loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utekelezwaji wa mtaala elimu ya awali Iramba wasuasua

Vitabu vya kiada vitakavyotumika ni vile vitakavyokuwa na ithibati, uchaguzi wa vifaa na zana utazingatia makundi ya watoto wakiwemo wenye mahitaji maalumu kama wasioona vizuri, wenye ulemavu wa akili, viziwi, wanaojifunza polepole na wenye vipaji maalumu.

Pia katika shule za msingi mtaala unaeleza kuwa kutakuwa na madarasa ya elimu ya awali kama sehemu ya shule kimuundo, itajumuisha shule za msingi zilizoanzishwa na watu binafsi, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, mashirika ya dini, mashirika ya umma na mamlaka mbalimbali.

Miundombinu ya shule kwa madarasa ya elimu ya awali itakuwa ni ile inayomjali mtoto kwa kuzingatia umri na utimamu wa maumbile. Ukubwa wa madarasa utakuwa ni mita 6.0 kwa mita 8.0 (wastani wa mita za ukubwa 1.9 kwa mtoto mmoja). Licha ya mtaala wa elimu ya awali kubainisha wazi kuhusu utaratibu unaotakiwa katika madarasa ya awali, hali imekuwa tofauti katika shule mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mapungufu mbalimbali.

Katika utafiti uliofanywa hivi karibuni kuhusu uwekezaji katika elimu ya awali pamoja na hali halisi ilivyo kwa wilaya ya Iramba, mkoani Singida ulibaini wanafunzi 44 wa darasa la awali katika shule ya msingi Lulumba, wanakabiliwa na tatizo la kukosa darasa ambapo hujikuta wakipata elimu yao wakiwa chini ya mti huku baridi na upepo vikiwakabili.

Wanafunzi hao ni wale wa awali moja ambao wana miaka mitano huku wale walio na miaka sita idadi yao ikiwa ni 44 wakitumia jengo la ufundi lililopo shuleni hapo. Akizungumzia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jacob Izack anasema uanzishwaji wa madarasa ya awali katika shule za msingi haukuwa na maandalizi ya kutosha, jambo linalosababisha kuwepo kwa changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi kwa wakati.

Kwa kuzingatia hilo, hata walimu wanaofundisha madarasa hayo ni wale wasiokuwa na mafunzo ya stadi maalum za madarasa ya awali ambapo huwalazimu kutumia walimu wa kawaida. Kuna uhaba mkubwa wa madarasa na hata madawati shuleni hapo, kwani huwalazimu watoto hao ambao bado ni wadogo kukaa chini asubuhi wakati wakipatiwa elimu jambo ambalo linaweza kuathiri maendeleo yao.

Mwalimu wa darasa la awali mbili (wale wenye miaka sita), Lucy Ngollo anasema vihesabio kwa wanafunzi wa shule hiyo imekuwa ni tatizo ambapo huwalazimu kutumia vijiti vilivyounganishwa na kamba, visoda na hata mabua ili kuwawezesha wanafunzi kuelewa wanachofundishwa na walimu wao.. Mbinu ya kuwafundisha watoto hao ni shirikishi ambapo darasa la awali moja (wale wenye miaka mitano) hawana darasa hukusanyika nje chini ya mti na kuwekewa ubao chini kwa ajili ya maelekezo zaidi.

Anabainisha kuwa wakati mwingine hutumia sakafu iliyojengwa shuleni hapo kama sehemu ya bwalo la kulia chakula ambapo ni eneo la wazi pia. Mbali na changamoto ya kukosa madarasa pia, shule inakabiliwa na changamoto ya kukosa vitabu vya haiba na michezo kwa watoto hao wa madarasa ya awali huku, vyoo wakiendelea kutumia vya wenzao jambo ambalo ni hatari kiafya kwa wanafunzi hao ambao bado ni wadogo kiumri.

Aidha, tatizo la wanafunzi wa darasa la awali kukosa vihesabio na kutumia mabua, vijiti na visoda linawakumba pia wanafunzi wa shule za Tutu, Kisiriri na Kizega. Upungufu huo wa vifaa vya kufundishia na kuhesabia pamoja na vitabu kwa watoto wanaosoma darasa la awali imewalazimu wanafunzi hao kutumia mabua, visoda na vijiti kwa ajili ya kuhesabia.

Aidha, kutokana na hali hiyo, walimu wakuu wa shule mbalimbali za msingi wilayani humo wanaiomba serikali kutoa ruzuku kwa watoto wa darasa la awali kwani huduma zao haziwezi kutenganishwa na madarasa mengine. Akizungumzia hali hiyo, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kizega, Elizante Gyuzi anasema licha ya shule yake kupata vifaa vingine lakini anailaumu serikali kutokuwa tayari kuithamini elimu hiyo ya awlai kw akuiwekea misingi thabiti.

Anasema kulingana na sera ya elimu ni lazima madarasa ya awali kuwa maalumu, kuwa na vyoo kwa ajili yaw a watoto hao, madarasa yanayojitegemea kwa wahusika ni watoto wadogo wenye uangalizi maalumu.

“Kwa mfano hapa shuleni kwangu lipo darasa ambalo lilikarabatiwa na wahisani na pia kutupatia vifaa mbalimbali ambapo imepunguza ile hali ya watoto kubeba vijiti ama mabua kwa ajili ya kuhesabia,” anasema Gyuzi ambaye shule yake ni maalum kutokana na kuwa na wanafunzi wenye mahitaji muhimu. “Ninawashukuru wakazi wa eneo hili ambao kwa nguvu moja wameemilishwa na kufahamu umuhimu wa elimu ambapo katika kuonesha jitihada zao wanafyatua tofali ili kujenga darasa la watoto wa awali,” alisema Gyuzi.

Kuhusu ruzuku kwa madarasa ya awali anasema kama kweli inahitaji kuyaona madarasa ya awali ni vyema kusimamia kwa vitendo hata kwa kuhakikisha inatoa ruzuku kwa watoto hao kama ilivyo kwa wengine. Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tutu, Rebecca Pyuza anasema vifaa vya kuhesabia shuleni hapo kwa ajili ya watoto ni vichache ambapo mwalimu anayewafundisha watoto hao hutumia mbinu ya kuwataka vijiti na kuvibeba katika mifuko yao.

Anasema elimu ya awali shuleni hapo ni changamoto kubwa kwani hata mwalimu anayefundisha watoto hao ni wa kujitolea ambaye awali alikuwa mwalimu lakini baadae alipumzishwa ambapo shule imeamua kumtumia.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi, Kisiriri Gerson Mkoma anasema shuleni hapo watoto wa awali hutumia visoda, mabua na vijiti kwa ajili ya kuhesabia huku michoro mingine wakisaidiwa na walimu wao. Anasema shule hiyo haijawahi kuwa na vifaa maalum kwa ajili ya mafunzo shuleni hapo na kuiomba serikali kuzikumbuka haswa shule ambazo ziko pembezo ama vijijini zaidi.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi