loader
Picha

Umakini unahitajika kipindi cha mvua

Binafsi nasisitizia umakini kwenye kukabiliana na athari za mvua ambapo tayari watu kadhaa wameripotiwa kupoteza maisha.

Ni imani yangu kuwa kutakuwapo mikakati bora zaidi ya kuwaokoa wananchi walionasa kwenye nyumba zao, hapa namaanisha vikosi vya Zimamoto na Uokoaji pamoja na vya jeshi kutumia mbinu na vifaa vya kisasa katika kuokoa maisha ya waliokumbwa na maafa hayo.

Tofauti na ambavyo kwa sasa wanaonekana wananchi wakiwaokoa wenzao kwa kutumia njia ambazo sio za kiusalama zaidi. Lakini pia kamati za maafa nazo zitenge maeneo maalumu ya kuwasitiri wananchi ambao makazi yao yameathiriwa na mvua.

Hii ni kama ilivyowahi kufanyika miaka ya nyuma ambapo waathirika wa mafuriko walisitiriwa kwenye majengo ya shule.

Pia wazazi na walezi, ni vema kuwa makini zaidi katika kufuatilia watoto wao ambapo ni juzi tu kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda aliwataka wanafunzi wasiruhusiwe kwenda shuleni kutokana na mvua lakini wengi wao wakajikuta wamezagaa mitaani bila uangalizi wa walezi au wazazi.

Hii inaweza kuwa hatari zaidi kwa watoto kwa kuwa wanaweza kusombwa na maji au kupatwa na athari nyingine kadhaa zinazosababishwa na mvua.

Lakini pia kwa kuwa mvua inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa hasa kipindupindu, umakini zaidi unahitajika katika suala zima la ulaji na upikwaji wa vyakula.

Huku walaji wakitakiwa kuchagua nini cha kula na mahala pa kula ili kuepuka vimelea vya kipindupindu ambavyo ni dhahiri kuwa zimezagaa, wapikaji nao wanapaswa kuongeza umakini zaidi katika usafi.

Hii ni sababu kuwa kwa sasa wapo watu ambao wamefungulia vyoo na kutiririsha maji taka mitaani, kwao mvua hizi ndio mwanya wa kutiririsha maji taka mitaani na kuhatarisha uwezekano wa kulipuka kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Ili kukabiliana na hali hii maofisa afya kutokea mamlaka husika za afya mnapaswa kufanya ukaguzi ili kubaini wale wanaofungulia maji taka hayo na kisha kuwachukulia hatua stahiki.

Ikumbukwe kuwa kutokana na mvua hizi, suala zima la upatikanaji wa chakula linaweza kuathiriwa hivyo ni vema kwa kuhakikisha kuwapo kwa akiba ya kutosha ya chakula ndani. Hii itasaidia zaidi iwapo kama mvua zikiendelea na kusababisha ukosefu wa chakula kwenye magenge, akiba hiyo itasaidia kwa kipindi hicho.

MSIMU wa sikukuu za mwisho wa mwaka umewadia. Siku ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi