loader
Dstv Habarileo  Mobile
Utanzania wetu ni muungano wetu, serikali 3 zitaulinda?

Utanzania wetu ni muungano wetu, serikali 3 zitaulinda?

Ikumbukwe kuwa Ukawa walitoka bungeni baada ya kushindwa kuelewana na wajumbe wenzao kwa kile walichokisema kuwa ni mchezo mchafu wa CCM baada ya kutolewa mapendekezo ya serikali mbili badala ya tatu walizozitegemea na kupendelea.

Pamoja na msimamo wa Ukawa bado watanzania wameshuhudia vioja vya baadhi ya wabunge wa Ukawa hasa kutoka vyama vya Chadema na CUF waliokuwa wakitinga bungeni na kusaini kisha wanatoroka Bunge.

Katika uelewa wa kawaida tunaweza kufikiria mambo mawili la kwanza; kwamba aidha, wajumbe hawa walikuja kuchukua posho kutokana na uroho wao wa fedha au ugumu wa maisha na hivyo bungeni ndiko kimbilio pekee la kuweza kupata fedha ya kukidhi mahitaji yao au mtazamo wa pili unadhihirisha kwamba kuna baadhi ya wajumbe wa Ukawa hawapendi kinachoendelea ila wanafanya ile unayoitwa bendera fuata upepo, wakizolewa na udikteta wa vyama vyao.

Kimsingi hadi hapo watanzania wameamini kabisa kuwa Ukawa wenyewe kwa wenyewe wanatofautiana kimisimamo ila tu wanalazimika kufuata kile kinachoamuliwa na uongozi wao na kwakuwa hawataki kupoteza ubunge wao kwa kufutwa uanachama, wanaamua kupinga kimya huku ndani wakiumia sana.

Hata hivyo, hii siyo sehemu kuu ya mada yetu ya leo ila nimeitanguliza ili watanzania wazidi kuona kuwa kutoka kwa Ukawa bungeni siyo misimamo ya wabunge waliotoka ila wengi wao wanalazimika kufanya hivyo ili kulinda kitumbua chao walichopewa na watanzania mnamo mwaka 2010.

Terejee kwenye mjadala wetu wa leo, jamani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa wa lazima kama Ukawa wanavyosema, wala haukuwa wa kilaghai kama wanavyodhani, na wala haukufanywa na viongozi wawili tu bali wao walikuwa ni waasisi na kutokana na dhamana ya uongozi waliokuwa nao kipindi hicho ilibidi wasimamie suala hilo.

Hata hivyo, zipo sababu kadha wa kadha zilizopelekea muungano huo uanzishwe: kwanza kuwepo kwa uhusiano wa karibu kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu (ambalo ni la msingi kabisa), biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya chama cha Tanganyika Africa National Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP). Lakini pili ni ule ya Moyo wa kuwa na Muungano wa Afrika hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki.

Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania utaifa katika ukanda wa Afrika Mashariki na hatimaye Afrika kwa ujumla walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Kinyume na matarajio walitangulia mbele ya haki kabla hata ya kutimiza matarajio yao.

Watanzia inabidi tutambue kwamba kinachotufanya tusimame na kufanya hata kile kidogo kinachobezwa ni kwa sababu ya umoja na udugu wetu uliopo. Kama tukiupoteza tutambue kabisa kwamba tunatengeneza dhambi ambayo haitokaa ikaisha hata siku moja.

Nadhani kuna jambo Ukawa hawalijui, kwenye familia siku zote mnaunganishwa na ile dhana ya ni “ndugu yangu” huku mkitupilia mbali tofauti zenu, lakini pindi kukitokea hali ya yule siyo ndugu yangu kwa mama au kwa baba lazima kutatokea kutokuelewana baina ya wanandugu hao na mara nyingi tumeshuhudia familia za aina hii zikiishia kuuana na hata kupelekana mahakamani na zaidi ya yote ni kujengeana uhasama wa milele.

Kuzaliwa jina Tanzania lilituonyesha kwamba sote ni ndugu wamoja na hakuna umama wa kambo wala baba wa kambo! Mara zote huwa najiuliza swali hili hivi ni kwanini tunapenda kudumisha mipaka na miungano ya kikoloni kuliko ya kwetu sisi wenyewe? Au ndo tumelewa ukoloni kwa kila jambo?

Mnamo mwaka 1995 mwalimu Nyerere aliwahi kuyanena haya wakati akihutubia hasa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, namnukuu “Watu wamezungumza Uzanzibari, baadhi ni viongozi wetu wanajivunia Uzanzibari. Nadhani wengine wanafikiria hata kujitenga, sio wengi, lakini wapo.

“Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi, kusiwe na nchi moja bali mbili. Hili ni jambo linazungumzwa. “Tunataka viongozi, wanaoelewa hilo. Kuzungumza Uzanzibari si jambo la fahari. Hatima yake utavunja nchi. Mtu mwenye akili, Mzanzibari ana akili hawezi akautukuza Uzanzibari wa kujiita sisi Wazanzibari na wao Watanganyika. Na adhani ile ina usalama ndani yake. Kufanya hivyo, hatima yake Zanzibar itajitenga.

“Zanzibar ikijitenga, kutokana na ulevi tu… Sisi Wazanzibari wao Watanganyika…sisi si wamoja. Ulevi tu… ulevi hasa ulevi wa madaraka. “Ikitokea hivyo, sisi Wazanzibari wao Watangayika. Wakumbuke kwamba muungano ndio unaowafanya waseme sisi Wazanzibari wao Watanganyika.

“Nje ya muungano hawawezi kusema hivyo, nje ya muungano hakuna Wazanzibari. Nje ya muungano kuna wao Wapemba sisi Waunguja. Nataka mjue hivyo… (kimsingi hili limekwisha anza kujitokeza kwani muda mfupi uliopita wapemba wameulizia hati ya muungano kati yao na waunguja) “Nje ya muungano hakuna sisi Wazanzibari wao Watanganyika. Hakuna… hakuna. Kinachowafanya sasa wajiite sisi ni ubaguzi wa kuwabagua Watanganyika. “Wakishakuwabagua Watanganyika, ile dhambi ya ubaguzi haifi, inaendelea. Dhambi ya ubaguzi ukisha kuitenda inaendelea, ni sawa na kula nyama ya mtu, ukila nyama ya mtu utaendelea tu.

Mtamaliza, mtatengana na Watanganyika halafu mara mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari… Kuna Wapemba na kuna Waunguja. ”Wapemba watapata msukosuko kidogo au aaah. Mtakuta kumbe kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama… hamtakaa salama.

“Hamuwezi kukaa salama baada ya kutenda dhambi ya kubagua watu wa nchi yenu ile ile moja, mkawaita wale wao na hawa sisi. Dhambi ile haishii hapo, ndiyo historia ilivyo, ni sheria ya historia sio sheria ya Mwalimu Nyerere.” Kimsingi mambo haya tunayasikia yakisemwa na tunaona kwamba labda sisi ni tofauti hivyo tunajidanganya kwamba hayawezi kutukuta lakini ukweli ni kwamba hii hali itatukuta tu iwapo tutaruhusu serikali tatu!

Jamani vitu vingine viko wazi kwamba kinachoifanya dunia isitawalike ni kwa sababu ya kila dola kuwa na mfumo wake tofauti wa kitawala suala hili tukiliruhusu Tanzania tutegemee ya kututukuta. Iangalie Sudani Kusini na Kaskazini! Wao pia walianza na vugu vugu kama hili la sisi ni Wasudani Kusini wao ni wa Kaskazini na mwisho wa siku yamewakuta yaliyowakuta na bado damu zinaendelea kumwagika.

Wale waliojiuona wa Sudan Kusini walikuja kugundua kwamba kumbe bado si wamoja. Wanasiasa wasiwadanganye watanzania kwa sababu ya uroho wa madaraka, ukweli ni kwamba ubaguzi ukianza hauishi hata siku moja! Tume ya katiba ilikuwa wazi kwenye mojawapo ya hasara za utawala wa serikali tatu kwamba muundo huu unaweza kuhatarisha muungano wetu na hivyo kupelekea kuuvunja! Sasa ukawa hili ndilo wanalo litaka?

Ningefurahi sana kama wangesema tumechoka serikali mbili sasa tunataka serikali moja, lakini mbadala wake wanapiga hatua kurudi nyuma badala ya kwenda mbele alafu wanatumia kivuli cha watanzania wote ili hali ukweli wanautambua ndani ya mioyo yao. Hivi watanzania tujiulize tukiendeleza hii vita ya kujitenga ni lini Afrika itaungana? Ni lini Afrika itakuwa na sauti moj? Hivi waasisi wetu wa Afrika tunawaenzi vipi? Mimi ninavyoamini chako ni chako tu hata kama kikoje utakipenda tu.

Ni nani anaweza kumuacha mkewe eti kisa wapishana maneno au ukiletewa umbea wa kwamba nimemkuta mke wako kasimama na fulani utamuacha? Kubali tusikubali, serikali tatu zikianza hata ukawa hawatakuwa pamoja, maana ubaguzi wa kikabila utaanza na ikifika wakati huo ni nani atasimama?

Haya tumeisha anza kuyaona, suala la wabunge wa CUF na CHADEMA kutinga bungeni mbali ya itikadi zao inaonyesha ni kwa kiasi gani umoja huo unaendeshwa kwa udikteta hasa pale baada ya mwanasheria wa CHADEMA kutamka wazi kwamba wale wabunge waliofuata mapenzi ya mioyo na nchi yao na hivyo kuamua kurejea bungeni wachukuliwa hatua; hivi kwanini wafanyiwe hivyo?

Kwani ile katiba ni ya ukawa au ya watanzania? Au tumesahau tunafikiri ni ya vyama vya siasa? Wakati sudani kusini wanataka kujitenga hawakulitambua suala la ukabila lakini baada ya kujitenga suala hilo likaibuka sasa hawajui watulize vita ipi ya ukabila au ya kisiasa?

Tutambue kabisa kwamba umoja ni nguvu na utengano siku zote ni udhaifu, kwa hiyo watanzania tusiruhusu kujitenga bali tudumishe udugu wetu kama zilivyo nchi zilizoungana na kudumu ikiwemo Marekani.

Makala haya yameandaliwa, mwanafunzi wa chuo kikuu huria cha Tanzania anayepatikana kwa +255 712 246 001, flugeiyamu@ gmail.com

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Felix Lugeiyamu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi