loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ushauri wa Mkapa uwe somo kwa nchi za Afrika

Katika hoja yake hiyo ambayo sisi tunaiunga mkono, Mkapa amesema wataalamu hao wana mchango mkubwa na wamefanya tafiti mbalimbali, hivyo wanapaswa wasipuuzwe.

Mkapa aliyasema hayo juzi wakati akifungua Mkutano wa Wataalamu wa Jiolojia, kutoka nchi takribani 42, barani Afrika. Alisema Waafrika wasipoangalia vizuri, suala la mafuta na gesi, linaweza kuwa chimbuko la vita na kwamba ni lazima wanasayansi wa masuala mbalimbali wakapewa kipaumbele kwenye utungaji sera, kwani wamefanya tafiti nyingi ingawa kwa sehemu kubwa hazizingatiwi.

Mbali ya hayo, Mkapa alisema jamii za nchi za Afrika, hazijaelewa vya kutosha mchango wa wanasayansi katika nyanja za jamii, siasa na uchumi na kwamba maendeleo yanahitaji rasilimali zikiwemo ardhi, kama vile madini, lakini wataalamu wa jiolojia pamoja na tafiti zao nyingi, hawajapewa nafasi ya kutosha.

Tumelazimika kuiunga mkono hoja hii ya Mkapa kutokana na ukweli kwamba miongoni mwa sababu zinazochelewesha maendeleo ya nchi nyingi za dunia ya tatu, Afrika ikiwemo, ni kutozingatia ushauri wa wataalamu kwa tafiti mbalimbali wanazozifanya.

Kwa Bara la Afrika, siasa zimekuwa zikipewa nafasi kubwa katika uandaaji, upitishaji na utekelezaji wa sera mbalimbali na mara nyingi ushauri wa wataalamu kuhusu sera hizo umekuwa ukipuuzwa na wanasiasa ambao wengi wao huwa na elimu ya chini au ya kati na hivyo kuwa na uelewa mdogo.

Kama alivyosema Mkapa, kwa suala kubwa linalohusu mafuta na gesi, ni lazima sasa Afrika iweze kubadili mtazamo ili sera kuhusu rasilimali hizo zikasimamiwa na wataalamu katika ngazi zote za utekelezaji wake na wanasiasa wasipewe nafasi kubwa kama ambavyo imekuwa inafanyika mara kadhaa kimakosa.

Hatuna sababu ya kuendelea kufanya makosa haya kwani tumejifunza mara kadhaa kutoka kwa nchi mbalimbali za Afrika namna ambavyo sera zilizopitishwa kwa kuzingatia maslahi ya kisiasa kwa masuala yanayohusu rasilimali muhimu kama mafuta na gesi, zilivyogeuka kuwa chimbuko la vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hizo.

Ni imani yetu kwamba wakati maeneo mbalimbali ya Afrika yakiendelea kugundulika kuwa na utajiri mkubwa wa gesi na mafuta, Tanzania ikiwemo, waandaaji na watekelezaji wa sera watakuwa makini katika kuzingatia ushauri huu wa Rais mstaafu Mkapa wa sera zao kuzingatia mahitaji ya kitaalamu zaidi ya siasa.

Hilo lisipofanyika upo uwezekano mkubwa wa kila siku nchi za Afrika zikawa katika migogoro, hatua ambayo inawapa urahisi maadui wanaouangalia utajiri huo wa Bara la Afrika kwa jicho la husuda kupata nafasi ya kujipenyeza na kuchochea migogoro ili kuweza kupata mwanya wa kuiba rasilimali hizo kirahisi.

Kwetu sisi tunaamini kuwa pamoja na changamoto za kuwa na uchache wa wataalamu, lakini nchi hizo za Afrika zinaweza kuongeza nguvu katika kuwajengea uwezo wataalamu wao katika kuhakikisha kuwa wanakuwa na utaalamu wa kutosha wa kuendesha sekta ya gesi na mafuta.

Kwa nafasi ya pekee tunapongeza hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na Tanzania katika kufanikisha hilo kwa kuwawezesha Watanzania kujifunza ili kubobea katika masuala yanayohusu mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali vya kimataifa katika azma yake ya kuhakikisha kuwa inakuwa na wataalamu wa kutosha ifikapo 2020.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: MHARIRI

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi