loader
Dstv Habarileo  Mobile
Utalii unavyoing’arisha Zanzibar

Utalii unavyoing’arisha Zanzibar

Nyota wa soka wa Afrika hawajifichi, maana machachari yao huonekana dimbani, ambapo tangu zama, wamiliki au mawakala wa klabu kubwa za Ulaya walimiminika Afrika kutafuta wachezaji. Ni kweli kwamba kwa Uingereza, hasa England, bei ya mchezaji mzawa ambaye ni mzuri kwenye Ligi Kuu (EPL) haishikiki hata kama si mahiri sana, lakini kwa Afrika, waliokwishaonesha vipaji vya hali ya juu na kung’ara mchezoni watazichezea noti barabara.

Ukiona kwenye klabu fulani hakuna mwanasoka Mwafrika au walau mwenye asili ya bara hilo, jua kwamba klabu hiyo ina tatizo ama ya kumaizi uwezo wao au kuna ubaguzi wa aina fulani. Kipaji, kujituma na kupanda chati kwa wachezaji ndivyo vitu vinavyookoteza sifa na kujenga msingi wa malipo makubwa kwao, na hakuna tofauti kwa wachezaji hao wa Afrika.

Si nia ya makala haya kuzungumzia kuhusiana na soka, ama Ligi Kuu England. Hapana, achana na hayo, wala haina uhusiano wowote ule, bali nilitaka msomaji wangu twende sawa ufahamu kwamba vipo vitu vingine vizuri vinavyoweza kukupa raha hapa hapa Tanzania.

Hamishia mawazo yako Kisiwani Zanzibar, ambako kuna visiwa viwili vya Unguja na Pemba na ipe nafsi yako imani kwamba kisiwa hicho kimetulia vya kutosha na ni sehemu tulivu ya wageni kutoka Ulaya, nilikotangulia kueleza sifa zake kwenye mambo ya soka na kwenda kisiwani Zanzibar kupumzika.

Ofisa Mipango wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk Miraji Ukuti Ussi anasema hivi sasa mchango wa sekta ya utalii kwa Pato la Taifa (GDP) Zanzibar umefikia asilimia 27 na unachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni. “Kwa hiyo utaona jinsi gani utalii ulivyo muhimu kama tutautumia ipasavyo na hiyo ndiyo dhamira yetu kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Anasema utalii ni sekta muhimu sana kwani nchi zote duniani zinajihusisha kwa njia moja au nyingine na biashara hiyo ambayo hufanywa kwa malengo mbalimbali yakiwemo ya kujifurahisha kwa kutembelea mandhari za kuvutia. Anasema kwa upande wa Zanzibar malengo ya kuendeleza sekta ya utalii yamekuwa yakibadilika kwa awamu na historia inaonesha kabla ya mapinduzi sekta hiyo ililenga zaidi kujenga uhusiano na urafiki.

“Zanzibar imejaaliwa kuwa na hali ya hewa mwanana, mandhari na fukwe nzuri pamoja na tamaduni ambazo si aghlabu kuzikuta katika eneo lolote jingine katika maeneo ya mwambao na nchi zilizomo katika bahari ya Hindi,” anasema Dk Ussi.

Kamishina huyo anasema sekta hiyo sasa imetoa mchango wa ajira ya moja kwa moja kwa vijana 13,017 na zaidi ya ajira 45,000 kwa zile nafasi zisizo na uhusiano wa moja kwa moja na kwamba matarajio ni kuwa zaidi ya asilimia 50 ya waajiriwa Zanzibar watatokana na sekta ya utalii ifikapo mwaka 2020.

Anasema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk Ali Mohammed Shein inatilia mkazo sana mambo ya utalii, hivyo wanaamini watapiga hatua kubwa kwa jambo hilo. Anasema dira ya mwaka 2020 na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupungunza Umasikini Zanzibar (Mkuza) kwa pamoja vinalenga kufikia ukuaji wa uchumi utakaowajali wananchi na zaidi masikini.

Pia anasema mkakati huo umeainisha kwamba sekta za utalii na biashara ndizo mihimili mikuu katika ukuzaji huo. “Hivyo ni wazi kwamba utalii una jukumu kubwa katika ukuzaji uchumi wa Zanzibar na kupunguza umasikini,” anasema na kuongeza kuwa ndiyo sababu sekta hiyo inachangia GDP kwa asilimia 27 na fedha za kigeni asilimia 80.

Anafafanua kuwa tokea kuanzishwa sera za kukaribisha vitega uchumi na sekta binafsi, asilimia 80 ya miradi iliyotekelezwa ni ile ya sekta ya hoteli na huduma za utalii ikiwa katika viwango mbalimbali.

“Jumla ya hoteli 454 na nyumba za kulaza wageni zenye vyumba 7,421 viliweza kuhudumia kiasi cha wageni 169,223 kwa mwaka 2012,” anasema. Pia anasema kampuni za kuongoza watalii zimeongezeka na kufikia 214 na kwamba huduma za usafiri wa ndani nazo zimeimarika na zile za usafiri wa anga na majini nazo zimeongezeka.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawekezaji Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), Abdulsamad Said Ahmed, anasema sekta hiyo hivi sasa imepanuka na kumekuwa na mafanikio makubwa zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita.

“Tunataka miaka michache ijayo, ukizungumzia utalii Zanzibar, basi ni kitu kinachoingiza fedha nyingi kwenye pato la Taifa kuliko hivi sasa. “Tunaamini kama tukiwekeza kwa nguvu kubwa basi utalii utaikomboa sana nchini yetu na hilo ndilo kubwa tunalodhamiria,” anasema Ahmed.

Kauli kama hiyo pia inazungumzwa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waongoza Watalii Zanzibar (ZATO) Hassan Ali Mzee, ambaye anaeleza kuwa kwa sasa utalii unaing’arisha kwa kiasi kikubwa Zanzibar. Anasema kuongezeka kwa watalii kunasaidia kuongeza pato kwa kuwa mtalii mmoja atalazimika kulipa dola za Marekani 95 anapoingia nchini hata kama hatalala.

“Dola 50 ni kwa ajili ya viza na dola 45 wakati anaondoka kurejea kwao. Hivyo hiyo ni mchango achilia mbali ile ya kulala katika hoteli ambako atalipia, pia akila chakula atalipia,” anasema Mzee.

Kwa mujibu wa Dk Ussi, hatua ya kukuza sekta ya utalii kibiashara zilianza kuchukuliwa kwa kasi kubwa ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa kamisheni ya utalii Juni mwaka 1992 ikiwa na majukumu ya kusimamia , kuendeleza mipango ya utalii Zanzibar na pamoja na kuitangaza Zanzibar kama kituo cha utalii ndani na nje ya nchi ili kuufanya utalii kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi.

Anasema mafanikio ya utalii ngazi ya kimataifa ni kupatikana kwa tuzo maalum ya Zanzibar kuwa kisiwa bora kiutalii kwa mwaka 2004 kwa Bara zima la Afrika, kanda ya Mashariki na Kati.

“Aidha tuzo ya Startarvel R.U ni aina ya tuzo iliyoipatia sifa Zanzibar katika kutathmini namna ya matumizi bora ya rasilimali za utalii, tuzo hii ilipatikana mwaka 2012 katika soko la utalii la Ulaya ya Mashariki baada ya Zanzibar kushiriki katika maonesho ya utalii ya kimataifa nchini Urusi.

“Kwa upande wa sekta binafsi ambao ni wadau wakubwa na muhimu katika sekta ya utali, nao wameweza kutumia vyema rasilimali za utalii sio kutuletea fedha za kigeni tu bali hata sifa kemkem. “Ni faraja iliyoje kwamba hakuna mwaka ambao kisiwa cha Chumbe kilikosa kufika fainali katika kuwania tunuku yoyote ile,” anasema Dk Ussi.

Anasema matumizi ya mtalii kwa siku yameongezeka Zanzibar kutoka wastani wa dola za Marekani 15.5 mwaka 1996 kufikia dola za Marekani 362 mwaka 2010. Huduma za usafiri wa anga na baharini nazo zinmeongezeka na kuimarika kati ya Zanzibar na nchi za nje, Zanzibar na Tanzania Bara na kati ya Visiwa vya Unguja na Pemba na kwamba kumekuwa na ongezeko la watalii wanaoingia Zanzibar.

Kwa upande wake Meneja Mauzo na Masoko wa hoteli ya Hideaway upande wa Afrika Mashariki, George Kiruku alipongeza kuimarika kwa sekta ya utalii na kwamba kumesababisha kuwepo kwa hoteli za kuvutia hivyo kuzidi kuwapa hamu watalii kutembelea Zanzibar.

“Zanzibar sasa ni tulivu na inavutia kuwekeza kwenye biashara ya hoteli maana watalii wamekuwa wakimiminika kwa kiasi kikubwa,” anasema na kuongeza kuwa hoteli yake ambayo bado mpya ikiwa na hadhi ya daraja la juu imekuwa ikipokea watalii wengi wa kutosha.

Kauli kama hiyo inazungumzwa pia na Meneja wa Hoteli ya Diamond Dream of Zanzibar, Allan Ochner, anayesema Zanzibar kwa sasa imekuwa kivutio kikubwa cha watalii. Meneja huyo ambaye ni mzaliwa wa Mombasa, Kenya, anasema Serikali imejenga mazingira mazuri ya watu kuwekeza Zanzibar kwenye hoteli na kwa kiasi kikubwa kukiwa na hoteli za kuvutia watalii nao wanaongezeka.

Kwa upande wake, Meneja wa Hifadhi ya Msitu wa Jozani Ghuba ya Chwaka, Ally Ally Mwinyi anasema kuna vitu vingi ambavyo watalii wanaweza kwenda kuviona Zanzibar ikiwemo kima wekundu ambao hawapatikani sehemu yoyote duniani.

“Msitu wa Hifadhi ya Jozani ni kivutio kikubwa cha watalii, wamekuwa wakifika hapo kuona vivutio mbalimbali vilivyopo eneo hilo. Anasema hifadhi hiyo ya miti ya asili yenye ukubwa wa hekta 5,000 ni sehemu inayovutia watalii wengi kwenda pamoja na watafiti kupita kufanya tafiti zao.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Amir Mhando

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi