loader
Dstv Habarileo  Mobile
Uyoga chanzo cha lishe bora, tiba, kipato

Uyoga chanzo cha lishe bora, tiba, kipato

Chama cha Wazalishaji Uyoga cha Dar es Salaam, (DMGA) kinasema kwamba uyoga umegawanyika katika makundi makuu matatu; kundi la kwanza likiwa la uyoga-taka (saprophyetes). Kinafafanua kwamba uyoga huu hupata virutubisho vyake kutoka kwenye miti mikavu na masalia ya mazao ya kilimo.

Aina nyingine kwa mujibu wa DMGA ni uyoga tegemezi (parasites) ambao hupata virutubisho vyake kutokana na mimea na wanyama hai na huweza kusababisha uharibifu mkubwa wa mimea na wanyama hao. Uyoga ufaano (symbionts) ni aina nyingine ambayo DMGA wanasema hupata virutubisho vyake kutokana na mimea na wanyama wanaoishi karibu nao bila kuleta madhara.

Huu pia ni uyoga unaoishi kwa kutegemeana. DMGA wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Judith Muro wanasema uyoga ni mmea mkavu ambao hauwezi kujitengenezea chakula, lakini hutoa vimeng’enyo vinavyosaidia kuyeyusha mabaki ya mimea au wanyama ili kujipatia chakula.

Uyoga huweza kuota wenyewe porini au kuoteshwa kitaalamu na matumizi ya uyoga kwa binadamu ni pamoja na lishe na tiba. Uyoga una vitamini lishe B, C na D, madini ya fosfarasi, chumvi, potasiam na chokaa na pia una protini kwa wingi kiasi cha wastani wa asilimia 10 hadi 49.

Mbali na wingi wa vitamini lishe, pia uyoga ni tiba inayosaidia kuimarika kwa kinga za mwili na kudhibiti magonjwa kutokana na kuwa na viinilishe vingi.

“Zipo aina mbalimbali za dawa kwa mtindo wa vidoge, maji na sindano zinazotengenezwa kutokana na uyoga,” anasema Muro. “Dawa hizo zinaweza kutibu au kuzuia magonjwa ya kifua kikuu, kusukari, moyo, shinikizo la damu, figo, saratani mbalimbali, vidonda vya tumbo na lehemu,” anasema.

Kutokana na umuhimu wa uyoga kuwa lishe na tiba kwa binadamu Juni 28, mwaka huu Chama cha Wazalishaji Uyoga cha Dar es Salaam kilifanya maonesho ya uyoga kwa vikundi vya wakulima wa zao hilo katika Shule ya Sekondari Mongola, iliyopo Kata ya Mzumbe, wilayani Mvomero, Morogoro.

Vikundi vya wakulima wa uyoga kutoka Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro na Kijiji cha Vigenge, Kata ya Mzumbe, vilishiriki kwa kuonesha bidhaa zitokanazo na uyoga na mapishi. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa DMGA, Judith Muro, vikundi vya akinamama vimekuwa na hamasa kubwa zaidi hasa baada ya kutambua kuwa uyoga unaweza kuwa chanzo cha mapato kwa familia na hivyo kuwa njia mojawapo ya kupunguza umasikini.

“Uyoga ni rafiki wa mazingira kwa kuwa unatumia makapi ya viwandani na mashambani ambayo yangeweza kuwa kero kwa jamii. “Baada ya kuvuna uyoga mabaki yake hutumika kurutubisha ardhi na kuua minyoo ya ardhini inayoshambulia mazao kama nyanya na migomba,” anaelezea Muro.

Anasema uyoga unaweza kuwa ajira kwa vijana pia wazee na unafaa pia kuwa kilimo cha wenye kipato kidogo mijini kwa kuwa hauhitaji eneo kubwa la kuzalishia. Anasema kwa kutambua umuhimu wa uyoga, Mwenyekiti huyo anaiomba Serikali hasa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika iliingize zao la uyoga kwenye mfumo wa kuendeleza mazao muhimu na lipatiwe rasilimali watu na fedha katika kuliendeleza.

“Bado uzalishaji wa mbegu bora za uyoga nchini hautoshelezi na uzalishaji wake haujaingizwa kwenye mfumo wa kudhibiti mbegu ili wakulima wapate mbegu bora. Ombi letu kwa serikali ni zao hili kuingizwa kwenye mfumo wa kuendeleza mazao nchini,” anabainisha. Kwa upande wake, mkulima wa uyoga wa Kijiji cha Vigenge, Kata ya Mzumbe, Janeth Mbwambo, anasema tangu ameanza kushiriki kilimo cha uyoga, kimempatia mafanikio makubwa ya kiuchumi.

Mbwambo ambaye ni Ofisa Ugani katika Kijiji hicho anasema ameotesha uyoga katika banda lenye urefu wa mita nne kwa mita tano. “Uyoga unaniingizia fedha kuanzia Sh milioni nne hadi nane kwa kipindi cha miezi mitatu ya uzalishaji. Fedha hizi zinanisaidia kuboresha maisha na familia yangu,” anasema Ofisa Ugani huyo.

Naye mkulima mwingine wa uyoga, Maria Shindika, anasema licha ya kuwepo kwa soko la zao hilo, bado wakulima wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mbegu, hali inayowafanya waoteshe kwenye maeneo madogo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Anthony Mtaka, ambaye alikuwa mgeni rasmi siku ya maonesho ya uyoga, anakitaka chama hicho kuweka mfumo utakaowaunganisha wakulima wa zao hilo wa mikoa yote nchini ili kuongeza uzalishaji utakaotosheleza soko la ndani na nje.

Mkuu wa Wilaya anasema, hatua hiyo itakuwa ni kuendeleza juhudi zilizokuwa zimeanzishwa na Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, marehemu Mzee Rashid Mfaume Kawawa. Anasema Mzee Kawawa, baada ya kustaafu alikijita katika kilimo cha uyoga hapa nchini na kuwa mhamasishaji mkuu wa zao hilo.

Hata hivyo anasema huko nyuma uyoga ulikuwa unaliwa na wale waliokuwa na utamaduni wa kuufahamu hususan ule wa msituni na wale waliokuwa wakitembelea hoteli kubwa hususan wapenzi wa supu ya uyoga.

“Kupitia siku hii ya maonesho ya uyoga, jamii inaweza kupata fursa ya kujifunza na kufahamu faida na matumizi ya uyoga katika mwili wa binadamu,” anasema Mkuu huyo wa Wilaya ya Mvomero. Anaongeza: “Historia ya kilimo cha uyoga inaonesha kuwa ina zaidi kidogo ya miaka 10 hivyo hapa ninaona kuna baadhi yetu tunahitaji kuweka nguvu zaidi katika kuendeleza zao hili.

Anasema kwamba tangu Mzee Kawawa afariki dunia kasi ya kuhamasisha kilimo cha uyoga nchini imeshuka na kwamba kutokana na umuhimu wake jamii inapaswa kufufua juhudi zilizoanzishwa na Mzee Kawawa. “Mzee Kawawa alikuwa ni kiungo muhimu katika uendelezaji wa zao la uyoga. Chama hiki kwa sasa kifanye kazi aliyoanzisha huyu mzee wetu kabla ya kifo chake kama njia ya kumuenzi pia,” anasisitiza Mtaka.

Mtaka pia anakishauri chama hicho kuelekeza nguvu zake katika kufundisha zaidi juu ya ujasiriamali wakulima wote na si wa uyoga pekee pamoja na kusimamia uzalishaji bora wa zao hilo. Anasema chama hicho kinapaswa kuwa na mtandao ikiwa ni pamoja na kuchukua jukumu la kuwatafutia wakulima masoko ya uhakika, hususan katika hoteli kubwa na maduka makubwa maarufu kama supermarkets.

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi