loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

UWIANO WA KIJINSIA na staha ya wabunge wanawake

Hawa si wengine, bali ni wanawake 255 wanaoshiriki Bunge Maalumu. Hoja waliyoibeba, si nyingine, bali ni kuhakikisha Katiba ijayo inatamka wazi uwiano wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 katika nyadhifa mbalimbali za uongozi. Wanawake hao hawamaanishi uwiano huo kuishia kwenye viti vya bungeni.

Bali wanataka Katiba mpya itakapoandikwa, kuanzia mwakani, uwiano huo uwe ni kwa wigo mpana katika maeneo tofauti. Mikakati ya kufanikisha hilo, iliwekwa wazi hivi karibuni katika semina iliyoandaliwa maalumu kwa wajumbe wanawake wanaoshiriki Bunge hilo maalumu, mjini Dodoma. Wanaamini sauti ya wanawake 255 waliomo kwenye Bunge hilo lenye wajumbe 629, haitapotea.

Wanaamini tamko rasmi la Umoja wa Afrika (AU) kuhusu uwiano wa 50 kwa 50 ambalo Tanzania imeridhia, litatekelezwa kwa vitendo na Serikali baada ya Katiba mpya kupatikana. Katika kuhakikisha wanakwenda na sauti ya pamoja, kupitia semina hiyo iliyoandaliwa na Tanzania Women Cross Party Platform (TWCP), wamepigwa msasa.

Profesa Ruth Meena kutoka Mtandao wa Wanawake na Katiba, anaainisha mapengo yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba kuhusu haki za wanawake. Anawaambia wajumbe hao wanawake wanapaswa kuyapatia majibu kwenye Bunge Maalumu ili yaingizwe kwenye Katiba.

Profesa Meena anasema ingawaje Rasimu ya Pili ya Katiba imekiri kwamba binadamu wote huzaliwa huru na sawa, usawa huo haukuainishwa kama lengo kuu wala tunu mojawapo ya taifa. “Kutokana na pengo hili, usawa wa jinsia haukutumika kama kigezo mojawapo cha uchaguzi wa uongozi katika sehemu mbalimbali za utawala, vyombo vya uchaguzi na vile vya uwajibikaji,” anasema Profesa Meena.

Anasema Rais akiwa na madaraka makubwa sana ya kuteua viongozi mbalimbali hawajibiki kuzingatia kanuni ya usawa wa jinsia. Pia anasema vyama vya siasa haviwajibishwi kuzingatia msingi huo. “Kwa mantiki hii, Rasimu haikuzingatia tamko rasmi la AU kuhusu 50 kwa 50 ambalo Serikali yetu imeridhia,” anasema Profesa Meena.

Anatoa mfano wa nchi ambazo suala la usawa wa jinsia limewekwa sawa kwenye dibaji za katiba zao. Mojawapo ni Misri ambayo inatamka ‘taifa lisiloheshimu utu wa mwanamke haliwezi kuwa na utu kwani wanawake ni dada na wadau wa wanaume katika mafanikio na katika uwajibikaji.’

Kwa upande wa Malawi, anasema inadhamiria kushughulikia ustawi wa jamii na maendeleo ya watu kuweka sera na mipango endelevu na sheria kuhakikisha usawa wa jinsia. Mfano mwingine aliotoa ni Rwanda ambayo dibaji yake inasema, “tumedhamiria kujenga jamii kwa kuzingatia haki sawa kwa Wanyarwanda wote, wanawake kwa wanaume…”.

Katika uchambuzi yakinifu wa Rasimu ya pili ya Katiba, kwa mtazamo wa wanawake, Profesa Meena anaainisha mapengo mengine yaliyomo kwenye sura mbalimbali za Rasimu. Anatoa mfano wa sura ya 7 ya Rasimu ya Katiba akisema, uteuzi wa uongozi wa juu wa Jamhuri ya Muungano pamoja na mihimili mikuu ya utawala, haukujikita katika msingi wa usawa wa jinsia kama ilivyoanishwa na tamko la AU la 50 kwa 50.

Hivyo Profesa Meena anataka wajumbe hao wanawake waende na sauti ya pamoja kuhakikisha uwiano wa asilimia 50 kwa 50 unakuwa katika uteuzi wa Baraza la Mawaziri na manaibu na makatibu wakuu. Nafasi nyingine ni wakurugenzi na manaibu, msajili wa vyama vya siasa, uongozi wa vyombo vya uwajibikaji ikiwa ni pamoja na Tume ya Maadili ya viongozi, Tume ya Haki za Binadamu na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Pia anahimiza vyama vya siasa viwajibishwe kuzingatia usawa wa kijinsia katika uongozi. Hata hivyo, kufanikisha malengo hayo ya kushawishi katiba ije na majibu hayo ya usawa wa kijinsia, wanawake wanaoshiriki Bunge Maalumu wanapewa angalizo. Nalo ni kuhusu dhana nzima ya kujiheshimu na staha mbele ya jamii.

Angalizo hilo linatolewa na Spika Anne Makinda wakati akifungua semina hiyo. Katika kufunda wanawake hao wa rika tofauti waliomo bungeni, Makinda anasema ushawishi wao utatokana na namna wanavyojiheshimu. Anahadharisha dhidi ya vitendo vinavyoweza kuwavunjia heshima.

Makinda ambaye hiki ni kipindi chake cha nane akiwa bungeni, anatoboa siri ya kukaa bungeni kipindi kirefu. Anasema yeye pamoja na wabunge wengine wanawake, wamefanikiwa katika hilo kutokana na kujiheshimu. Mbunge mwingine aliyekaa bungeni kwa vipindi vinane, ni Anna Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake.

“Niliingia mdogo, kama wadogo wengine hapa, lakini nilijiheshimu… Ukijiheshimu unachokisema watakuamini,” anasema Makinda akihadharisha wajumbe hao dhidi ya Ukimwi na vitendo vinavyoweza kuwavunjia heshima ikiwemo, ulevi. Spika anasema kitendo cha wanawake kutojiheshimu na hatimaye kutoa mwanya wa kuandikwa kwenye magazeti ya udaku, ni miongoni mwa mambo yanayoathiri ushinikizaji wa hoja ya usawa wa kijinsia.

Makinda anatoa mfano kwamba yuko mbunge (hakumtaja) alikuwa akichangia hoja ambayo ilikuwa nzuri, lakini kutokana na matendo yake, haikuthaminiwa zaidi ya kumbeza. “Alipozungumza, aliambiwa hayo maneno akamwambie fulani; wakimaanisha aliye kwenye uhusiano naye…tukiwa na nidhamu sisi, hoja zetu zitakubalika,” anasisitiza.

Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake Tanzania, Anna Abdallah anaunga mkono angalizo hilo la Makinda. Anasisitiza kwamba mwanamke kutunza heshima yake, ndiyo ustawi wake. Katika kusisitiza nafasi ya wajumbe hao kuhakikisha hoja kuhusu jinsia zinapata mashiko katika katiba, Abdallah anahimiza pamoja na staha, wanawake wanapaswa kuwa na umoja na kupendana.

Profesa Meena pia anahimiza dhana nzima ya heshima kwa mwanamke akisema, “tutaweza kuwasuta wanaotudhihaki kama tutajiheshimu kama ambavyo Mama Makinda amesema.” “Ninyi ni wachache lakini mnaonekana. Kuonekana kwenu kutakuwepo kama hoja zenu zitajikita katika mambo ya msingi,” Profesa Meena anaendelea kuwafunda.

Hata hivyo Profesa Meena anasema Wanawake wa Mtandao wa Katiba sanjari na hao wanaoshiriki Bunge Maalumu, wanapaswa kuendelea kutetea na kupigania haki za msingi za kikatiba katika mchakato huo wa kihistoria. “Tutalinda yale mafanikio tuliyopata ili yasiondolewe wakati wa Bunge la Katiba na tutaendelea kudai msingi wa usawa uwekwe kwenye malengo na tunu za taifa,” anasema.

Anahimiza wanawake kuipa ridhaa Katiba iwapo itatamka kwamba Katiba ni mali ya Watanzania; wanawake kwa wanaume. Anasisitiza wajumbe kutosahau kusimama imara kupaza sauti uwiano wa kijinsia asilimia 50 kwa 50 uingizwe kwenye Katiba na utekelezeke katika maeneo mbalimbali.

TANZANIA imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi