loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Unaweza kuhudhuria kazini miaka 28 bila kukosa?

Jamii nyingi, tangu zama, walijijengea utaratibu wa kufanya kazi, kwa sababu bila hivyo ingekuwa vigumu kupata chakula, ambacho pengine ndiyo yalikuwa matumizi makubwa zaidi. Katika maisha ya leo yapo mengi zaidi ya chakula, kwa sababu ukiachilia mbali makazi, kuna mavazi, lakini linalowatumbukia nyongo wengi sasa ni gharama za elimu kuanzia ile ya chekechea hadi ya juu. Ni kwa msingi huo, ilitarajiwa watu wengi wangejijengea nidhamu ya kazi, ambayo ni msingi wa mafanikio bora kazini, na katika maisha kwa ujumla.

Na awali nidhamu ni kuhudhuria kazini, pili ni jinsi ya kutenda kazi yenyewe na utatu wake umelundika mambo mengi. Tuanze na hili la kuhudhuria kazini.

Kwamba ile tu kuiheshimu kazi na kufika, kwa kujinyima usingizi, mapumziko na starehe, ni jambo la msingi, la maana na wakati mwingine, kuendana na wingi wa utendaji, ni jambo kubwa.

Kwa Antonio de Sousa, kazi ina maana kubwa sana, na anaiheshimu na kuilinda kama anavyofanya kwa mboni ya jicho lake. Anaipenda.

Huyu ni mlinzi hotelini jijini Tampa, katika Jimbo la Florida nchini Marekani. Yaweza kuonwa na wanajamii wengine kuwa ni kazi ndogo, lakini ameiheshimu na bado anaendelea nayo.

Tunavyozungumza sasa amefikisha miaka 28 na ushee bila kukosa kazini kwa sababu yoyote ile. Hana cha kusema anaumwa kwa hiyo akae nyumbani baada ya kuwajulisha wakuu wa idara ya utawala na utumishi wala hana cha kusema mtoto ameachwa na gari ya shule hivyo anampeleka. Ni yeye na kazi, na kazi imemjibu vyema kwa kuamua ni yenyewe na yeye.

Anaendelea na kazi yake kwa furaha na kujituma kwa mwaka wa 28 sasa. Siku moja gari lake liliharibika njiani, akiwa kwenye ratiba ya kufika kazini ndani ya muda baada ya kutekeleza majukumu ya nyumbani kwake, kama ipasavyo katika jamii mbalimbali. Lakini lilipomfika hilo, ambapo wale wanaomwangalia kwa jicho pembe wakidhani alikuwa amepatikana, walikuwa wamekosea kabisa.

Sousa mwenyewe hakuingiwa hata na wazo la kuita gari livutalo magari mabovu au yaliyoharibika. Alichofanya Sousa siku hiyo, ni kulisukuma gari lake kando ya barabara, akafunga milango na kukimbia umbali wa maili tano hadi mjini ili kuwahi kwenye nafasi yake ya ulinzi kazini, katika Hoteli ya Hyatt Regency, kisha akatumia njia za kulishughulikia bila yeye kukosa kazini kwa muda wote aliotakiwa.

“Nilikuwa nimeloa jasho, lakini nilifanikiwa kufika katika muda unaotakiwa – saa tisa kamili,” anasema kwa furaha.

Na kweli furaha hiyo sio ya bure, kwa sababu pamoja na matatizo yote hayo ameitunza rekodi yake ya kutokosa kazini kwa zaidi ya robo karne. Naam, miaka ya mahudhurio timilifu. Huyu amekuwa mtu wa kawaida, na hata nyakati za mafuriko au milipuko ya magonjwa, ambapo watu wengi hufikia kutoa udhuru, yeye amekuwa ni wa kwenda kazini kama kawaida.

Imekuwa pia kawaida kwa baadhi ya watu kuona kwamba nyakati kama hizo, au hata katika mazingira tofauti, wanaona kwamba wale wa ngazi za juu ndio wanaotakiwa kuwa na mahudhurio mazuri zaidi. Lakini hali sio hivyo, hata wale ambao sio mameneja wanatakiwa kuwahi kazini, hasa katika maeneo ya uzalishaji, afya na utoaji huduma nyingine.

Wapo wengine ambao huitoroka kazi kwa kujidai kwamba wapo ‘field’, huku wengine wakisoma mfumo wa kampuni kujua kiongozi gani yupo wapi ili wapange utoro. Sousa (53) anasema yeye amejifungamanisha na kazi yake kwa sababu ndiyo iliyomfikisha alipo kwa kumpatia matumizi yote muhimu.

“Naipenda tu kazi yangu,” anasema Sousa ambaye kwa mujibu wa sheria za hesabu, amehudhuria kazini kwa karibu nusu ya umri wake. Anavuta kumbukumbu zake kuhusu nyuso za watu na mara wanapotembelea kazini kwake, yaani hotelini hapo, na kusalimiana, huku wakiulizana kuhusu biashara zao na maisha.

“Watu wanapenda kweli kuulizana kuhusu biashara zao na kujadili yatokanayo, navutwa na jinsi wanavyosalimiana na kuelezana biashara zinavyokwenda huku macho yakiwatoka wengine,” anasema Sousa.

Bosi wa Sousa, yaani meneja wa hoteli husika, Derrick Morrow, amezoea kumwita Sousa kwa jina la ‘Meneja wa Mtaa wa Tampa’. Ilivyo ni kwamba hoteli yenyewe ipo Mtaa wa Tampa, achilia mbali Jiji lenyewe la Tampa. Meneja Morrow anasema kwamba baadhi ya wateja wakubwa hotelini hapo wanasema kwamba hurejea tena na tena hapo kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni uchangamfu wa Sousa.

“Huyu (Sousa) ndiye mkuu wetu wa masoko kwa mstari wa mbele,” anasema meneja huyo. Wafanyakazi wenzake Sousa wanamtuhumu kwamba alifanya makusudi tarehe za kuzaliwa kwa watoto wake, ambapo ingekuwa nafasi kubwa kwao kushuhudia akikosa kazini kwa mara ya kwanza.

Ni kwamba Natalie na John walizaliwa siku ambazo Sousa alikuwa off, kwa hiyo hakuwa na sababu ya kuomba ruhusa kazini kwa sababu ya udhuru. Off yake ilipoisha aliingia kazini kama kawaida. Alisherehekea kuzaliwa kwa watoto wake kisha ilipofika saa tisa mchana kesho yake akaenda kazini kama kawaida.

“Ilitokea tu kugongana,” anasema Sousa, akikanusha madai ya kupanga siku za kuzaliwa watoto wake. Mkewe anaitwa Diane, na anafanya kazi kwenye duka la vitabu, na kwa kusaidiana pamoja, watoto wao Natalie (21) na John (23) sasa wamepita chuoni.

Makala haya yameandaliwa na SELEMANI NZARO kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

TANZANIA na dunia nzima kwa sasa ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi