loader
Dstv Habarileo  Mobile
USSY CHARUGAMBA: Mwanasheria anayetamba katika Injili

USSY CHARUGAMBA: Mwanasheria anayetamba katika Injili

Kwa kulitambua hilo, wapo baadhi ya wadau wa muziki ambao ndoto zao kila siku ni kufanya mazuri kwa maslahi ya Taifa kwa bidii ili liwe katika ramani nzuri kimataifa katika tasnia ya muziki. Ussy Charugamba ni mwanamuziki wa Injili mwenye makazi yake mkoani Morogoro ambaye amepania kuhakikisha anafanya mazuri katika muziki huo pamoja na kusaidia vijana chipukizi wenye vipaji ili kuendelea kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa njia ya uimbaji.

Anasema: “Najua kuwa wapo wasanii wengi vijana mtaani lakini hawana uwezo wa kuingia studio kurekodi, wanatamani kupata nafasi ili angalau kufikisha ujumbe wao kwa jamii kwa njia ya uimbaji. Katika kutimiza malengo yake ya kuwasaidia vijana tayari ameanzisha asasi inayojulikana kwa jina la Furure Organization for the Young People (FOYO) Development Programme’ ili kukamilisha lengo hilo lake.“Naamini naweza kuwainua wasanii chipukizi wenye malengo kwani Morogoro vipaji vipo vingi katika nyanja ya muziki huu na ninaweza kuwafikia wengi kupitia organization yangu,” anasema.

Anasema taasisi hiyo ataizindua rasmi kuanzia mwakani mkoani humo akiwa na matumaini ya kupata vijana wengi kwa ajili ya kufanya nao kazi. Charugamba anasema amekuwa akiona jinsi vijana wengi wanavyopata shida hasa katika kutafuta nafasi ya kutoka, hawapati sapoti yoyote kwa jamii inayowazunguka.

Anasema mara baada ya kuizindua anategemea kuwasaidia vijana wengi wa mkoani kwake watatimiza ndoto zao. Licha ya kuwa na nia ya kuwasaidia vijana yeye mwenyewe anajivunia kuwa na kipaji ambacho kinakubalika kwa mashabiki wa muziki huo sio tu kwa upande wa Morogoro, bali Tanzania yote.

Anasema uimbaji wake umewasaidia wengi wanaosikiliza nyimbo zake kupona kiroho, kwani wanaelimika, wanaburudika, lakini pia wanabadilika kutoka kwenye matendo yasiyofaa na kutenda yanayompendeza Mungu. Msanii huyo ni tofauti na wengine ambao wamekuwa wakihama mikoa kwa ajili ya kufanya kazi ya muziki. Ingawa ni mzaliwa wa Mkoa wa Kagera, anaishi Morogoro kikazi na familia yake, lakini ndiko anakofanyia muziki.

Historia yake

Charugamba ni msanii mwanasheria aliyehitimu Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2004 baada ya kumaliza elimu ya sekondari katika Shule ya Tambaza Dar es Salaam.

Anasema alizaliwa miaka 36 iliyopita wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera ambako alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Umoja wilayani huo. Alianza kazi ya muziki mwaka 2000 ambako alirekodi wimbo wa muziki wa kizazi kipya uliojulikana kama ‘Mapenzi matamu’ ambako baadaye aliamua kuachana na muziki huo.

Sababu kubwa iliyomfanya kuachana na muziki wa kizazi kipya anasema aliamua kubadili mtindo wa maisha yake kwa kuokoka ili kuachana na mambo ya kidunia. “Baada ya kuokoka niliachana na muziki wa kizazi kipya ambapo kwa sasa namshukuru Mungu nimekuwa nikiwaelimisha watu kupitia uimbaji wangu,” anasema.

Tangu ameanza muziki wa Injili tayari ametoa nyimbo nyingi ambazo zimekuwa zikimtambulisha katika ulimwengu wa muziki huo na kukubalika kwa haraka kwani amekuwa akiwavutia mashabiki wake. Amewahi kuvuma na ngoma zake kadhaa kama Tawala Bwana Yesu na nyingine nyingi.

Kwa sasa anajivunia kukamilisha albamu yake ya kwanza chini ya mwandaaji Ezekiel William katika Studio ya Easy Production mjini Morogoro. Charugamba anazitaja nyimbo zilizoko kwenye albam hiyo kuwa ni Mtegemee Mungu, Namshukuru Mungu, Nakuabudu Bwana, Usikate tamaa, Nakupenda Bwana, Dhuruba melini na Haki kwa Yesu.

Msanii huyo anasema amekamilisha albamu hiyo yenye nyimbo nane itakayozinduliwa rasmi Desemba 22, mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambako anatarajia kuwaalika wasanii wengine kwa ajili ya kumuunga mkono. Charugamba anasema anaamini kupitia yeye vipaji mbalimbali vya muziki wa Injili vinaweza kuonekana na kutikisa nchi katika tasnia ya muziki huo ambao unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki.

“Nawaomba wapenzi wa muziki wa Injili waje kushuhudia onyesho ‘live’ la albamu yangu nikisindikizwa na wasanii wenzangu kwani bado maandalizi yanaendelea kuelekea tamasha hilo,” anasema Charugamba. Anasema anategemea kutokana na maandalizi mazuri aliyofanya kabla ya kutengeneza kazi yake, mashabiki watamuunga mkono.

Malengo yake

Kama ilivyo kwa wasanii wengine wa muziki, anasema licha ya kuwa ni mwanasheria, malengo yake makubwa ni kuwa msanii wa kimataifa wa nyimbo za Injili pamoja na kumiliki bendi yake. Anasema ikiwa atafanikisha kuwa na bendi, baadaye itamsaidia kupiga muziki wa ‘live’ pindi anapoalikwa kwenye shoo zake mbalimbali ndani na nje ya nje.

Jambo kubwa anaomba wasanii wenzake wote wa Morogoro na kwingineko kuwa na umoja hususani wakati wa matamasha kwa kutiana moyo wenyewe kwa wenyewe, kwa kuondoa tofauti ili kufika mbali. Pamoja na hilo, anawasisitiza wasanii wote wasikate tamaa, kwa kuwa kila kitu kinawezeka, kwani hata yeye licha ya kukumbana na changamoto katika muziki wa Injili ataendelea kupambana ili kutimiza malengo yake aliyojiwekea.

Changamoto

Charugamba anabainisha kuwa anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha ya kurekodia ambapo gharama zimepanda hususani katika studio maarufu. “Sisi wasanii tulioko mikoani tunashindwa kupata ushirikiano kutoka kwa wasanii wakubwa pale tunapotaka kuwashirikisha maana wanatuomba fedha nyingi ambazo wanajua tunaweza kukwama, kuzipata,” anasema Charugamba.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi