loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Unyanyapaa ukitoweka, Ukimwi pia utaisha nchini’

Kiwango cha maambukizo ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi nchini kimepungua kutoka asilimia 13 mwaka 2000 hadi asilimia 7.8 mwaka 2007 na kwenda chini zaidi mpaka asilimia 5.1 mwaka huu 2013.

Licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na wahisani kuhakikisha Tanzania inafikia wastani wa kiwango sifuri cha maambukizi ya ukimwi, kuna baadhi ya watu katika jamii bado wamekuwa wakiendekeza tabia ya unyanyapaa kwa waathirika wa ukimwi na hivyo kuchelewesha mpango huo.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), takriban watu milioni 1.6 wanaishi na virusi vya Ukimwi Tanzania, huku watoto milion 1.3 wakipoteza wazazi wao kutokana na ugonjwa huo, hatua inayoashiria wazi kuwa bado kunahitajika nguvu za ziada kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa.

Ukweli ni kuwa tatizo la ugonjwa huo umezikumba familia nyingi hapa nchini kwa namna moja au nyingine lakini kwa kiasi kikubwa jamii bado imeshindwa kujipa ujasiri na kukubaliana nao na kuuona kama ugonjwa wa kawaida na hivyo kuchukua hatua za kupambana nao.

Hatua hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya waathirika kuwa na hofu ya kujitokeza hadharani na kujitangaza wazi kuwa wanaishi na ugonjwa huo wakihofia kunyooshewa vidole. Upo ushahidi wa kutosha kuwa wapo baadhi ya waathirika wa ugonjwa huo wameamua kukatiza tiba za dawa za kurefusha maisha kutokana na tatizo hilo la unyanyapaa uliokithiri hasa pale wanapogundulika kuwa wanatumia dawa hizo.

Wapo wengine ambao licha ya kutambua ukweli wa afya zao kuhusiana na ugonjwa huo wameamua kujificha kwa hofu ya kunyanyapaliwa na watu wao wa karibu au hata wale wanaofahamiana nao kwa namna moja au nyingine.

Pamoja na elimu inayotolewa na taasisi mbalimbali kuhusu maadhara ya unyanyapaa, bado jamii ya watanzania haijaelimika hivyo inaendelea kuleta majeraha kwa ndugu na jamaa wanaoishi virusi vya ukimwi au kuugua ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tacaids, Dk Fatma Mrisho, pamoja na kiwango cha unyanyapaa kuendelea kupungua siku hadi siku hapa nchini bado jamii ina nafasi nzuri kuhakikisha hali hiyo inatoweka kabisa na kufikia sifuri. Anasema unyanyapaa ndiyo changamoto kubwa iliyopo na kusisitiza kwamba endapo jamii itaendelea na utamaduni wa kuwanyanyapaa watu wenye kuishi na VVU, tatizo la ukimwi litakuwa gumu kumalizika katika jamii yetu.

Anasema sababu kubwa ni kwamba watu hawatajitokeza kupima kwa lengo la kujua afya zao ili waweze kuchukua hatua na badala yake kiasi cha maambukizi kinaendelea kukua. Endapo jamii italiona suala hilo kuwa la kawaida na kuepuka kunyoosheana vidole, wengi watajitokeza kupima na hivyo kupunguza maambukizi mapya.

“Malengo ni kwamba ifikapo 2020 kiasi cha maambikizi kiwe sifuri, hili litawezekana endapo kila mmoja atachukua hatua zinazostahili kuanzia sasa tukiamini kuwa tunaweza … na tuache kabisa kunyanyapaa wagonjwa,” anasema Dk Fatma. Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Tacaids, wadau mbalimbali yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wamejitokeza kushiriki katika kupambana dhidi ugonjwa huo kupitia kampeni mbalimbali wanazozifanya kwa ajili ya kutoa elimu.

Hata hivyo, unyanyapaa, tofauti na miaka ya nyuma, umepungua kwa kiasi kikubwa jambo linalochangiwa na elimu zinazotolewa na wadau hao, lakini elimu zaidi bado inahitajika.

Aidha Kama moja ya jitihada za kuongeza uelewa juu ya ukimwi, Rais Jakaya Kikwete pia alizindua kampeni ya upimaji wa hiyari wa Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi (VVU) kwa kutumia mwamvuli wa “Kilimanjaro Challenge” na kuitaka jamii kuachana na tabia ya unyanyapaa kwa waathirika pale wanapojitangaza kuishi na ugonjwa huo.

Kampeni hiyo ya utoaji elimu ya ukimwi ‘Kilimanjaro Challenge’ tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 na kuratibiwa na mgodi wa dhahabu (GGM), kwa kiasi fulani hadi sasa imesaidia kuleta mafanikio kwa wananchi, hususani katika kutoa elimu juu ya janga hili kwa lengo la kujenga jamii iliyo huru dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Hata hivyo, tatizo la unyanyapaa halitajwi kuwepo Tanzania pekee bali hata kwenye mataifa mengine ya ndani na nje ya Bara la Afrika ambapo kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, nchi ya India pia ni moja ya nchi ambayo watu wake wengi wanapoteza maisha kutokana na hali hiyo ya unyanyapaa.

Shirika lisilo la kiserikali linapambana na maambukizi ya VVU nchini India lijulikanalo kama ‘The Delhi Network of Positive People” (DNP+), limetaja changamoto zinazolikabiili katika kazi ya kusaidia waathirika wa ugonjwa huo kuwa ni uhaba wa fedha na Loon Gange ambaye ni rais na mwanachama mwanzilishi wa DNP+ anasema kuwa ameshuhudia watu wengi wakiaga dunia kwa sababu hawakutibiwa kutokana na uhaba wa fedha na wengine kuona haya kujitokeza kutokana na unyanyapaa.

Kimsingi kama jamii itaungana kwa pamoja na kuamua kushirikiana kwa nia ya kuutokomeza ugonjwa huu, silaha kubwa ni kuachana na unyanyapaa, hatua ambayo pamoja na taasisi zinazoshughulika na mapambano ya ugonjwa huu inaaminika kwamba mafanikio yatapatikana.

Mkakati wa Serikali wa kufikia kiwango sifuri cha maambukizi ifikapo Mwaka 2020 utafanikiwa kama hatua stahili ikiwemo ya kupinga unyanyapaa zitachukuliwa.

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi