loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uvumilivu wa kiimani kielelezo cha tunu ya amani, maendeleo

Bila hiana, walipokelewa na wakoloni wa Kiarabu waliokuwa wakitawala visiwa hivyo wakati huo. Kisiwa cha Zanzibar kilikuwa lango la kuenea kwa Ukristo Afrika Mashariki na Kati.

Wakristo wa kwanza kufika huko mwaka huo wa 1499 ni Wamonaki Waagustino kutoka Ureno. Baadae walifukuzwa na waarabu mwaka 1698. Kufukuzwa kwao, kukawa chanzo cha kufika baadae Wakapuchini mwaka 1857 na wakakaa kipindi kifupi.

Tangu hapo, Zanzibar pamoja na kuwa na watu wenye imani na dini toafuti tofauti, imani kubwa mbili visiwani humo ni Uislamu na Ukristo. Waislamu wakiwa wengi zaidi kuliko watu wa imani nyingine, kutokana na imani hiyo kuingia visiwani humo miaka 800 kabla ya imani nyingine.

Jumapili iliyopita, Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, liliadhimisha miaka 150 ya Imani Endelevu Katoliki jimboni humo. Maadhimisho hayo yalifanyika huku viongozi wa kanisa hilo wakishindwa kuvumilia kuelezea uvumilivu wa kiimani uliokuwepo karne kadhaa nchini humo. Pia walilaani vikali baadhi ya watu wachache ambao wanatumia dini kama kisingizio, wanaokubali kutumika kuharibu amani visiwani humo, amani iliyodumu vizazi na vizazi, na kutaka kujenga uadui baina ya watu waungwana waliojenga udugu wa kudumu uliojenga mizizi yake katikati ya tofauti za kiimani, kikabila na hata rangi.

Viongozi wa kanisa hilo wanasema matukio yaliyotokea mwishoni mwa mwaka juzi na mapema mwaka jana ya baadhi ya viongozi wa kanisa hilo kuuawa kwa kupigwa risasi, kujeruhiwa na wengine wa Kiislamu akiwemo shehe kumwagiwa tindikali, yalikusudiwa kuvuruga udugu uliodumu kwa amani karne na karne.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili kuhusu maadhimisho hayo ya miaka 150 endelevu ya kiimani Zanzibar, Maaskofu hao wa Kanisa wanasema kwa miaka mingi, imani kubwa mbili visiwani humo (Uislamu na Ukikristo) zimekuwa chachu na tunu ya amani na kuchangia ustawi wa maisha ya watu ya kiroho na kimwili lakini mwishoni mwa mwaka 2012 na mapema mwaka 2013 uvumilivu uliingiliwa.

Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao anasema tangu Ukristo uingie Zanzibar katika karne ya 15 kabla ya kurejea tena miaka 150 iliyopita, kumekuwa na uvumilivu wa kiimani lakini Kanisa la kipindi hiki cha sasa limo katika nyakati za kutindikiwa kwa uvumilivu huo.

“Haikuwa hivi tangu awali, sasa tumekosa uvumilivu wa kuishi pamoja kwa tofauti za imani zetu, kuona wenye imani nyingine walio wachache hawana haki, lazima katika jumuiya ya wengi wawepo watu wasiojali utu, sisi ni Watanzania lazima tuishi pamoja, makabila, dini na rangi zetu ni viunganishi na tunu,” anasema Askofu Shao na kuongeza;

“Hakuna dini ya Taifa, changamoto tunazoziona miaka hii tunaziweka katika sehemu ya kutojua kwamba hakutakaa kuwe na dini ya Taifa, kumkubali mwenzako pamoja na tofauti zake za kiimani, kabila na itikadi za kisiasa inapaswa kuwa utajiri na tunu ya pekee kwetu,” anasema alipoelezea changamoto za Kanisa visiwani Zanzibar kuelekea kilele cha maadhimisho hayo.

Askofu Shao anasema, hakuna dini visiwani humo inayoagiza wala kutoa amri ya kutenda mabaya, bali watu wachache katika jamii walioamua kwa matakwa yao kutumiwa, iwe kwa kutaka fedha ama vinginevyo, kutengeneza chuki na kuvuruga amani, ambao hawana budi kusaidiwa kutoka katika tamaa za fujo zilizojaza mioyo yao tofauti na maagizo ya imani zao.

Katika Ibada ya Misa siku hiyo ya Jumapili, msisitizo wa viongozi hao katika mahubiri ulikuwa amani, upendo, mshikamano na uvumilivu wa tofauti za watu. Msingi huu ambao Serikali imekuwa ikiusisitiza unaelezwa kuwa chachu ya maendeleo na tunu pekee ya amani visiwani humo hivyo waungwana hawapo tayari kuona inasambaratishwa na wachache.

Askofu Shao ambaye ni Askofu wa pili Mtanzania tangu Zanzibar kufanywa Jimbo mwaka 1980, anasema shukrani hiyo kwa Mungu ililenga uvumilivu wa kiimani uliodumu miaka hiyo yote endelevu ya kiimani visiwani humo na ilishirikisha maaskofu wa majimbo yote 33 Tanzania Bara, makasisi, watawa wa kike na wa kiume na waumini kwa ujumla.

Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Method Kilaini anasema wapo watu wachache wanaokubali kutumiwa na watu wa nje ya nchi kuharibu tunu ya udugu na uvumilivu wa kiimani iliyopo nchini hivyo hawapaswi kuendelea kupata nafasi hiyo.

“Udugu ulikuwa mkubwa Zanzibar lakini msukosuko ukaingia hivi karibuni baada ya watu wachache, wengi wao wakiwa vijana wakarubuniwa kwa fedha kwa kutaka maisha rahisi na kufanya vitendo vibaya na vya kinyama na hali sasa ni mbaya,” anaisema Askofu Kilaini na kuongeza;

“Waislamu wa Zanzibar ni watu wazuri, ingawa ni wengi kuliko Wakristo kwa kuwa waliingia Zanzibar miaka 800 kabla ya Wakristo lakini walionesha kuvumiliana, wapo watu wachache wanafuata mkumbo kutoka nje na si Zanzibar, huu ni wakati kwa Waislamu, Wakristo na Serikali tuwe kitu kimoja kukomesha hali hii”.

Askofu Shao anasema hali ya usalama visiwani humo kwa sasa inatia moyo, wana uhakika wa usalama kwa kuwa ni ahadi endelevu ya Serikali tangu yalipotokea matukio ya kuhatarisha amani kwao na kwa jamii nzima.

Matukio hayo ni pamoja na mauaji ya Padri Evarist Mushi, Februari mwaka jana na kujeruhiwa kwa risasi Padri Ambrose Mkenda, Desemba mwaka juzi. Pia Katibu wa Mufti, Shehe Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.

Matukio hayo pia yaliwakuta viongozi wa serikali ambapo Sheha wa Tumondo Mohamed Omary Said naye alijeruhiwa kwa kumwagiwa tindikali huku watalii wawili raia wa kigeni nao wakikumbwa na janga hilo.

“Tuna uhakika wa usalama kwa kuwa ni ahadi endelevu ya serikali walisema kwamba hawataruhusu yatokee yaliotokea, tunaona amani inarejea na tuna imani na hilo kwa kuwa hata uongozi umepanguliwa katika Polisi, ni matumaini yetu ulinzi utaimarishwa,” anasisitiza Askofu Shao.

Shao aliteuliwa kuwa Askofu wa Zanzibar Aprili 27 mwaka 1997, miezi michache baada ya aliyekuwa Askofu wa kwanza Bernard Ngaviliau kumaliza muda wake. Ngaviliau alisimamia kanisa la Zanzibar kabla halijawa Jimbo naye akiwa kasisi tu tangu mwaka 1973 hadi 1980 lilipofanywa Jimbo nae kuwa Askofu.

Kabla yake alikuwepo Padri Adrian Mkoba (1968-1973) baadae alikuwa Askofu wa Morogoro na alilipokea kanisa kutoka kwa Padri Joseph Spendi aliyelisimamia tangu mwaka 1968 hadi 1973.

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi