loader
Dstv Habarileo  Mobile
Utaalamu na siasa vitenganishwe kusaidia wakulima

Utaalamu na siasa vitenganishwe kusaidia wakulima

Je ni kweli kuwa mbolea hii haifai? BEDA MSIMBE anazungumza na wataalamu na watengeneza mbolea wenyewe kuhusu ubora wake.

‘MAZOEA yana hatari sana yanapofanywa kuwa kanuni na ada za kuishi’, alishawahi kuniambia baba yangu John Luwanda, mtangazaji wa zamani wa Radio Tanzania. Nchini Tanzania kwa miaka zaidi ya 50 mbolea iliyozoeleka sana ni DAP ambayo, umaarufu wake katika maeneo ya kilimo sio wa kusimuliwa.

Ndio kusema kuna mazoea makubwa na mbolea hiyo kiasi ya kwamba kunapotakiwa mabadiliko mfumo wake hudhaniwa kuwa ndio kanuni na ada. Ni kutokana na mazoea hayo hayo, wanasiasa na wataalamu wamekuwa wakisigana kuhusu mbolea ya minjingu.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chizza alisema kuna haja ya kutumia busara katika kuzungumzia mbolea na matumizi yake, lakini Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye akasema waziri huyo ajiandae kujibu maswali katika Kamati Kuu.

Mbolea ya minjingu ambayo inazalishwa na Minjingu Mines and Fertilizer iliyopo barabara ya Dodoma Arusha mkoani Arusha kwa sasa imeboreshwa zaidi kuliko ilipoanza kutumika miaka michache iliyopita kwa kuzingatia mahitaji halisi ya udongo nchini Tanzania. Katika mazungumzo na mmoja wa wataalamu wa kilimo ambaye amestaafu Dk Mshindo Msolla anaamini kwamba tatizo lililopo sasa sio la mbolea bali elimu darasa ya matumizi ya mbolea hiyo ambayo ina manufaa makubwa nchini.

“Sio suala la ushabiki, lakini mbolea hii ina manufaa makubwa kwa Tanzania kutokana na bei na mahitaji ya virutubisho nchini,” alisema Dk Msolla. Mtaalamu huyo ambaye ni miongoni mwa watu waliowezesha mfumo wa mbolea kufika vijijini kutoka wilayani alisema kwamba, kelele za sasa kuhusu ubaya wa mbolea hiyo anaamini yanatokana na mazoea na wataalamu hawana budi kuendelea na shamba darasa ili watu waelewe kinachotakiwa.

“Wakati DAP iliyozoeleka kwa miaka 50 sasa ina naitrojeni asilimia 18 na fosfate asilimia 46, minjingu mazao ukichukua mifuko miwili kwa eka inayoshauriwa ina naitrojeni asilimia 20 na fosfate 40,” alisema Dk Msolla na kuongeza kwamba ina virutubisho vingi ikiwamo salfa. Alisema virutubisho vilivyomo katika mbolea hiyo vimeongezwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya udongo wa Tanzania.

“Minjingu ya zamani ilikuwa na fosfate tu, ilikuwa ya unga na ilihitaji unyevunyevu na tindikali ya udongo ilikuwa iwe chini ya asilimia 5, wakulima walilalamikia vumbi na wataalamu wakasema lazima ijibu mahitaji ya wakulima ndipo ikaletwa Minjingu mazao” alisema Dk Msolla na kuongeza watu wanapozungumzia kwamba haifai ni lazima waseme ni kwa namna gani.

Katika taarifa ya bei, minjingu inaweza kufika Sh elfu 60 hadi inafika Kigoma wakati sasa hivi Kigoma wananunua DAP kwa Sh 120,000. “Mbolea ya minjingu ambayo ni oganiki na inasaidia ardhi kujirekebisha na tofauti kubwa sana na mbolea za kiwandani,” anasema ofisa mmoja wa Minjingu ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.

Anasema mbolea hiyo pamoja na kuipa virutubisho vinavyohitajika katika udongo kama vitamin, inawezesha wadudu wanaotengeneza uhai wa udongo kuendelea kuwapo huku ikihakikisha kwamba fosfate ipo muda wote.

Pamoja na wakulima wa Ileje na kwingineko kutaka kuambiwa ukweli kuhusu mbolea hii ya minjingu na majibu ya wanasiasa katika kulumbana kwao kwamba asilimia 80 ya watu waliozungumza katika mikutano ya CCM hawakuwa na uzuri bali ubaya, bado wataalamu wanasema mbolea hiyo imetengenezwa kutumika katika udongo wa Tanzania.

Wataalamu wanasema kwamba wakulima wanaotumia minjingu kwa maelekezo watavuna mambo mazuri na kama kuna tatizo katika mbolea suala ni wataalamu kuangalia kuna kasoro gani.

“Katika matumizi ya mbolea kuna mazoea na watu wanapoletewa kitu ambacho hawana mazoea nacho ni vyema wakauliza wataalamu kwa kuzingatia maeneo yao,” anasema ofisa wa Minjingu. “Mimi nadhani ni kutokuelewa. Kunaweza kuwapo mambo mengi mchanganyiko kama hali ya udongo, mvua,” alisema ofisa huyo na kuongeza kuwa mbolea ya sasa ni matokeo ya utafiti na ni vyema watu wakafanya utafiti kabla ya kuanza kuzungumza.

Taarifa zilizopo kwamba sehemu kubwa ya udongo wa Tanzania ilipimwa miaka 20 iliyopita na sasa unafanyika upya ili kuujua unahitaji nini. “Mbolea ya minjingu mazao imelenga kupandia na kukuzia, kuupa mmea unaotaka nguvu imara ya kukua,” anasema Dk Msolla na kusema inafaa wakulima wakaelezwa kuwa ni lazima wajue tabia ya mbolea namna ya kuweka, kuichanganya kabla ya kutia mbegu.

Kimsingi mtaalamu huyo anataka kuangaliwa kwa tabia za kilimo na si kawaida ya tunalimaje. Ni dhahiri kuingia kwa minjingu mazao katika miaka ya karibuni kunaleta ushindani mkubwa kwa DAP hasa kwa kuzingatia kwamba ndio mbolea ambayo wakulima wengi wameizoea na wanaiona inatoa matokea haraka kuliko mbolea nyingine kama NKP na Urea hasa kwa kiwango chake cha Naitrojeni ambacho ni kwa ajili ya kukua na kuweka ujani na kutoa mmea wenye nguvu.

Mkulima mmoja wa mpunga Dakawa, Ng’atighwa yeye katika mazungumzo alikuwa anatamani kurejeshwa kwa mbolea ya minjingu ya unga kwani ilikuwa inamsaidia katika kilimo chake. Mbolea hiyo kwa sasa haipo sokoni lakini wakulima wengine walikuwa wanaiona inafaa kutokana na tabia yake ya mwakani kutoa mazao zaidi hasa kwenye majaruba.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya kutengeneza mbolea ya Minjingu ,Tosky Hans, alisema kwamba bado wanachambua taarifa mbalimbali za wakulima kuhusiana na uwezo wa minjingu mazao shambani ingawa kitaalamu inaonesha kuwa na mafanikio makubwa.

“Minjingu Mazao ni zao jipya la mbolea ikiwa na naitrojeni na hivyo kuwa sambamba na DAP katika masuala ya upandaji,” anasema mtendaji huyo na kuongeza kwamba wakulima wengi wanataka mbolea zilizoagizwa toka nje kutokana na kasi yake ya kufanyakazi. DAP ikiwa na fosfate asilimia 46 inasaidia kukuza kwa kasi mmea huku naitrojeni yake ya asilimia 18 inafanya mmea kuwa kijani. Minjingu ya zamani ilikuwa na asilimia 30 ya fosfate.

”Kwa maoni yangu ya jumla kuhusu usambazaji wa teknolojia za kilimo, nguzo kubwa ni watumishi wa ugani ambao hata hivyo kwa sababu hawana motisha, hawafanyi kazi ya uelimishaji ipasavyo. Mbolea ya minjingu mazao imekuwa ikitumiwa na wakulima kwa takribani miaka mitatu na wengi wameifurahia. Kwa maeneo yale ambayo wakulima wanalalamika, ushauri wangu ni kwamba kiwanda kwa kushirikiana na halmashauri husika waangalie sababu kama ni sifa ya udongo au hali ya hewa au vyote,” amesema Dk Msolla.

Wakati wataalamu walikutana Mei mwaka huu kuzungumnzia majaribio na tafiti mbalimbali za udongo mkoani Iringa, ni busara zaidi kuwauliza wataalamu kunatokea nini kwani matumizi ya mbolea nchini bado ni madogo sana.

Tanzania kwa sasa tafiti zinaonesha kwamba inatumia kilo 15 za mbolea kwa hekta , tukiwa nyuma ya Azimio la Arusha la kilo 50 kwa hekta kelele za wanasiasa dhidi ya wataalamu waziwazi haziwezi kutufikisha kokote, ndio maana wanatakiwa wataalamu wa ugani kila kijiji kusaidia wakulima kufanya mambo kitaalamu.

“Kama kweli tunataka Wizara ya kilimo kutekeleza Ilani ya chama tawala sawasawa kwa ahadi ya kuongeza matumizi ya mbolea kwa wakulima wadogo wataalamu wanatakiwa kusikilizwa, tuache blaa blaa,” anasema Giovanni Brian wa Ddodoma.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi