loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utoro sugu wachangia kudidimiza elimu Rukwa

Mbali na matokeo mabaya, kumekuwa pia na tatizo kubwa la utoro ambapo mamia ya watoto hushindwa kuhitimu elimu ya msingi ama ya sekondari kila mwaka.

Taswira hiyo si tu inawatia hofu kubwa wadau wa elimu mkoani humo bali pia inaufanya Mkoa wa Rukwa kuonekana ni miongoni mwa mikoa yenye mwamko mdogo wa elimu kutokana na kila mwaka kuzalisha watoto lukuki waliofeli darasa la saba.

Katika Wilaya ya Nkasi, kikao cha ushauri cha ya wilaya (DDC) kilichofanyika Septemba mwaka jana mjini Namanyere ambapo mwandishi wa makala haya alipata furasa ya kuhudhuria, wadau wa elimu wilayani humo walisema hali hii ni fedheha na janga kubwa, si kwa wilaya na mkoa pekee, bali kwa taifa zima pia.

Walisema kila mshirika wa elimu; serikali, waalimu, wazazi na wanafunzi wanatakiwa kubadilika na kusimama imara ili kuokoa elimu mkoani Rukwa. Wadau hao walikemea zaidi utoro sugu shuleni, jambo ambalo kimsingi liko katika uwezo wa wazazi na waalimu.

Walionyooshewa kidole zaidi ni wazazi, hususan wale wanaoruhusu watoto wao kushiriki katika ajira. Wadau hao walilazimika kueleza masikitiko yao kuhusu kuanguka kwa elimu mkoani Rukwa kufuatia taarifa ya elimu wilayani humo iliyowasilishwa na Ofisa Elimu (Taaluma) wa Wilaya, Linno Mwageni.

Katika taarifa yake, Mwageni alisema kwamba ni watoto 907 tu miongoni mwa 2,277 waliojiunga na Kidato cha Kwanza miaka minne iliyopita ndio waliofanikiwa kuhitimu kidato cha nne mwaka juzi.

Taarifa hiyo inaonesha kuwa katika suala la utoro hali ni mbaya pia kwa upande wa shule za msingi wilayani humo ambapo kati ya watoto 9,910 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2007 ni watoto 3,772 ndio waliofanya mtihani wao wa kumaliza elimu ya msingi mwaka juzi.

Ilielezwa kwamba miongoni mwa sababu za utoro shuleni, jambo ambalo ndilo tatizo kubwa zaidi ni watoto kujiingiza katika ajira ikiwemo uvuvi, kutumikishwa mashambani na kuchunga ng’ombe.

"Kuna wazazi na walezi ambao huridhia watoto wao kufanya vibarua bila kuangalia madhara ya watoto kukosa elimu," anasema Basilio Mbwilo, Diwani wa Kata ya Kipili, mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani humo.

Hali ya utoro pia huzikumbuka wilaya za Sumbawanga na wilaya mpya ya Kalambo ambapo Mkuu wa Wilaya Sumbawanga, Moshi Chang’a, alibainisha kuwa mwaka jana zaidi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari wapatao 5,585, (watoto 2,484 kutoka Wilaya ya Kalambo na 3,111 wa Wilaya ya Sumbawanga) walikatisha masomo kutokana na utoro.

Chang’a alifafanua kuwa wanafunzi hao kutoka wilaya hizo mbili wameacha masomo baada ya wazazi na walezi wao kuwaingiza katika ajira, hususan za kupalilia mashamba ya mahindi kama vibarua ambako wanalipwa ujira mdogo tu.

Mkoa wa Rukwa ni kati ya mikoa inayoongoza kwa kilimo cha mahindi nchini.

Pia taarifa ya matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2012 mkoani Rukwa inabainisha kuwa shule za msingi 48 katika mikoa ya Rukwa na Katavi (kabla ya mgawanyo rasmi wa sekta ya elimu) hazikuweza kufaulisha wanafunzi kabisa ingawa walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

“Shule hizo 48 ni miongoni mwa shule za msingi 502 zilizopo katika mikoa hiyo miwili zilizokuwa na wanafunzi 1,276 waliohitimu elimu ya msingi, lakini hakuna hata mmoja aliyefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi,” inabainisha sehemu ya taarifa hiyo.

Mikoa ya Rukwa na Katavi ina shule za msingi 502 ambapo wanafunzi 25,698 walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana lakini ni 6,382 tu waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shule za msingi 11 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ndizo ambazo hazikuweza kufaulisha wanafunzi wapatao 244 waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi huku shule za msingi tatu zilizokuwa na jumla ya wanafunzi 135 katika Manispaa ya Sumbawanga nazo zikiambulia sufuri.

Taarifa inasema shule 22 zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga zenye idadi ya wanafunzi 692 pia hazikufaulisha mwanafunzi hata mmoja.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa Baraza la Mitihani liliwafutia matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wanafunzi 15, wakiwemo wasichana 10 na wavulana watano kutoka Shule ya Msingi Kilesha iliyopo katika Halmashauri ya Sumbawanga kutokana na kubaini udanganyifu.

“Awali Baraza la Mitihani lilikuwa limezuia matokeo ya wanafunzi wote 18 kutoka Shule ya Msingi Kilesha lakini baada ya taarifa ya uchunguzi kuwasilishwa katika baraza hilo matokeo ya wanafunzi watatu yalikubaliwa,” inafafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Kushuka kwa elimu na matokeo mabaya ya kumaliza elimu ya msingi mkoani Rukwa bado hali ni ile ile ya miaka ya nyuma ambapo ufaulu umekuwa ni wastani wa asilimia 40 huku kukiwa idadi kubwa ya watoto 885 walioshindwa kuhitimu elimu ya msingi kwa sababu ya utoro.

Akisoma matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwishoni mwa mwaka jana, katika kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Rukwa, Steven Mgina alisema ni watoto 6,878 tu walifaulu kati ya watoto 17,109 waliofanya mtihani huo Septemba mwaka jana na kwamba ufaulu huo ni sawa na asilimia 40.

Mgina alisema watoto 885 walioandikishwa darasa la kwanza katika shule mbalimbali za msingi mkoani Rukwa miaka saba iliyokuwa imepita walishindwa kufanya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi, Septemba mwaka jana kutokana na utoro au mimba.

Mgina alizitaja shule kumi bora zilizofanya vizuri kuwa ni pamoja na Shule ya Msingi Mvimwa (Nkasi), Hill Crest Junior Academic, Ufipa English Medium, Mbwendi, St Mathias English Medium (Manispaa), Namanyere, Ntatumbila, Isunta (Nkasi ) Laela 'A' na Shule ya Msingi Laela 'B' (Sumbawanga).

Shule kumi zilizofanya vibaya mwaka jana mkoani Rukwa ni pamoja na Madibira, Kapere, Kachele, Tunyi, Mpanga, Mwaya, Ntumbi, Sikaungu, Kasamvu pamoja na Shule ya Msingi Mombo.

“WANAOFANYA shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi