loader
Dstv Habarileo  Mobile
Utamaduni wa kurithishana watoto majina unapotea?

Utamaduni wa kurithishana watoto majina unapotea?

Hii ni kutokana na hali halisi ya mabadiliko ya teknolojia yanayofanya dunia kuwa kijiji kimoja na hivyo kuwa rahisi sana tamaduni za mataifa mbalimbali kuingiliana. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopelekwa mbio na upepo wa mabadiliko yanayotokana na utandawazi unaoathiri tamaduni zake ambapo vizazi vya miaka ya karibuni vimekuwa na mitazamo tofauti kuhusu mila na desturi zao.

Mitazamo hii inakifanya kizazi cha sasa kiweke pembeni baadhi ya taratibu za kimila na kufuata za mataifa ya nje, hususan ya Magharibi. Baadhi ya vijana wamekuwa wakishawishika kuiga mila za nje, wakiamini kwamba pengine ndio kwenda na wakati na kwamba kufuata mila na desturi zao kulingana na makabila yao ni sawa na kubaki nyuma ya wakati.

Picha ya nini kitatokea katika mila za makabila mengi nchini kadri siku zinavyokenda inaanza kujionesha katika mambo mbalimbali, moja wapo likiwa ni hili la kuwarithisha watoto majina ya bibi na babu zao. Muingiliano wa ndoa, kwa maana ya mtu wa kabila hili kuolewa na wa kabila lile ni jambo lingine linalochangia watu kuzidi kuacha utamaduni wa kurithisha majina ya mabibi na mababu zao.

Kutokana na kinachotokea sasa kwamba si wazazi wote wanafuata matakwa ya mila za makabila mengi ya Tanzania kuwarithisha watoto majina ya bibi na babu zao, baadhi ya waliozungumza na mwandishi wa makala hii wameeleza ni kwa nini wamewapa watoto wao majina tofauti na ya wazazi wao.

Kati ya watu 10 niliowahoji kwa nyakati tofauti, kuhusu kama wanafuata mila na desturi na pia kama bado kuna umuhimu huo, tisa walisema wanafuata na kwamba umuhimu upo. Lakini mmoja alisema kwa sababu amekulia katika familia ya kidini nje ya nchi, hakupata nafasi ya kujifunza chochote kuhusu mila na desturi za Kitanzania.

Hata hivyo, alipoulizwa endapo angepata watoto pacha wa kike na wa kiume angewapa majina ya nani? Kijana huyo (hakutaka kutaja jina lake) alisema wa kike angemwita jina la mama yake mzazi aitwaye Gwantwa na wa kiume angemwita jina la baba yake mzazi, aitwaye Timothy.

“Majina haya hayana maana yoyote ya kidini au kimila kwangu, isipokuwa ni imani yangu kuwa kuwapa watoto majina ya wazazi kunaonesha upendo wangu kwa baba na mama yangu hasa ikizingatiwa kuwa wamekwishatangulia mbele za haki kutokana na ajali ya gari mwaka 1994,” anasema kijana huyo.

“Nitakapowaita wanangu Timothy na Gwantwa, au Timothy kama atazaliwa wa kiume pekee na Gwantwa endapo atazaliwa wa kike pekee, itakuwa faraja kwangu. Majina mengine yatakayotolewa na walezi wangu yatakuwa ni ya ziada tu kwa sababu sitayatumia kuwaandikisha watoto shuleni wala kanisani,” anasema kijana huyo ambaye yuko katika harakati za kuoa.

Wale tu tisa waliohojiwa na gazeti hili kuhusu majina waliyowapa au wanayotarajia kuwapa watoto wao wamesema, hayatokani na mila na desturi zao ni kutokana na sababu mbalimbali.

Wengi wanasema wametumia vitabu vya dini kuiga majina ya watu maarufu kutoka pande tofauti duniani, pamoja na majina yanayotokana na matukio yanayoambatana au yaliyotokea kabla, mara tu na wakati watoto wao wakizaliwa, na wala si ya kurithi kutoka kwa wazee wao.

Fundi viatu, Chande Chande wa Posta Mpya, Dar es Salaam, anazungumzia jinsi kaka yake alivyofikia uamuzi wa kumpa mtoto wake wa kike jina la Siamini. Anasema hakufuata utamaduni uliozoeleka kwao kwamba mtoto akizaliwa wa kike anapewa jina la mama wa baba wa mtoto na akizaliwa wa kike, anapewa jina la mama wa baba wa mtoto.

Anasema, kutokana na tatizo la kuharibika mimba pamoja na kufariki watoto wakiwa na umri wa mwaka mmoja au karibia miaka miwili, wazazi wa mtoto aliyebarikiwa kuishi hadi leo waliamua kumwita jina hilo Siamini kuonesha kwamba ni miujiza ya Mungu tu ndio iliyomfanya aishi hadi kufikia kuwatia moyo wazazi wake ambao awali hakuwamini kama naye ataishi.

“Kaka yangu na mkewe walifikiria kuhusu yaliyokuwa yakitokea na kushindwa kuamini kwamba ilifika miaka miwili mtoto akiwa hai, hivyo, waliamua kuishirikisha familia kuhusu jina na kufikia mwafaka kuwa mtoto aitwe jina hilo,” anasema fundi viatu huyo.

Sleyum Myala ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Kurasini, Dar es Salaam, anasema hategemei kuwapa watoto wake majina ya kurithi kwa wazazi wake kwa sabbu ya hofu kuwa huenda wakarithi tabia au mienendo ya wazazi hao.

Anasema, “Baba yangu ni mtu wa Iringa anaitwa Muvemba au Paschal Myala na mama yangu ni wa Kondoa, anaitwa Kisome au Rehema. Hadi nimekuwa mtu mzima, sijashuhudia wakifanya matukio ya ajabu au kusikia kwa watu wakiwazungumza kuwa wamefanya mambo mabaya, lakini sifikirii kuwapa watoto wangu majina yao kutokana na imani kwamba kama kuna mabaya yoyote yaliyojificha ndani yao, wanangu wanaweza kuyarithi.”

Mwingine niliyehojiana naye kuhusu hoja hii ni mkusanya madeni wa Kampuni inayochapisha gazeti hili, Tanzania Standard News papers (TSN), Omary Mbonde anayesema amekwishamaliza masuala ya uzazi kwa sasa na hakuna mtoto hata mmoja aliyempa jina la kurithi kutoka kwa wazazi wake.

“Nimeoa na nina watoto wanne.Kati yao, mmoja wa mwisho ni wa kike anayeitwa Zawadi. Sikufikiria kumpa mtoto wangu yeyote jina la wazazi wangu kwa kuwa nilitaka kwenda na wakati na niliamini kuwa kuwapa watoto majina yaliyo katika vitabu vya dini ni kuwapa baraka,” anasema Mbonde.

Anasema alipokuwa mdogo alipewa jina la Mwendapole kutokana na tabia yake ya kutembea polepole na kurejea nyumbani baada ya wenzake wote.

“Mwendo wangu wa taratibu uliwafanya wazazi wanipe jina la Mwendapole lililo maarufu zaidi nyumbani hapa Dar es Salaam na hasa kijijini nilipozaliwa. Kazini watu hawalifahamu kwa sababu ninatumia jina langu halisi, ambalo hata hivyo, halikutokana na kurithi kwa babu wala ndugu yake mwingine,” anasema.

Mbonde anasema, haoni umuhimu wa kurithisha watoto majina kwa sababu mengine huwafanya wanaoyarithi wawe na tabia za waliowapa majina hayo, hivyo kuwa athiri, endapo wanakuwa na tabia mbaya.

Akielezea jinsi jina la mwanawe wa mwisho lilivyopatikana, Mbonde anasema: “Jina lake lilitolewa na mke wangu siku alipojifungua. Mke wangu aliniambia kuwa mtoto huyo ni zawadi yangu kwa kuwa hayuko tayari kubeba ujauzito tena kutokana na kuchoka kufanyiwa upasuaji. Jina lilizoeleka na kukubalika hadi leo.”

Marietha Joseph anayejitambulisha kama mwalimu wa shule ya sekondari anasema yeye na mumewe hawakuona sababu ya kuwapa watoto wao majina ya kurithi, bali ya wanamuziki maarufu wanaowavutia.

Anasema wana watoto watatu; wawili ni wa kiume na mmoja wa kike na kwamba, uamuzi kuhusu majina ya watoto ambao waliamini Mungu angewajalia baada ya kufunga ndoa waliufikia siku moja walipokuwa wakiangalia video ya muziki mchanganyiko wa wanamuziki wa Ulaya.

“Nilivutiwa na sauti ya Whitney Houston na mume wangu alimpenda zaidi Lionel Richie, kwa hiyo tukajikuta tukifikia muafaka kwamba endapo tutapata watoto basi majina yao yatafanana na ya wasanii hao.Kwa bahati nzuri tulimpata Whitney, Richie na Lionel”.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, hawakuwahi kufikiria majina ya wazazi wao na wala wazazi hao hawakuwahi kuhoji sababu za wajukuu kutokupewa majina yao kama ilivyozoeleka katika tamaduni za makabila mengi ya kitanzania.

Akijibu endapo wazazi wangetaka wawape watoto majina ya kurithi wangefanya nini, Joseph anajibu hakuna ambaye angekubali, kwa sababu wanaamini kurithi majina ni kurithi kila jambo baya la anayetoa jina. Wengine ni Natujwa Hosea anayefanya kazi katika duka la dawa Tegeta Dar es Salaam.

Yeye anasema ameolewa na ana watoto wawili, pacha wa kike na wa kiume, lakini hawakuwapa majina ya wazazi wao kwa sababu walihofia kuwa pengine wangekuwa walevi kama bibi na babu yao.

“Uamuzi wa kuwapa majina Carren na Calvin ulifikiwa na babu yao mzaa baba aliyetuomba tutafute majina tunayotaka ili wajukuu zake wasiwe walevi kama wao. Baba mkwe wangu amekuwa akisema kila wakati kuwa jina lake alilirithi kutoka kwa babu yake aliyekuwa mlevi ndio maana naye akawa mlevi aliyesababisha mke wake naye awe mlevi,” anasema.

Fundi magari, Likas Kennedy wa Sinza, Dar es Salaam anayemiliki gereji katika eneo la Tabata, nje kidogo ya jiji hilo anasema kwa sababu anapenda majina mazuri yanayoendana na wakati, hakusumbuka kuwapa watoto wake wawili majina ya kilugha ya wazazi wake, Nighenjijwe ambaye ni mama mzazi na Yonafika ambaye ni baba yake mzazi kwa sababu alitaka kuendana na wakati.

“Baba yangu hakujali aliposikia nimemwita mwanangu wa kiume jina Marcus kwa sababu hata langu alichukua la rafiki yake aliyemsaidia wakati akisoma sekondari huko Upareni. Lakini, alituomba mimi na mke wangu tumfikirie mama na kumpa mtoto wetu wa pili jina lake kwa sababu amekuwa akiomba sana azaliwe wajina wake. “Kwa kuwa sharti lilikubaliwa, mtoto aliyezaliwa aliitwa Merylin, ambalo ni jina la ubatizo na Nighenjijwe likiwa ni jina linaloitwa na watu wachache tu wa familia, akiwemo mama yangu mzazi, baba na ndugu wengine wa familia yangu,” Kennedy anasema.

Kwa upande wake, mzazi mwingine, Batholomew Rutahakamwa ambaye ni baba wa watoto wanne anasema, alitaka majina ya watoto wake wote yaanzie na herufi “S” kwa sababu ndiyo aliyoipenda zadi akiwa shuleni. “Kwa kuwa nimebahatika kupata watoto wawili wa kike na wawili wa kiume, nimewaita majina Samuel, Shirley, Shedrack na Stephanie, ambayo hayatoki katika upande wowote wa familia zetu, si kwa mke wangu wala kwetu,” Rutahakamwa anasema.

Anaweka wazi kuwa haelewi ni kwanini anaipenda herufi hiyo lakini, hata kama isingekuwa suala la herufi, asingewapa watoto wake majina ya wazazi wake au wa mkewe, kwa sababu ni ya kienyeji sana wakati wao wanataka kuendana na wakati kwa majina yanayoweza kutamkwa kirahisi.

Prosper Sabasy Shirima mwenye mtoto mmoja wa kike aitwaye Michelle anasema haamini katika kuwapa watoto majina ya bibi au babu zao kwa sababu mbalimbali, kubwa ikiwa kuepusha kuwarithisha tabia zisizo stahili kama vile uchawi, ulevi, wizi, umalaya, uongo na nyingine zisizo mpendeza Mungu.

Maelezo ya wataalamu Mtandao wa www.answers. com unaoandikwa na wataalamu wa mambo mbalimbali, wakiwmo wanasosholojia unasema kwamba dhana kuwa mtoto anapozaliwa anaweza kurithi tabia nzuri au mbaya ya wazazi wake au bibi na babu ni potofu kwa sababu, tabia hujengwa na mazingira yanayomzunguka wakiwmo watu anaoishi nao.

“Ikiwa mtoto anayezaliwa atalelewa katika mazingira ya wizi na akashuhudia kila wakati walezi au wazazi, ndugu na jamaa wanaomzunguka wakiiba, asipoelezwa kuwa wizi ni mbaya na haufai, mtoto huyo atakuwa akiiga vitendo hivyo vya wizi na kuwa mwizi,” unasema mtandao huo, www. answers.com inaeleza.

Ustaadhi mmoja aliyeongea kwa sharti la kutotaka jina lake litajwe gazetini, anasema mafundisho ya Uislamu yanamtaka mzazi kumpa mwanae jina zuri. Anafafanua kwamba si vyema kumpa mtoto jina linaloomba dua mbaya kwa Mungu kama vile Taabu, Mashaka ama majina ya watu ambayo jamii haiwapendi.

“Lakini inaposemwa majina mazuri, haimaanishi majina ya Kiarabu, bali hata ya kimila ambayo hayana maana mbaya kwa sababu Uislamu si jina bali matendo na imani ya mtu. Lakini kuwapa watoto majina ya mitume na watakatifu wengine inapendekezwa sana pia,” anasema ustaadh huyo.

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Namsembaeli Mduma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi