loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Unapofurahia ujana usisahau uzee

Umri haurudi nyuma, siku ikipita imepita, huwezi kulazimisha jana iwe leo, uzee haukwepeki, zitumie vizuri siku za ujana wako, fainali uzeeni, utavuna ulichopanda.

Nimeyasema hayo kwa sababu nafahamu changamoto za ujana, wapo waliopita salama na leo wanafurahi wanakula matunda, kuna walioharibikiwa kwenye umri huo sasa wanajuta, wanasema ningejua, wakumbuke majuto mjukuu.

Ney wa Mitego anasema, maisha yenyewe mafupi aachwe ale ujana, anajisifu kwa kukesha kwenye kumbi za starehe na akasema halali kama popo. Si hivyo tu, kijana huyo msanii wa muziki wa bongo fleva anajisifu kuwa akilewa anagawa bia, na akipenda anagharamia.

Msanii huyo anawakilisha uhalisia wa maisha ya vijana wengi ambao ukithubutu kuwakosoa watakuambia haikuhusu, kausha, fanya yako, nipotezee, nakula ‘bata’, Ulaya popote hela yako tu.

Wanaoishi maisha kama alivyoimba kijana huyo tunao kwenye familia zetu, mtaani kwetu, ni jirani zetu , kaka zetu, wadogo zetu, rafiki zetu hivyo ukiweza waulize maswali haya, ujana unaanzia wapi na unakwisha lini, na wamejiaanda vipi kwa maisha ya uzee?

Unapokula ‘bata’ leo kumbuka kuna uzee, na ukisema maisha yenyewe mafupi niambie pia utakufa lini.

Anayesema maisha ni mafupi muulize anayalinganisha na ya nani, maisha marefu ni yapi? Anataka aishi miaka mingapi ili aone maisha yake ni marefu?

Na hata kama maisha yangekuwa mafupi, jambo la msingi ni kustarehe tu, kulewa, na ngono tu? Utapata faida gani ukila ‘bata’ leo, halafu ukaishi maisha ya shida uzeeni?

Kumbuka ‘unajirusha’, ‘unajiachia’ na unayafanya hayo sasa kwa sababu bado una nguvu, umri unaruhusu, utafika wakati hutaweza kuyafanya, utakuwa mtazamaji tu kwa sababu ya uzee, utatamani kufanya mambo fulani haitawezekana, utajuta na kujilaumu, bado una nafasi, epuka majuto.

Tumia muda, fursa na kipato chako vizuri kujiwekea akiba ya kesho, usiishi kwa kuiga, kufuata mkumbo, au kwa shinikizo la ujana.

Kumbuka unaishi mara moja tu, umri ukipita haurudi, ulioyafanya jana ni historia, ya kesho fumbo, mwenye masikio na asikie, jiandae. bmsongo@hotmail.com

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi