mabati na hatimaye mmoja wao kutiwa mbaroni pamoja na mtu huyo.

Wilayani Newala mkoani Mtwara wakati wa kilimo wanawake katika ndoa hushirikishwa kikamilifu katika uzalishaji, lakini ushiriki wao hufikia mwisho wakati wa mavuno na ndipo furaha kwao hugeuka kuwa maumivu. Gazeti la Sauti ya Siti Toleo Namba 33 la Juni 2013 limeandika kuwa hicho ni kipindi ambacho wanaume wengi, hutoa talaka kwa wake zao na kuoa wanawake wengi na ukatili huu wa kupindukia huitwa “kusafisha ghala”.

Linasema, “Ni wakati ambao kaya nyingi husafisha maghala kwa ajili ya mazao mapya, pia ni wakati ambao kaya nazo ‘husafishwa’ upya na katika zoezi hilo, wake wengi wa zamani nao hutalikiwa na kutoa nafasi kwa ‘wake wapya’ kuolewa.” Kasumba ya kusafisha ghala, uchunguzi umebaini kuwa huenda sambamba na unywaji wa pombe kupindukia, unaofanywa na wanaume hao huku mkoani Mara, ukale wa kupiga wanawake na watoto baada ya kurejea kutoka kilabuni, ukiwa unaendelea.

Mwandishi Christopher Gamaina wa wilayani Tarime anasema wanaume wengi wanawapora wake zao pesa, hata walizohangaika kuzitafuta na kwenda kunywea pombe. Lakini, dhambi wanayoifanya ni kwamba hata wanapowapora pesa zote, wakirudi nyumbani wamelewa, wanataka vyakula vizuri bila kujua vitatoka wapi, kama hawaachi pesa na pesa kidogo za kubahatisha zinazoweza kuwapo, wanawapora wake zao.

Kimsingi, haya ni miongoni mwa mambo yanayomfanya Msoka kusema kuwa haki ya wanawake kumiliki mali, haina budi kutazamwa upya, kutajwa katika katiba na kupewa nguvu za kisheria ili kuimarisha usawa wa kijinsia na ustawi wa umma.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Alexander Joseph

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi