loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uunganishaji umeme waelezwa kero kwa wateja wapya jijini Mwanza

Hiyo ni kauli ya mkazi wa jijini Mwanza, ambaye anaelezea adha anayoipata anapokwenda kuomba aunganishiwe umeme kwenye nyumba yake na Tanesco, ambayo anasema ameijenga kwa muda mrefu hadi anaelekea kustaafu hajaunganishiwa umeme kutokana na urasimu na gharama.

George William mkazi wa Mahina naye anasema ilibidi achangie gharama ya kuunganishiwa umeme na jirani yake, ambapo jumla walichanga kiasi cha Shilingi 700,000 ndipo alipoweza kuunganishiwa umeme lakini kwa kuchelewa sana!

Lwige Masanja mkazi wa Buswelu ambaye tayari nyumba yake imekwishakamilika anasema hajui ni lini ataweza kuunganishiwa umeme katika nyumba yake, hasa baada ya kumuona jirani yake akihangaika kuunganishiwa umeme.

Mary Maiko ( Sio jina lake halisi) mkazi wa Igoma ambaye ni mjasiriamali ambaye anatamani kupata huduma ya umeme naye anadai yuko njia panda. “Mwandishi shangazi yangu amejenga nyumba imekamilika lakini kila akienda Tanesco kuomba umeme anaambiwa njoo kesho, njoo kesho imekuwa njoo kesho, sijui kwa vile wanaona hana uwezo,” anaeleza.

Mwikwabe Chacha yeye anasema hana hamu na Tanesco, kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia aunganishiwe umeme nyumbani kwake ikiwa ni miaka miwili sasa. Hiyo ndiyo hali halisi ya uunganishaji wa umeme inayotolewa na Shirika la Umeme nchini, hali hiyo inawapata wakazi wa jijini Mwanza achilia mbali mikoa mingine, miji na majiji mengine.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya jijini Mwanza, kuhusiana na huduma ya usambazaji umeme kwa wateja, ipo minong’ono ya uombaji rushwa ambayo haijathibitishwa na gazeti hili ili mteja aweze kuharakishiwa umeme.

Lakini wakati ikiwepo minong’ono hiyo, utaratibu unaotolewa na Tanesco juu ya makadirio ya gharama za kuunganisha umeme kwa mteja, ikiwa mteja ameishajaza fomu ya kuomba huduma hiyo na kuwasilisha viambatanisho vyote muhimu.

Viambatanisho hivyo ni pamoja na picha yake na mchoro utakaoonesha nyaya zilivyosambazwa kwenye jengo au nyumba uliosainiwa na kupigwa mhuri na mkandarasi wa umeme aliyesajiliwa, mteja aliyeomba huduma ya kuunganishiwa umeme atapewa muda wa siku saba iwapo miundombinu iliyopo inaweza kutumika ndani ya mita 30 kutoka kwenye nguzo iliyo karibu.

Na ndani ya siku kumi za kazi kama ujenzi wa njia ya umeme unaohitajika ambao sio zaidi ya mita 100 kutoka kwenye nguzo iliyo karibu na kama mfumo mpya wa usambazaji unahitajika kujengwa, au kama uunganishi wa mfumo unatakiwa kwa wateja wenye viwanda au biashara kubwa, makadirio sharti yatolewe ndani ya siku 14 za kazi.

Ulipiaji wa gharama za kuunganishiwa umeme kwa awamu, hufanywa baada ya mteja kupewa makadirio ya gharama, ambapo mteja anayetaka kulipia gharama za kuunganisha umeme kwa awamu ataomba kwa kuingia mkataba na Tanesco kwa kulipia gharama hizo kwa awamu.

Tanesco wao wataruhusu awamu za malipo zisizozidi tatu kwa miezi mitatu mfululizo na ndani ya siku 60 za kazi, kama ujenzi wa njia ya nyongeza unahitajika ( njia hiyo ni kama mteja yuko kati ya mita 30 na mita 100 kutoka kwenye nguzo iliyo karibu) kama mfumo mpya wa usambazaji unahitajika kujengwa au unahitajika kuongezwa kwa ajili ya kiwanda au biashara kubwa, muda wa kumuunganishia mteja sharti uwe ndani ya siku 90 za kazi.

Na fedha zilizolipwa na mteja kwa Tanesco na kuendelea kuwa mikononi mwake, kwa zaidi ya siku 90 za kazi, huzaa riba ya asilimia 0.5 ya kiasi alicholipia mteja kila siku lakini kisizidi asilimia 50 ya gharama. Na ikiwa Tanesco itashindwa kumuunganishia mteja umeme kwa muda uliotakiwa, Tanesco itawajibika kumtaarifu mteja mapema kuhusiana na hali hiyo, na mteja sharti afahamishwe ni lini ataunganishiwa umeme.

Huo ndio utaratibu unaotakiwa ufuatwe na watumishi wa Tanesco, lakini kuna manung’uniko ya watumiaji wa umeme hali inayoashiria huenda utaratibu unawezwa kukiukwa. Haiingii akilini kuona Shirika la Tanesco linalotoa huduma ya umeme kama bidhaa zake, huku likiwa na uhitaji mkubwa wa wateja, linakabiliwa na changamoto ya usambazaji wa huduma hiyo kwa wakati!

Kwa dunia ya sasa ya Sayansi na Teknolojia, lazima urasimu wa aina hii uondoke. Na kama Tanesco inashindwa katika hili, ni vyema itungwe sheria ya kuruhusu mashirika mengine yaje kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuleta ufanisi na tija. Haiwezekani Shirika lisuesue kufanya biashara ili lijiongezee kipato na liweze kujiendesha kwa ufanisi zaidi! Linatakiwa ndilo lichangamkie wateja na sio wateja wapige “mark time”, kwenda katika ofisi zao.

Akiwa katika moja ya ziara zake jijini Mwanza, Rais Jakaya Kikwete alipewa taarifa na uongozi wa PPF jijini Mwanza ya kucheleweshewa kuunganishiwa umeme kwenye nyumba 1500 katika eneo la Kiseke zilizojengwa na PPF ili PPF waweze kuuza nyumba hizo kwa wateja.

Rais Kikwete aliwashangaa Tanesco kuona ni jinsi gani ambavyo sio wabunifu katika kufanya biashara. Rais alisema na hapa namnukuu, “Nyie mnasubiri kupewa chakula kwenye sahani, kazi yenu ni nini? Hebu changamkieni zile nyumba mpeleke umeme pale, zile tayari ni fedha,” alisema Rais Kikwete kwa wakati huo.

Nilidhani kwa wakati ule kauli ya Rais Jakaya Kikwete iliawaamusha Tanesco, kumbe bado ndio kwanza wametulia! Kinacholeta shida zaidi ni wakati wa usambazaji wa nguzo. Msiko Omera mkazi wa Buswelu anasema kununua nguzo tatu za umeme hugharimu kiasi cha zaidi ya Sh milioni moja, ambapo anasema mwananchi wa kawaida anayehitaji kuunganishiwa umeme hawezi.

“Kuna baba mmoja tunaishi jirani naye, yeye alitaka aunganishiwe umeme kwa gharama yoyote ili mradi apate, lakini alipigiwa mahesabu zaidi ya milioni moja, gharama zote zilihusisha hadi kuunganishiwa nyaya za umeme( wiring), lakini hadi anafariki nyumba yake haikuwahi kuwekewa umeme,” anaeleza.

Kutungwa kwa sheria mpya ya kuruhusu wawekezaji wengine kuja kuwekeza katika sekta ya nishati kwa mazingira ya sasa kunastahili! Hasa wakati huu ambapo Serikali kupitia wakala wa usambazaji umeme vijijini (REA) inaendelea kusambaza umeme vijijini. Katika hili la kupeleka umeme vijijini nalo linaweza kukumbwa na dhana ya wenye uwezo wa kutoa chochote ndipo wapate huduma hiyo.

Kama wataruhusiwa wawekezaji wengine wa ndani au nje kuwekeza katika sekta ya umeme, ambayo ni maendeleo nadhani urasimu wa aina hii, ukiwemo wa akina Masanja, Mwikwabe na Mary kuchelewa kuunganishiwa umeme utakwisha! Taarifa zilizopo ni kwamba gharama ya kuunganisha umeme kwa wateja wapya, ada ya maombi ya kuunganishwa ni Sh 5,000, na gharama za uunganishaji umeme ni kama ilivyoainishwa hapa chini.

Kuunganisha umeme kwa mteja aliye umbali wa mita 30 katika njia moja na kwa mita ya LUKU kwa mteja wa wateja wa vijijini ni Sh 150,000 na kwa wateja wa mjini ni Sh 272,000. Gharama hizo ni tofauti kwa wateja wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambao wataunganishwa kwa gharama ya Sh 99,000 ambazo zilitakiwa kutumika hadi Juni 30 mwaka huu.

Na kwa mteja aliye umbali wa mita 30 kwa njia tatu na mita ya LUKU kwa wateja wa vijijini ni Sh 772,893.00 na kwa wale wa mijini ni Sh 772,893.00 na kwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni Sh 99,000. Kwa umbali wa mita 70-njia moja, nguzo moja kwa wateja wa vijijini Sh 286,220, mjini Sh 436,964 na kwa umbali wa mita 70 njia tatu, nguzo moja na mita ya LUKU kwa wateja wa vijijini na mijini ni Sh 1,058,801.

Na umbali wa mita 120-njia moja, nguzo mbili na mita ya luku kwa wateja wa vijijini ni Sh 385,300 na wa mjini ni Sh 590,398 na kwa umbali wa mita 120 kwa njia tatu, nguzo mbili na mita ya Luku kwa wateja wa vijijini na mijini ni Sh 1,389, 115 Na ili mteja aweze kuunganishiwa umeme kwa mtumiaji wa kawaida wa mjini (urban customer) gharama yake ni Sh 320,000, uunganishwaji wa umeme kwa urefu usiozidi mita 30 bila ya nguzo (pillar) ni Sh 177,000.

Kwa mtumiaji wa kijiji anayehitaji umeme wa njia moja na nguzo moja, gharama yake ni Sh 337,740 na mtumiaji wa mjini anayeunganishiwa umeme kupitia nguzo moja (through one by one pillar) gharama yake ni Sh 515,618 na mtumiaji wa kijiji aliyechukua njia moja na nguzo mbili gharama yake ni Sh 454,654 na wa mjini anayechukua njia moja na nguzo mbili naye atatozwa kiasi cha Sh 696,670.

Kinachohojiwa na wananchi hizo gharama za mamilioni zinatoka wapi? Baadhi yao wanasema Tanesco haiko tayari kufanya biashara na kutengeneza faida. Hali hiyo ya kutosambaza umeme kwa wakati alikutana nayo Rais Kikwete katika moja ya ziara yake nyingine katika Kata ya Buswelu wilayani Ilemela makao makuu ya Wilaya ya Ilemela, ambapo wananchi waliwasilisha kilio hicho kwake ili waweze kupatiwa huduma hiyo.

Kati ya wananchi 15 waliorodheshwa kupata huduma hiyo, takribani zaidi ya miaka minne sasa ni wachache tu walioweza kupatiwa huduma hiyo. Hii ina maana kuwa Tanesco hawajui kufanya biashara! Idadi ya watu wenye kiu ya kuunganishiwa umeme wana fedha ambazo zinastahili kuchukuliwa na shirika hilo, lakini hakuna wa kuzichangamkia.

Kwa mfumo huu ni dhahiri Tanesco wanataka kurudisha hali iliyokuwa katika Shirika la Simu nchini kwa wakati huo ambapo ilikuwa inamchukua mtu muda mrefu kupata huduma ya kupiga simu.

Hivi ni nani leo hii hakumbuki hali iliyokuwepo katika shirika hilo? Ingawa kwa sasa mashirika hayo yametenganishwa na yameboreshwa kutokana na kuwekeza, ilikuwa inamchukua takribani siku nzima mtu kupata laini ya simu kuongea na mtu aliyeko Dar es Salaam au Dodoma kwa mtu aliyekuwa Musoma.

Mimi na mama yangu mzazi ni miongoni mwa watu tuliopata adha hiyo pale tulipoenda Musoma mjini ili tuweze kuwasiliana kwa njia ya simu na baba ambaye kwa wakati huo, alikuwa anafanya kazi Dar es Salaam, lakini ilituchukua muda wa siku mbili.

Lakini mara baada ya Serikali kuruhusu mashirika mengine ya mawasiliano, leo hii hata TTCL wenyewe wamepunguza urasimu, huduma zao za usafirishaji wa vifurushi na nyingine nyingi zimeboreshwa licha ya kupata ushindani katika soko, kwanini Tanesco isibinafsishwe?

Ibinafsishwe ili iondokane na kile kinachoitwa kwa Kiingereza “monopoly” na kujiona wao ndio wenye haki pekee ya kusambaza huduma hiyo hapa nchini, hali inayopelekea kuwepo kwa urasimu usiokwisha! Aidha Tanesco inaweza kufanya kazi kisayansi zaidi, kwa kuwafungia wananchi nguzo na kuchaji gharama zake wakati wa malipo ili kuwezesha watu wengi zaidi kujiunga na huduma hiyo kutokana na urasimu uliopo.

Lakini kutokana na taarifa “Literatures” mbalimbali nilizozipitia zinazohusu mipango na mikakati kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na dira ya kuwa “ taasisi,” yenye ufanisi na inayojali tija ili kuhakikisha rasilimali za nishati na madini kuchangia maendeleo ya nchi ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi, bado mipango na mikakati hiyo ni ya kutia shaka.

Ofisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja wa Mkoa wa Mwanza, Flaviana Moshi anasema kuwa madai yalitolewa na baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza juu ya kuwepo kwa urasimu sio ya kweli. Kwa mujibu wake, Tanesco ni Shirika linalotoa huduma ya umeme na kwamba hoja ya urasimu wa ucheleweshaji wa nguzo lilikuwa ni tatizo la kitaifa kuanzia mwezi Januari mwaka 2013 kutokana na nguzo kukosekana.

“ Lakini kwa hivi sasa hakuna ucheleweshaji na tumekuwa tunazingatia kwa jinsi wateja wetu walivyokuja kulipa, na mteja anayekuja kulipia umeme mwezi wa kwanza, na mwingine wa pili na wa tatu, tunatoa kipaumbele kwa mteja wa kwanza.” Alisema na kwa wakati huo mkakati wa Shirika ulikuwa ni kuhakikisha nguzo itakayopatikana mteja atakayekuwa amelipia ndiyo huunganishiwa huduma ya umeme mara moja bila ya urasimu.

“Na nikuhakikishie hakuna mteja anayekaa miaka mitatu akiwa amekamilisha taratibu zote za malipo na apewe umeme, kwakweli niseme kwa hivi sasa tumejitahidi kuboresha huduma zetu,” anasema Moshi.

Kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2014/15, Tanzania yenye jumla ya wakazi milioni 45, ni asilimia 24 ya Watanzania waliounganishiwa umeme hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu kutoka asilimia 21 ya mwaka 2012/13 ikiwa ni sawa na jumla ya watu wazima milioni 15 tu!

Na kiwango cha uunganishwaji wa umeme nchini kimekuwa kinakua kwa asilimia 10 kila mwaka, huku idadi ya watu wanaofikiwa na huduma ya umeme hadi kipindi hicho ni asilimia 36 tu. Pamoja na kupitishwa kwa sera ya gesi asilia mwezi Oktoba mwaka 2013 na kukamilika kwa ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia ambayo imekumbwa na mikikimikiki ya kisiasa kwa mikoa ya Kusini, kutoka Mtwara hadi Lindi kwa asilimia 77.8.

Kukamilika kwa maandalizi ya ufungaji wa mitambo ya kusafisha gesi kwa zaidi ya asilimia 44 na kugunduliwa kwa gesi asilia inayofikia futi za ujazo trilioni 4.8 kwenye visima vilivyopo hapa nchini, lazima iwepo mipango ya kisayansi isiyo ya kisiasa ya kuhakikisha rasilimali hizo zinawafikia Watanzania wote milioni 45.

Nasema hivi kwa sababu kama taifa tumekuwa maarufu katika kupanga mipango na mikakati mizuri ya maendeleo na kuandika maandiko ya miradi lakini utekelezaji wake umekuwa sifuri.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam Juni 26 mwaka 2011, juu ya jitihada zilizokuwa zinafanywa na Serikali (TANESCO) za kukabiliana na mgawo wa umeme nchini, alisema kuwa mgawo wa umeme kwa wakati huo kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na upungufu wa maji katika mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme ya Mtera, Kidatu, Kihansi, Hale na Nyumba ya Mungu.

Aliongeza kuwa upungufu huo ulisababishwa na kiasi kidogo cha mvua kilichonyesha kwa mwaka huo, ambapo alikaririwa akisema kina cha maji cha bwawa la Mtera, ambalo ndilo bwawa mhimili kwa wakati huo kilifikia kiasi cha meta 690.87 juu ya usawa wa bahari, wakati kina cha juu cha maji yanapojaa hufikia meta 698.50.

“Tunapenda kuwakumbusha Watanzania kwamba upungufu huu wa maji katika mabwawa yetu umeathiri sana uwezo wetu wa kuzalisha umeme kwa sababu kwa sasa hivi asilimia 55 ya umeme wetu unatokana na maji, 34 gesi asilia na 11 mafuta,” alisema Ngeleja wakati huo.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Ngeleja alijigamba mbele ya wandishi wa habari kuwa, serikali ilibuni miradi minne ya uzalishaji wa umeme usiotegemea maji, lengo likiwa ni kuiondoa nchi kwenye utegemezi wa umeme unaotokana na maji na kuifanya nchi itegemee vyanzo vingine vya uhakika zaidi visivyoweza kuathiriwa na uhaba wa mvua.

Kwa mujibu wa Ngeleja, miradi hiyo minne iliyobuniwa na serikali iliyokusudia kuongeza cha umeme unoazalishwa kwenye gridi ya taifa (kwa wakati huo MW 645) kuwa ni mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira-Mbeya uliotegemewa kuzalisha MW 200, mradi wa gesi asilia wa Mnazi Bay uliotarajiwa kuzalisha MW 300 na kukamilika mwaka 2010.

Miradi mingine ni pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme (gesi asili) wa MW 100 ulionunuliwa na serikali kupitia TANESO na kufungwa ubungo ulioanza rasmi kazi mwaka 2008 na mradi mwingine ni mitambo ya kuzalisha umeme kutokana na gesi asili (MW 45) iliyonunuliwa na Serikali na kufungwa Tegeta jijini Dar es Salaam.

Lengo kwa mujibu wa Ngeleja, miradi yote hiyo ililenga kuongeza kwenye gridi ya taifa MW 645 kwa mwaka 2006 -2010, lakini juhudi hizo hazikuwezekana kwani ni MW 145 tu zilizoweza kuzalishwa katika kipindi hicho (Ubungo MW 100 na Tegeta MW 45).

Katika kukabiliana na hali hiyo, Ngeleja alisema Serikali ilianzisha mpango wa dharula, ambapo kupitia Kampuni ya Symbion ilipanga kuzalisha MW 112.5 na Tanesco pia iliingia mkataba na Kampuni ya Aggreko kwa lengo la kuzalisha MW 100 za mafuta ya dizeli ili kukabiliana na mgao wa umeme, lakini pamoja na mipango hiyo, bado kwa baadhi ya maeneo nchini kumeendelea kuwepo kwa mgao wa umeme.

Changamoto zingine ambazo zimeendelea kuikumba sekta ya nishati ni za kimfumo ambazo zinahitaji mabadiliko ya kisera. Kutokamilika kwa bajeti ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya utendaji wa kazi za wizara ni changamoto nyingine.

Licha ya serikali kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme na kufikia kuzalisha MW 1,583 ( maji- asilimia 35), gesi asilia -34 na mafuta asilimia 31 hadi kufikia mwezi April mwaka huu ikilinganishwa na MW 891 zilizozalishwa mwaka 2005, bado hali sio ya kuridhisha sana.

Kwa mfano changamoto ya kutokamilika kwa bajeti ni tatizo sugu. Kwa mfano katika bajeti ya mwaka 2013/14 ambapo licha ya kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Gridi ya Taifa kiliongezeka na kufikia GWh 5,997.41 ikilinganishwa na GWh 5,760 za mwaka 2012, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 4 na kufanya mahitaji ya umeme kwa mwaka 2013/14 kufikia wastani wa MW 898.72 ikilinganishwa na MW 851.35 kwa mwaka 2012/13 sawa na ongezeko la asilimia 6, bajeti ya wizara inayoidhinishwa imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka na hivyo kusababisha tija kushuka.

Kwa mfano hadi kufikia Mei 23 mwaka huu jumla ya Sh milioni 83 sawa na asilimia 75 ya fedha za matumizi ya kawaida zilipokelewa na Wizara kutoka hazina. Aidha jumla ya zaidi ya Sh 577 bilioni sawa na asilimia 49 ya bajeti yote ya maendeleo zilipokelewa.

Kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 431 ambazo ni fedha za ndani sawa na asilimia 58 ya fedha zilizotengwa na Sh bilioni 147 zilikuwa fedha za nje sawa na asilimia 34 ya fedha za nje zilizotengwa, hivyo katika kipindi hicho Wizara ilipokea jumla ya Sh bilioni 661 sawa na asilimia 51 ya bajeti yote iliyoidhinishwa kwa wizara kwa mwaka 2013/14.

Akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka 2014/15, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikaririwa akisema kuwa moja ya mikakati ya wizara yake ni kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maeneo ya vijijini na mijini kwa kuongeza wateja hasa wa vijijini.

Mkakati mwingine kwa mujibu wa Profesa Muhongo ni kuvutia uwekezaji katika sekta za nishati na madini na kupeleka umeme katika makao makuu ya wilaya ambazo hazijapatiwa umeme, kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kujenga uwezo wa usimamizi na ufuatiliaji kwa sekta za nishati na madini ili kukuza uchumi wa taifa na kuharakisha maendeleo.

Nichukue fursa kumshauri Profesa Muhongo ambaye ni msomi aliyebobea katika mambo ya nishati wafikirie kuwa na mawazo ya kubinafsisha Tanesco ili ifanye kazi kwa ufanisi ili mikakati aliyoiainisha katika bajeti yake iweze kutekelezwa. Ingawa juhudi yake kupitia REA ya kupeleka umeme vijijini imeanza kuzaa matunda.

Lakini kupeleka umeme vijijini hakutakuwa na maana endapo Serikali haitawaandaa vijana na nguvu kazi ya huko ili kuanza kutumia umeme huo katika kuzalisha na kukuza vipato vyao ili kuondokana na umasikini. Kwa mfumo huu ni dhahiri utekelezaji wa mambo ya msingi ni dhahiri yatakwama na ndio maana nashauri sekta nyeti tulizo nazo nchini kwa mazingira ya sasa zibinafsishwe kwa wawekezaji ili ziondokane na urasimu usiokuwa na tija.

Kwa mazingira ya sasa watu wanataka huduma ya haraka na sio urasimu usio na msingi ndio maana nashauri sekta ya nishati nayo hasa TANESCO libinafsishwe ili liweze kutoa huduma ya usambazaji wa umeme kwa wakati!

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimembariki Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi